Na Munir Shemweta, WANMM
Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete
ametembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mvua iliyoambatana na
upepo kwenye jimbo la Chalinze mkoani Pwani na kutoa pole kwa wote
walioathirika na mvua hizo.
Usiku
wa kuamkia Januari 20, 2022 ilinyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo
mkali kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam
ambapo katika jimbo la Chalinze mkoa Pwani takriban nyumba 36 zikiwemo
shule mbili za msingi za Makombe na Bwilingu ziliathirika.
Naibu
Waziri wa Ardhi Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze
Jumamosi ya Januari 22, 2022 alitembelea familia za waathirika pamoja
na shule mbili za msingi ambazo mapaa yake yaliezuliwa na mvua hizo.
Akiwa
katika kijiji cha Makombe kilichopo kata ya Lugoba, Chalinze mkoani
Pwani, Ridhiwani alijionea athari iliyosababishwa na mvua hizo ambapo
aliwafariji waathirika na kuwaeleza kuwa, yeye kama mbunge kwa
kushirikiana na Halmashauri ya Chalinze wataangalia namna ya kuwasadia
wale walioathirika na kadhia hiyo ili waweze kurudi katika maisha yao ya
kawaida.
“Binafsi
yangu nieleze nimesikitishwa na janga lililotokea lakini wakati
mwingine tuamini kila jambo limepangwa na Mwenyezi Mungu na lina sababu
zake nyingi,”amesema Ridhiwani.
Akiekezea
uharibifu uliotokea kwenye shule ya Msingi Makombe, Ridhiwani ameagiza
kufanyika jitihada za haraka ili kuyarejesha madarasa yaliyoathirika
kurudi katika hali yake ya kawaida ili wanafunzi waweze kuyatumia kwa
kuwa tayari shule zimefunguliwa.
“Binafasi
namshukuru Mungu kwa sababu katika taarifa yenu hatukupata taarifa ya
mtu aliyeumizwa kwa sababu wakati mwingine inapotokea wanafunzi wako
darasani inakuwa ni hatari sana na kushukuru chama kwa kutoa kipaumbele
kwa maisha ya watu,"amesema Ridhiwani.
Katika
kinachoonekana kuunga mkono hatua zinazofanyika kutokana na kadhia
iliyotokea kwa madarasa ya shule, Mbunge huyo wa Jimbo la Chalinze
mkoani Pwani alitoa kiasi cha shilingi milioni 5 ili kusaidia
kurekebisha sehemu zilizopata athari ya mvua ili wanafunzi waweze
kuendelea na masomo.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhani Possi alimueleza Naibu Waziri
Ridhiwani kuwa, mvua iliyonesha mbali na kuezua mapaa ya takriban nyumba
36 lakini mvua hiyo pia ilileta athari kwa shule mbili za msingi za
Makombe na Bwilingu A.
Hata
hivyo, alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, ofisi yake ilianza
kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya tathmini ya uharibifu
uliotolea shule ya msingi Makombe na kuahidi ndani ya wiki moja madarasa
kuanza kutumika.
“Kule
katika kijiji cja Makombe tatizo ni kubwa zaidi ambapo hatua tumeanza
kuchukua kama Halmashauri na leo mbunge ametuongezea nguvu, katika
gharama ya milioni 26 anatuongezea milioni 5 na hela ikiingia itasaidia
zaidi,”amesema Possi.
Kwa
upande wake Diwani wa Bwilingu Nasser Karama alieleza kuwa, mvua
iliyonesha imeleta athari kwa baadhi ya wananchi wa kitongoji cha
Bwilingu pamoja na shule ya msingi Bwilingu ‘A’ ambapo baadhi ya
wananchi wamepata hifadhi na kusaidiwa vyakula na wadau mbalimbali.
Hata
hivyo, alikishukuru Chama cha Mapinduzi pamoja na Mbunge wa jimbo la
Chalinze kwa kuchukua hatua za haraka mara baada ya kupata taarifa ya
kutokea kwa maafa hayo ambapo alisema hatua hiyo imewafariji sana.
“Mie
katika kata yangu nimeathirika hili darasa moja na nyumba ya mwalimu
pamoja na madarasa yaliyochakaa ila tumepata tumaini baada ya
kutembelewa na mbunge na mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze,”amesema
Karama.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mbunge wa Chalinze, Pwani Ridhiwani Kikwete akimsikiliza mmoja wa
waathirika wa maafa ya mvua (aliyevaa kilemba) katika kijiji cha
Makombe.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇