LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 20, 2021

CHUO CHA MAENDELEO YA WANANCHI KISARAWE KUANZA KUJENGWA NOVEMBA 2021

 


 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (katikati) akikagua eneo kitakapojengwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe, mkoani Pwani. Mhe. Kipanga ameambatana na uongozi wa Wilaya ya Kisarawe.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson John (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (kushoto) wakati alipotembelea eneo kitakapojengwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe.

 

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (katikati) akifafanua jambo wakati alipokuwa akikagua eneo kitakapojengwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe, mkoani Pwani.

 ……………………………………………………………

Na WyEST

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga ametembelea kukagua eneo kitakapojengwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe lililopo Kata ya Mzenga Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuanza Novemba 2021.

Akiwa hapo ameelezea kufurahishwa na jitihada zilizofanywa na Uongozi wa Wilaya ya Kisarawe za kuwashirikisha wananchi wa Kata ya Mzenga katika kusafisha eneo la ujenzi kwa gharama ya Shilingi milioni 3 kutoka milioni 26 iliyotajwa awali.

Aidha, Mhe. Kipanga amewataka wasimamizi wa ujenzi kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha mradi unatekelezeka kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati.

“Mradi huu ni wetu sote na chuo hiki kitatoa elimu kwa watoto wetu wa eneo hili, hivyo niwaombe wote mshirikiane kuhakikisha mradi unatekelezwa vizuri ili matokeo yanayotarajiwa yaweze kufikiwa,” amesema Mhe. Kipanga.

Akitoa taarifa ya Mradi huo, Mshauri Elekezi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha, Nestory Robert amesema awamu ya kwanza ya ujenzi wa chuo hicho utahusisha majengo 11 yatakayogharimu Shilingi bilioni 1.04 na utakamilika ndani ya miezi sita.

Ameyataja majengo hayo kuwa ni jengo la Utawala, madarasa, karakana 3, bwalo la chakula, vyoo, mabweni 2 yenye uwezo wa kuchukua wanachuo 160, nyumba ya mkuu wa chuo pamoja na nyumba 2 za watumishi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisarawe, Joseph Mugeta amesema chuo hicho kwa sasa kinatumia majengo ya Kanisa la KKKT yaliyopo Kisarawe mjini.

Amesema chuo chake kwa sasa kina jumla ya wanachuo 518 kati yao 232 ni wa kozi fupi. Amezitaja kozi zinazotolewa chuoni hapo kuwa ni ufundi magari, ushonaji, upishi, uchomeleaji vyuma na uwashi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages