LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 7, 2021

MBUNGE KILAVE AJA NA MKAKATI WA KUJENGWA VYUMBA VYA MADARASA VYA GHOROFA KATIKA KATA ZENYE UHABA WA MAENEO JIMBO LA TEMEKE

Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dorothy Kilave akizungumza Wajumbe wa Kamati ya Siasa na Watendaji wa Kata ya Sandali, leo. Katikati ni Diwani wa Sandali Christopher Kabalika na Kulia ni Katibu wa CCM wa Kata hiyo Willey Mwatandika.


Na Bashir Nkoromo, CCM Blog, Temeke
Mbunge wa Temeke Jijini Dar es Salaam Dorothy Kilave,  ameibua mkakati mbadala wa kujengwa vyumba vya madarasa vya ghorofa katika Kata zenye uhaba wa maeneo katika jimbo hilo, ili kuepuka kukosa fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mifuko ya Serikali ukiwemo wa fedha za Uviko 19.

Mkakati mwingine ambao Mbunge Kilave ameibuka nao, ni Viongozi wa katika Kata zenye uhaba huo wa maeneo kutafuta yanayomilikiwa na Taasisi za umma yaliyopo katika Kata zao na kuyaomba kupitia Mamlaka zinazohusika ili yatumike kujengwa shule au vituo vya Afya kupitia fedha hizo zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.

Aidha, Mkakati mwingine ambao ameupendekeza Mbunge Kilave ni wa kutafuta  majengo yanayomilikiwa na watu au taaisisi za Umma na kuomba kuyavunja kwa kuyalipia fidia, ili kupata nafasi hizo za kujengwa Shule, Zahanati au Vituo vya Afya.

Mbunge Kilave ameeleza mikakati hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungunguza na Wajumbe wa
Kamati za Siasa na Watendaji wa Kata, alipokuwa katika ziara za kukagua Miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Kata mbali mbali jimboni kwake.

Akiwa katika ziara hizo alizozianza mwezi uliopita, amewaambia Viongozi hao kwamba baadhi ya Kata wamekosa fedha hadi sh, milioni 200 walizokuwa wametengewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Shule au Vutuo vya Afya baada ya kuonekana  Kata hizo hazina maeneo ya kujengwa shule au vituo hivyo vya Afya.

"Unaona ninyi hapa Sandali mlikuwa mmepangiwa kupata fedha za kujenga vyumba 10 vya madarasa ambavyo kila moja kingegharimu sh. milioni 20, lakini ikaonekana hamna eneo la kujengwa vyumba hivyo, fedha zikarudishwa, maana yake ni kwamba kama maeneo yangekuwepo hapa mngepata sh. milioni 200", alisema Mbunge Kilave alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Siasa na Watendaji wa Kata hiyo ya Sandali, leo.

"Kwa hiyo pamoja na changamoto zingine naomba ndugu viongozi tutafute namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili kwa lengo la kuifanya Sandali yetu iendelee", akasema Mbunge Kilave na kuungwa mkono na Diwani wa Kata hiyo
Christopher Kabalika ambaye pia alishiriki kikao hicho, kilichofanyika katika Ofisi ya CCM Kata hiyo ya Sandali.

Kwa upande wake Mbunge Kilave aliazimia kwamba sasa watakapokuwa wanaomba fedha, wawe wanaomba kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa vya ghorofa ili kukidhi ufinyu wa maeneo.

Nao wajumbe wote waliunga mkono azimio hilo, huku baadhi yao wakitaja maeneo ambayo wanadhani serikali ikiombwa Kata inaweza kupewa ikayatumia kujenga shule yenye hadhi bora.

Katika Mjadala huo Diwani Kabalika, tayari ameshaanza mchakato wa kuiomba CCM ili kuvunjwa Ofisi yake Kata hiyo ya Sandali kwa fidia, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Kituo cha Afya na kwamba kwa upande wake CCM imesharidhia na kinasubiriwa sasa ni kupatikana fedha kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Katika kikao hicho Mbali na Changamoto ya Elimu na Afya, Mbunge Kilave na wajumbe walijadili pia changamoto zingine kadhaa ikiwemo zinazohusu miundombinu na mikopo kwa wananchi wa Kata hiyo ya Sandali.

Mapema Mbunge Kilave alianza leo ziara yake katika Kata ya Keko ambako alikagua ujenzi wa chumba cha darasa kinachojengwa katika shule ya Sekondari Keko kwa gharama ya sh. milioni 20. Kuona Picha za Ziara ya Mbunge Kilave Kata za Mbagala na Sandali, Bofya👉 HAPA

1 comment:

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages