Na CCM Blog, Tegeta.
Jumapili mbili zilizopita Kanisa Halisi la Mungu Baba, lenye Makao yake Makuu Tegeta jijini Dar es Salaam, lilifanya Ibada kubwa mbili zilizowalenga Wanajamii walio ndani na nje ya ufuasi wa Kanisa hilo kwa lengo la kuwainua na kuwabariki ili waweze kufanya shughuli au kazi zao za uzalishaji kwa haki na faida zaidi.
Ibada ya kwanza ilikuwa ya kubariki waandishi wa Habari ambapo kwenye ibada hiyo zaidi ya Waandishi wa habari na watagazaji zaidi ya 50 kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini hususan Jijini Dar es Salaam walihudhuria.
Iliyofuata ilikuwa ni Ibada ya kufuta ajali hasa kwa waendesha pikipiki za kupakia abiria maarufu Bodaboda ambapo zaidi ya waendesha Bodaboda zaidi ya 45 waliitikia mwaliko na kuhudhuria kwenye Ibada hiyo.
Kwa Jumla Ibada hizo zilisisimua mno kwa kuwa Waandishi wa habari na Bodaboda baadaye walilipongeza Kanisa Halisi la Mungu Baba, kwa namna Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, Baba Halisi alivyoziendesha kiasi cha kuacha amewatia matumaini mapya.
Katika mwendelezo wa Ibada zinazohusisha Wanajamii hadi walio nje ya Uzao (Waumini) wa Kanaisa hilo, sasa ni zamu ya Mama na Baba Lishe, ambapo Kanisa Halisi limeandaa Ibada mahsusi kwa ajili yao ambayo itafanyika keshokutwa Jumapili, Oktoba 31, 2021 (19 ELULI, VOL.2), Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta.
Tayari Kanisa hilo limeshatoa Mwaliko kwa Mama na Baba Lishe mbalimbali popote walipo ili kuhudhuria Ibada hiyo, Mwaliko huo ambao Baba Halisi ameusambaza unaujumbe mzito kutoka kwenye Maandiko Matakatifu wenye maneno haya; "Nanyi mtakula chakula tele na kushiba na kumhimidi Chanzo Halisi, Mungu Wenu".
Baba Halisi ameuandika Mwaliko huo, kama ifuatavyo;
Tafadhali, Usome Hapo
👇
Mama/Baba lishe kazi yao ni kulisha watu bila kujali itikadi zao. Uwe Mwislamu, Mkristo, Mbudha au Muhindu unakula tu kwa Mama/Baba lishe bila shida yoyote. Ni kweli unalipa kwanza ndipo uhudumiwe, lakini pia nikweli kwamba hakuna anayeweza kutafuna nakula noti au sarafu.
MUNGU BABA, ambayeni CHANZO CHA MEMA NA MAZURI peke yake yuko hivyo. Anatupatia mvua na uhai bila kujali dini, dhehebu la mtu wala itikadi.Maana katika Efeso 4:6 anasema kuwa yeye ni Mmoja na ni Baba wa wote, aliye ndani ya yote na katika yote.
Wakati wa Majira ya Mwana, kulikuwa na mafundisho ya Imani na Tumaini (bila upendo) ambayo yalisababisha tuchukiane bila sababu za msingi. Maana katika 1 Korintho 13:13, kitabu kinasema kuna Imani, Tumaini na Upendo na katika hayo matatu lililo kuu ni Upendo. Hivyo, alichokuja nacho CHANZO CHA MEMA NA MAZURI juu ya Nchi ni upendo tena uliopitiliza kwa wote.
Ili Mama/Baba lishe waendelee kupika kwa ajili ya Jamii kama nilivyotangulia kusema hatimaye tule na tushibe, inahitajika Baraka ya mvua kwa kipimo cha haki kama tunavyosoma katika Yoeli2:23-24.
Katika kipindi hiki tulichonacho wataalamu wa hali ya hewa wametangaza kuwa kutakuwa na ukame na uhaba wa chakula nchini kwa kuwa mvua za vuli zimechelewa kunyesha.
Hapa ndipo sote tunapotakiwa kumkimbilia MUNGU BABA ambaye ni CHANZO CHA MEMA NA MAZURI ili atupe mvua lakini ni kwa kipimo cha haki. Tunapaswa kutenda haki ndipo tupate Baraka za mvua yenye utoshelevu hatimaye tule na kushiba:
(1) Haki ya Kwanza ambayo tunatakiwa kuwa nayo mbele ya CHANZO HALISI, aliyekuwepo kabla ya nafsi na roho yoyote ni kumwabudu na kumsujudia yeye tu aliyetuumba kwa jinsi ya ajabu na ya kutisha (Zaburi 139:14);
(2) Hakiya Pili ambayo tunatakiwa kuwa nayo ni Kumshukuru kwa yote anayotutendea kila iitwapo leo (Yohana 6:11-13);
(3) Haki ya Tatu tunayotakiwa kuwa nayo ni kumuita kwa Moyo Mmoja kutokana na tatizo lililoko mbele yetu la Ukame na uhaba wa chakula ambao umekwishatabiriwa na wataalam (Matendo ya Mitume 4:23-24), ili tupate jibu sahihi kutoka kwake;
(4) Haki ya Nne tunayopaswa kuwa nayo ni kukusanyika tukiwa na Moyo Safi (Mathayo 5:8), yaani kuwa na upendo usio na ubaguzi kwa kuwa hakuja kutafuta dini wala dhehebu bali Uzao Halisi juu ya Nchi (Isaya52:5);
(5) Haki ya Tano tunayopaswa kuwa nayo ni unyenyekevu mbele zake (2 Nyakati7:14-16), ili tukiomba asikie na kutujibu huku jicho lake likiendelea kutuangalia kwa karibu;
(6) Haki ya Sita tunayotakiwa kuwa nayo ni kutoa fungu la kumi la mapatoyetu yote, kwa kuwa anasema katika kitabu cha Hagai 1:8-11, kuwa bila kutoa Zaka atakausha Mbingu;
(7) Haki ya Saba tunayotakiwa kuwa nayo ni kujitambua kuwa tumependelewa kuwaTaifa Baba, ikiwa na maana ya kuwa chanzo cha Baraka kwa mataifa mengine. Hii ina maana hatutakiwi kuruhusu ukame na uhaba wa chakula (Mathayo 21:43). Kwa kuwa ndivyo ilivyo, tupeleke matunda mahali alipopachagua (Kumbukumbu12:5-7)
Kanisa Halisi la MUNGU BABA, tunawakaribisha Mama/Baba lishe wote na Wananchi wote bila kubagua Lango la 19 Eluli, Vol.2 (31 Oktoba, 2021)
Ili tuinue sauti kuomba mvua inyeshe. Tukiomba wakati tuna haki, lazima tupate. Mvua itanyesha kwa kipimo cha haki, tutakula na kushiba na kuendelea na Ibada niUzalishaji bila tatizo. HERI ULIYEBARIKIWA KULIKO WOTE.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇