Mwanamuziki Nguli wa Congo-DCR Hayati Generali Defao
Dar es Salaam
Muziki wa Rhumba umepata pigo baada ya aliyekuwa mtunzi na mtumbuizaji mkongwe wa Muziki wa Dansi Afrika na mashuhuri Duniani Le Jenerali Defao Matumona kufariki Dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Laquintinie, mjini Douala nchini Cameroun akiwa na umri wa miaka 62 kuelekea kutimiza miaka 63.
Le Jenerali Defao aliyezaliwa Disemba 31,1958, katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo-DRC), amefariki ikiwa bado siku 3 tu kabla ya siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake (Birthday) yaani Disemba 31, 2021.
Hakika kifo cha Defao, kinakumbusha maneno ya muimbaji Hassan Bitchuka katika wimbo maarufu wa Bendi ya Mlimani Park Orchestra (Sikinde) uitwao 'Huruma kwa Wagonjwa' ambapo katika wimbo huo, kuna maneno yasemayo "Nani kauona Mwaka, ni Majaliwa yake Mungu kuuona mwaka", Maana amefariki ikiwa bado siku 4 tu auone mwaka mpya wa 2022.
Siku ya Sikukuu ya Krismas, Disemba 25, 2021 nchini Tanzania kulifanyika onesho kubwa la kihistoria ambalo linajulikana kama 'usiku wa Rhumba kali', onyesho hili liliwakutanisha wakongwe mbalimbali wa muziki wa dansi hapa nchini na kulingana na mipango ya awali ya waandaaji wa onyeso hilo, kulikua na mikakati ya kuwakutanisha wakongwe wa Tanzania na wakongwe wenzao waliopata umaarufu mkubwa duniani wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika wanamuziki waliopendekezwa na waratibu hao jina la Defao lilikua mojawapo ambapo mwezi Novemba 2021, mmoja wa waratibu wa Onyesho la Usiku wa Rhumba Kali aliongea moja kwa moja kwa simu na Jenerali Defao kwa ajili ya kumualika kuwa mmoja wa wanamuziki wageni mashuhuri wa Kimataifa katika Onyesho hilo nchini Tanzania.
Defao alikubali mwaliko huo na kuahidi yuko tayari kuhudhuria bila kuhitaji malipo yoyote bali gharama za kujikimu tu watakazopanga waandaaji. "Watanzania ni rafiki zangu, nitakuja kuimba pamoja na ninyi nitaimba Sala Noki, Kolza na Abdallah" alisema Defao kwa mmoja wa waratibu onyesho hilo aliyewasiliana nae kumpa mwaliko.
Defao kwa shauku aliahidi kuwa tayari kuja kuhudhuria na alikua tayari kujirekodi video ya kuhamasisha onesho hilo na kuituma kwa ajili ya kuirusha mitandaoni ili kupromoti onesho, hakutoa masharti magumu kwa waandaaji maana alihitaji vitu viwili tu, uhakika wa usafiri (Tiketi ya kuja na kurudi) na uhakika wa malazi kabla na baada ya onyesho.
Bahati mbaya Kamati ilijaribu kuona baadhi ya wadau ili wasaidie lakini kutokana na muda kuwa mfupi haikuweza kufanikiwa kupata wadhamini au wadau ambao wangeweza kulipia tiketi na gharama kidogo za kujikimu yeye binafsi kwani malazi haikua shida kwa kuwa Hoteli ya Nefaland ambayo ndio palipangwa kufanyika onesho hilo palikua panafaa yeye kufikia.
Hivyo, kutokana na kukosekana bajeti, Kamati ililazimika kuondoa mpango wa kumleta Defao ili kuja kuungana na wakongwe wa Tanzania kunogesha onyesho hilo. Kwa lugha nyingine, endapo Waratibu wangefanikiwa kupata tiketi basi Defao asingeenda Cameroun na kufia huko, bila shaka Juzi Disemba 25, 2021 ambayo ilikuwa pia Sikukuu ya Krismas, angetumbuiza pamoja na kina Tshimanga Assosa, Nguza Vicking na Komandoo Hamza Kalala.
Ndio kusema kuwa kama Jenerali Defao angefanikiwa kuja Tanzania na kushiriki onyesho hilo Nefaland Hotel basi kifo chake kama Mungu alishapanga afe jana kingetokea hapa Tanzania akiwa ameshatumbuiza hapa Tanania katika Onyesho hilo la Usiku wa Rhumba Kali.
Ingawa Defao hakufanikiwa kuja alikua akisubiri kutumiwa 'clips' za video za tukio hilo. Kamati ilikua inasubiri mkanda uliorekodiwa ili kuchagua picha za kumtumia, Hata hivyo, apangalo binadamu Mola huweza kulipangua, Defao hakuweza kuiona video ya Onyesho hilo na amefariki kabla ya onyesho lijalo la 'Usiku wa Rhumba Kali' ambalo kutokana na ahadi yake aliahidi kushiriki.
Defao amefariki ikiwa ni siku 3 tu kabla ya siku ya kusherehekea kuzaliwa kwake (Birthday) na pia ilisalia siku nne tu kuuona mwaka mwaka 2022, kifo hiki knafikirisha sana na kusadifu maneno ya hekima ya muimbaji Hassan Rehani Bitchuka katika wimbo maarufu wa bendi ya Mlimani Park Orchestra (Sikinde) uitwao Huruma kwa Wagonjwa”.
Wimbo huu, mbali ya kuhadharisha kwa tanbihi nzito kuwa ni majaaliwa yake Mwenyezi Mungu kuuona mwaka mwingine, unafingirisha kipopo cha fikara. Na ndivyo ilivyotokea kwa Le Jenerali Defao, hakujaaliwa kuuona mwaka. Isingekua kudra za Mwenyezi Mungu isingemshinda Defao kupita siku tatu na kuuona mwaka mpya wa 2021. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu pia ndiye mwenye uamuzi wa mja afie wapi.
Bahati mbaya Kamati ilijaribu kuona baadhi ya wadau ili wasaidie lakini kutokana na muda kuwa mfupi haikuweza kufanikiwa kupata wadhamini au wadau ambao wangeweza kulipia tiketi na gharama kidogo za kujikimu yeye binafsi kwani malazi haikua shida kwa kuwa Hoteli ya Nefaland ambayo ndio palipangwa kufanyika onesho hilo palikua panafaa yeye kufikia.
Imeandikwa na Sir. Katanga na Kuhaririwa na Bashir Nkoromo, Msimamizi Mkuu wa Blog hii ya Taifa ya CCM
(Itaendelea Part 2)
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇