LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 15, 2021

MATOKEO YA UTAFITI WA TARI:MICHIKICHI ALIYOSHIRIKI KUPANDA WAZIRI MKUU MAJALIWA KUANZA KUVUNWA DESEMBA 2021

 Mkuu wa Gereza Kwitanga lililopo Mkoani Kigoma Kamishna Msaidizi wa Magereza Dkt Uswege Mwakahesya akiwaonyesha Mkurugenzi wa Uhaulishaji Teknolojia wa TARI Dkt Juliana Mwakasendo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Kihinga Dkt. Filson Kagimbo mikungu ya chikichi aina ya TENERA kutoka kwenye mchikichi uliopandwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.


Mkurugenzi wa Uhaulishaji Teknolojia wa TARI Dkt. Juliana Mwakasendo  akishuhudia matokeo ya mchikichi wa TENERA uliopandwa na kutoa matunda ya kwanza kwa kipindi kilichotarajiwa kulingana na utafiti uliofanywa na TARI.


Mti ukionesha uzao wa kwanza wa mchikichi aina ya TENERA uliopandwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa  katika shamba la gereza Kwitanga mkoani Kigoma.




Na.  Evelyne Mpasha – TARI Kigoma

Mchikichi aina ya TENERA uliofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)  na kupandwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika shamba la gereza Kwitanga Halmashauri ya Wilaya ya kigoma, Mkoani Kigoma mwezi Februari, 2019 umeanza kuzaa ikiashiria ubora wa mbegu hiyo kukomaa kwa kipindi kifupi.

Akizungumza na waandishi wa habari na Watendaji wa TARI waliotembelea shamba hilo,  Mkuu wa gereza la Kwitanga Kamishna Msaidizi wa Magereza Dkt. Uswege Mwakahesya alieleza kuwa kuzaa kwa mchikichi huo ni ishara tosha kuwa utafiti uliofanywa na TARI umezaa matunda yaliyotarajiwa  kwa muda muafaka.

Dkt. Mwakahesya aliongeza kuwa miche hiyo iliyopandwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa upandaji michikichi bora Mkoani Kigoma  inatarajiwa kuanza kuvunwa mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu 2021.

“Nawapongeza sana TARI kwa matokeo haya ya utafiti ambayo yanaonesha uhalisia. Nawashauri wananchi wachangamkie fursa hii, miche ipo ya kutosha na inatolewa bure kwa wakulima kwa kufuata taratibu” alisema Dkt. Mwakahesya.

Akizungumzia hali ya uendelezaji wa zao hilo, Dkt. Mwakahesya alieleza kuwa Kitalu cha gereza Kwitanga kina jumla ya miche 324,812 ambapo kati ya miche hiyo, 220,315 iko tayari kupelekwa shambani wakati wowote kuanzia mwezi huu wa Oktoba, miche 62,675 ni midogo na inatarajiwa kupandwa shambani kuanzia mwezi Februari, 2022 huku miche 23,775 imepandwa katika shamba lenye ekari 475. 

Aidha, Miche 18,22 imesambazwa kwa wadau mbalimbali ambao ni  Wilaya ya Buhigwe, Gereza la Kimbiji  Dar es Salam na Gereza la Kalilankulukulu lililopo Mpanda Katavi.

Michikichi aina ya TENERA ambayo hukomaa kwa muda mfupi (miaka 2 na nusu – 3) ina uwezo wa kuzalisha tani 4-5 za mafuta ya kula ya mawese kwa hekta moja  tofauti na mbegu ya asili (jiwe) ambayo hutoa mafuta  tani 1.6 kwa hekta na pia huchukua muda   wa miaka 7 -10 kabla ya kuanza kukamuliwa mafuta.

Katika moja ya mikutano yake, Mheshimiwa Majaliwa aliwahi kueleza kuwa Serikali imeamua kufufua zao hilo la michikichi ili kuondokana na uagizaji wa mafuta ya kula nchini ambapo nchi hutumia tani 640,000 za mafuta ya kula kila mwaka ilihali uwezo wa kuzalisha nchini ni tani 240,000  na kwamba tani 400,000  zinaagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu Serikali kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 470 (takribani nusu tirioni)  kila mwaka.

Mheshimiwa Majaliwa amekuwa mhamasishaji mkubwa wa zao la michikichichi ili kukabiliana na uhaba wa mafuta ya kula  nchini na amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara mkoani Kigoma kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za TENERA kwa wingi na kuwataka wananchi kuachana na mbegu za asili ambazo uzalishaji wake wa mafuta ni mdogo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano wa TARI  Dkt. Juliana Mwakasendo alieleza kuwa ili kukamilisha mche mmoja wa mchikichi kuanzia kuuchavusha hadi kumfikia mkulima Serikali inatumia zaidi ya  shilingi 10,000, ila kwa sasa miche hiyo  inagaiwa bure na Serikali hivyo wakulima wanapaswa  kuchangamkia fursa hiyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TARI Kituo cha Kihinga Dkt. Filson Kagimbo  alieleza kuwa Kituo chake mpaka hivi  sasa kimeshazalisha zaidi ya mbegu  milioni 7 za TENERA na kuzisambaza katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma na Halmashauri nyingine 11 nje ya Mkoa wa Kigoma ambazo ni Mkuranga, Kisarawe, Tanganyika, Ngara, Urambo, Kyela, Nkasi, Sumbawanga, Ndarambo, Nyasa na  Mrimba.  Aidha, katika kuhakikisha upandaji na utunzaji wa mbegu hizo, Kituo cha TARI Kihinga kinaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima na maafisa ugani.

Dkt. Kagimbo aliongeza kuwa licha ya kutoa mafunzo TARI imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu utunzaji wa miche hiyo na maendeleo yake kwa wakulima na Halmashauri.

Shamba la Gereza Kwitanga ambalo ni shamba mahiri kwa zao la michikichi lilizinduliwa rasmi mwaka 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kuwa kituo cha uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za michikichi aina ya TANERA.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages