LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 20, 2021

WAZIRI MKENDA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUZALISHA MBOLEA CHA FOMI JIJINI BUJUMBURA-BURUNDI

 

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide akikagua mbolea mbadala ya kukuzia aina ya Fomi Imbura wakati alipotembelea na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha FOMI Ndg Ntirampeba Simion kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM Mjini Bujumbura nchini Burundi wakati akitoa maelezo kuhusu umuhimu wa mbolea mbadala ya kukuzia aina ya Fomi Imbura, tarehe 19 Octoba 2021.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide akipokelewa na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo chini ya kampuni ya ITRACOM mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Burundi.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi akitoa taarifa ya Balozi kwa Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ubalozi nchini Burundi wakati wa ziara ya kikazi ya waziri ya siku mbili Mjini Bujumbura, tarehe 19 Octoba 2021. 
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mjini Bujumbura nchini Burundi.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza akizungumza na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi wakati alipotembelea Ubalozini ili kujionea utendaji kazi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wote, tarehe 19 Octoba 2021.
 

Na Mathias Canal, Wizara
ya Kilimo, Bujumbura-Burundi

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 19 Octoba 2021 ametembelea
na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho
kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini
Dodoma nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo Waziri Mkenda pamoja na wataalamu mbalimbali
aliombatana nao amekagua kiwanda cha FOMI na kuona kinavyofanya kazi ikia ni
lengo la kuona uwezekano wa kiwanda hicho kama kinaweza kuuza mbolea yake
Tanzania kwa bei nafuu kwa wakulima na kupatikana kwa wingi na kwa wakati.

Prof Mkenda amesema kuwa kiwanda hicho nchini Burundi
kinazalisha Tani kati ya 120,000 mpaka Tani 150,000 kwa mwaka kulingana na soko
la mbolea huku kikiwa kimeanza ujenzi wa kiwanda cha kisasa Jijini Dodoma nchini
Tanzania ambapo kitapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za
mbolea ambazo ni zaidi ya mahitaji ya mbolea nchini Tanzania ambayo ni kati ya
Tani 400,000 mpaka Tani 500,000 kwa mwaka.

 

Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa
kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania vilevile inaendelea na mkakati wa
kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia
wakulima kwa bei nafuu.

Waziri Mkenda amemuhakikishia Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw
Ntirampeba Simon kuwa serikali ya Tanzania itakuwa bega kwa bega kuhakikisha
kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.

“Wawekezaji wote wanaowekeza kwenye biashara ya Pembejeo
Tanzania tunawahakikishia kuwa Tanzania ni nchi salama kwa uwekezaji hivyo wajitokeze
kwa wingi kwa ajili ya kuwekeza” Amekaririwa Waziri Mkenda

 

Kwa upande wake Waziri wa Mazingira, Kilimo
na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide amesema kuwa
mazungumzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yameongeza wigo mpana Zaidi kwa
kubadilishana mawazo katika sekta ya kilimo.

 

Dkt Rurema amesisitiza
kuwa katika muktadha wa kuongeza uzalishaji na tija katika mazao ya kilimo kuna
mambo muhimu mawili ya kuzingatia ambayo ni maji, ardhi na mbolea na katika
nchi ya Burundi sekta ya mbolea imeimarika na uzalishaji unatosheleza mahitaji
ya wakulima,

Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Mbolea cha FOMI kilichopo
chini ya kampuni ya ITRACOM Bw Ntirampeba Simon amesema kuwa Menejimenti ya
kiwanda hicho imeendelea kufurahishwa sana kwa ushirikiano unaoonyesha wa
viongozi wakuu wa Tanzania kwa kutembelea Burundi mara kwa mara hususani
kukitambua na kukithamini kiwanda hicho.

Amesema kuwa mbolea inayozalishwa kiwanda hapo ni nzuri na
inayohimili hali yoyote ya hewa na ardhi kwa mujibu wa utafiti walioufanya.

Awali Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda amekutana na kufanya
mazungumzo na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi ambapo amewapongeza
kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya huku akiwasihi kuhakikisha kuwa
wanaendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw
Salvatory Mbilinyi amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa Ubalozi unaendelea kuwa
kiungo muhimu katika juhudi za serikali ya Tanzania za kuhakikisha Burundi kama
nchi jirani inaendelea kuwa na Amani.

Ameongeza kuwa, ubalozi unatekeleza Diplomasia ya uchumi kwa
kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, kutangaza fursa za
kiuchumi zilizopo Burundi ambazo watanzania wanaweza kunufaika nazo, kutafuta
masoko ya mazao ya kilimo pamoja na bidhaa za viwandani za Tanzania, kutangaza
vivutio vya utalii vya Tanzania na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano
mbalimbali baina ya Tanzania na Burundi yenye maslahi kwa nchi zote mbili.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages