LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 7, 2021

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI DK. FELESHI AHIMIZA USHIRIKIANO JUMUISHI WA TAASISI TATU, ASEMA ZINABEBA TASWIRA YA NCHI

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi, ametoa rai kuwa Taasisi za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni lazima zifanyekazi kama timu moja kwa kuwa Taasisi hizo zinabeba taswira ya Nchi.

Rai hiyo ameutoa katika mkutano wake na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Evaristo Longopa,  Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Boniphace Luhende, Kaimu Naibu Mwendesha Mashtaka Neema Mwenda na  Wakurugenzi wa Idara za Mipango za Taasisi hizo tatu, uliofanyika leo Jumatano, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.

“Taasisi hizi zinabeba taswira ya nchi, rai yangu kwenu ningependa kuona tunafanya kazi kama timu moja, tunakuwa na ushirikiano jumuishi bila ya kuathiri majukumu lengwa ya Kitaasisi kwa mujibu wa miundo ya Taasisi, kwa sababu wote tunaitumika Serikali moja, Serikali  ambayo ipo tayari kutusaidia   katika utekelezaji wa Majukumu  yetu”. Amesema Dk. Feleshi.

Dk. Feleshi amesema kutokana na sababu hiyo, ndiyo maana ameamua kuitisha kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine, amewapa watendaji wa Taasisi hizo, jukumu la kuandaa mchanganuo na mapendekezo ya kina ya maeneo ambayo yatajengewa hoja za kuomba kuongezewa bajeti katika mwaka wa fedha 2022/2023.
 
Dk. Feleshi amebainisha kuwa, ikiwa ni miaka minne sasa tangu maboresho ya mwisho yaliyofanywa na Serikali mwaka 2018, ambayo yaliyowezesha kuundwa kwa Taasisi hizo tatu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu. bado  lengo la maboresho hayo halijaweza kufikiwa kutokana na Taasisi hizo kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo la ufinyu wa bajeti.

Amesema ameshakutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Mwendesha Mshtaka Mkuu, na Wakili Mkuu wa Serikali na katika mazungumzo yao yapo mambo ambayo wamekubaliana kuyafanyia kazi.
 
“Nipo katika kujifunza, leo nimewaita nyinyi kwa sababu ndiyo maafisa mahsusi ili kwa  pamoja tujadiliane na kubadilishana mawazo ya namna Taasisi hizi tatu zitaweza kuandaa bajeti zenye uhalisia na zinazozungumza kulingana na ukubwa wa majukumu yetu na changamoto tunazokabiliana nazo ”. Akasema Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali.

Amesisitiza kwamba, kila  Taasisi  iandae mchanganuo wake na mapendekezo kwa kuzingatia vipaumbele vyake muhimu na ambavyo ni halisia.

Hata hivyo amekiri kwamba, Serikali haiwezi kufanya kila kinachoombwa katika bajeti inayoombwa na Taasisi, lakini kubwa na la muhimu ni kuandaa bajeti yenye uhalisia na zitakazoifanya Taasisi hizo kuendesha shughuli zake kwa weledi na kwa kuzingatia hadhi  na taswira ya nchi.

Pamoja na changamoto kubwa ya ufinyu wa Bajeti unaozikabili Taasisi hizo tatu, pia zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hususani mawakili wa serikali na wa kada nyingi ambapo kwa upande wa mawakili hao wa serikali peke yake kuna upungufu wa mawakili zaidi ya 4,303 katika Taasisi zote tatu.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho wamemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuitisha kikao hicho  muhimu ambapo pia kimeweza kuwapatia fursa ya kufahamu maono  yake, vipaumbele vyake na mwelekeo wa mbeleni wa Taasisi hizo. Na kuahidi  kwamba, watakwenda kuyafanyika  kazi maagizo na maelekezo yake kwa wakati.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi akiongoza kikao kilichowahusisha Manaibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wakurugenzi wa Idara za Mipango  za Ofisi hizo tatu. kikao  kilifanyika leo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.(Na Mpigapicha Maalum).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages