LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 12, 2021

WAFUNGWA 69 WANAOSUBIRI KUNYONGWA WAOMBA HURUMA YA RAIS

 Na Mwandishi Maalum, Tabora
Wafungwa 69 ambao wamehukumiwa adhabu ya  kunyongwa  , wamemwomba  Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania, awapunguzie adhabu ya  kunyongwa na kuwapatia adhabu mbadala.

Wafungwa hao ambao wapo katika Gereza Kuu la Uyui Mkoani  Tabora, wametoa ombi lao hilo kupitia risala yao waliyoisoma mbele ya  Makatibu wakuu watatu wakiongozwa na Katibu Mkuu , Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa  Sifuni Mchome  waliofika  Gerezani hapo kuzungumza na  Uongozi wa Gereza , mahabusu na wafungwa.

Akisoma  risala hiyo  kwa niaba ya wafungwa wenzake waliohukumiwa  kunyongwa,  mfungwa kiongozi No 143/2012 Masali Misalaba, wafungwa hao wamesema, wanaomba  huruma ya  Mhe. Rais awabadilishie adhabu hiyo na kupewa  adhabu mbadala ili nao waweze kufanya kazi kama ilivyo kwa wafungwa wengine.

“Mhe. Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria,  kwanza, tunashukuru sana kwa kututembelea wewe na ujumbe wako,  sisi wafungwa ambao tumehukumiwa kunyongwa,  tunakuomba utufikishie ombi letu kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan  atuonee huruma   na atupunguzie adhabu hii  ili nasi  tuweze kufanya kazi, kwa kweli tunawakati mgumu na tunawasumbua sana  askari magereza  tunaomba sana utufikishie ombi letu kwa Mhe. Rais.” akasema Mfungwa Kiongozi kwa niaba ya wenzake.

Wafungwa hao ambao wamehukuhimiwa kunyongwa hadi  kufa, walipewa nafasi na uongozi wa Gereza Kuu  la  Uyui kujumuika na   mahabusu na wafungwa wenzao  katika kikao hicho ambacho walipata fursa ya kuelezea changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Wafungwa hao waliohukumiwa adhabu ya  kunyongwa walikuwa wamevalia  sare  yao ya rangi ya blue, wenye umri tofauti wengine ni wazee ambao walisaidiwa  kutembea na wafungwa wenzao, wengine wlionekana  wamevaa rosali zao shingoni au wameshika tasbihi mikononi, wengine hata walikuwa  na  biblia,  walikuwa  ni wasafi na nyuso zenye matumaini licha ya kwamba walikuwa wamehukumiwa  adhabu ya kifo.

Pamoja na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa kuomba huruma ya Rais.  Mahabusu na  wafungwa wengine nao walitoa yao ya moyoni mbele ya Makatibu Wakuu hao  ambao ni nadara sana  kutokea kwamba Makatibu Wakuu watatu kutoka  Wizara  Tofauti lakini majukumu  yao yanaingiliana katika masuala ya utoaji  haki jinai na haki madai wakawa na ziara ya pamoja.
Katika  risala yao,  iliyosomwa kwa  niaba yao na  Mfungwa   Enock Ezekiel Kakamba, wameiomba  serikali  kuangalia upya  utaratibu wa  msamaha wa wafungwa unaotolewa na Rais.

Wamependekeza kwamba  wigo wa msamaha unaotolewa na Rais upanuliwe zaidi na kuwahusisha pia wafungwa ambao  wametumiki  vifungo virefu vya zaidi ya miaka  kumi.

“Mhe. Katibu Mkuu, tunaomba kwamba,  msamaha wa Rais  ikiwezekana  uhusishe pia wafungwa ambao wameshatumikia  vifungo vyao kwa zaidi ya miaka kumi na kuonyesha tabia njema, tunaomba hivi kwa sababu  msamaha ambao umekuwa ukitolewa kwa wafungwa  ambao hawajatumikia vifungo vyao kwa muda mrefu,  wakishaachiwa  baada ya muda mfupi wanarejea tena magerezani kwa sababu muda waliokaa  wanakuwa  hawajajifunza chochote tofauti na mfungwa ambaye ametumikia zaidi ya miaka 10 huyu  akipata msamaha hawezi tena kurudi kwenye  uhalifu kwa sababu tayari ameshajifunza na hatatamani kurudi tena  gerezani”

 Vile vile mahabusu hao wameomba kushughulikiwa kwa  suala la uchelewesheaji wa upelelezi,  uchelewaji wa kutolewa kwa nakala ya  hukumu kwa wakati,  uchache  wa viakao  maalaum vya mahakama kuu na mahakama ya rufani hasa kwa kesi za mauaji na kesi za uhujumu uchumi.

Pia wafungwa  na mahabusu wao wameomba sheria ya Parole  inagaliwe upya ili  iweze kuwa na wigo mpana  tofauti na ulivyo hivi sasa ambapo ina wigo mfinyu katika  makosa na muda. Kutokana na kwamba ni makosa machache sana yanayokubalika  wa parole na muda wa kuwa na sifa ya kupendekezwa kwenye Parole ni  mrefu sana ambao ni 1/3 ya kifungo.

Akijibu  ombi la wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, Katibu Mkuu, Profesa Mchome, amesema atalifikisha ombi hilo kwa mamlaka  zinazohusika.

Kabla ya  kuzungumza na mahabusu na wafungwa, Makatibu  wakuu hao pamoja na ujumbe walioongoza nao  walipata fursa ya kuonja au kula chakula  ambacho kilikuwa kimeandaliwa kwaajili ya mahababusu na wafungwa .

Kwa mujibu wa  Mkuu wa Gereza Kuu la Uyui ACP Mussa Said Mkisi,  Gereza la Uyui ambalo limejengwa mwaka  1946 linauwezo  wa kupokea  wafungwa na mahabusu wa kiume kutoka mikoa ya jirani,  na vile vile kupokea wafungwa kutoka  Magereza Makuu  kama vile  Butimba – Mwanza, Isanga- Dodoma, Maweni-Tanga na Ukonga Dare es Salaam.

 Hadi wakati Makatibu Wakuu  hao wanatembelea  Gereza hilo,  kulikuwa na wafungwa na  mahabusu  767. Idadi hiyo ikijumuisha wahalifu ambao  si raia wa Tanzania  kutoka nchi za  Burundi,   Kongo ( DRC)  na Ethiopia.

Mkuu wa Gereza hilo ACP Mussa Saidi Mkisi amewaambia  Makatibu wakuu hao ingawa msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza hilo ni wawastani,  lakini changamoto  hiyo bado  kutokana na ongezeko la  watu na uhalifu nchini  licha ya kwamba Mahakama imekuwa ikijitahidi kusikiliza kesi za mahabusu na wafungwa.

“ Gereza lina msongano wa wastani wa wahalifu kwani hadu leo ( jumatatu) tunao  wahalifu 767 wakati uwezo wa Gereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 650  ziada ni wahalifu 117 sawa na  asilimia 18” akaeleza   Mkuu wa Gereza ACP Mussa Saidi Mkisi.

Katika taarifa yake,   Mkuu wa Magereza  alielezea changamoto nyingine  kuwa ni    ukosefu wa magodoro na mablanketi kwa ajili ya mahabusu na wafungwa,  uchache wa  maafisa na askari magereza. Na wadau wa hakijinai na baadhi ya wananchi  kutokuwa na  elimu ya kutosha kuhusu adhabu mbadala.

Makatibu Wakuu Profesa Sifuni Mchome, ( Wizara ya Katiba na Sheria) John Jingu( Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) na   Christopher Kadio ( Mambo  ya Ndani) wapo katika ziara ya  kujifunza na kufanya tathimini kuhusu  mnyororo wa utoaji haki jinai na haki madai katika mikoa    ya  Tabora,  Kigoma  na  Kagera.

Wakiwa  mkoani Tabora   pamoja na kutembelea Gereza Kuu la Uyui lakini pia wamekuwa na  vikao mbalimbali na wadau wanaohusika  na suala zima la utoaji haki, wakiwamo Mahakama,  Magereza, Polisi,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa  Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na  Ustawi wa Jamii.
 
Makatibu Wakuu Sifuni Mchome, John JIngu na Christopher Kadio wakiwa nje  ya  Gereza  Kuu la Uyui lililopo Mkoani  Tabora mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo  yao  na  Viongozi wa  Gereza, wafungwa na  Mahabusu. Katika mazungumzo hayo na   na mahabusu na wafungwa, wafungwa  waliohukumiwa kuyongwa  wamemwomba Mhe. Rais awaonee huruma

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages