Sep 20, 2021

PINDA AVUNJA NGOME YA VYAMA VYA UPINZANI SHINYANGA



Waziri Mkuu Mstaafu Mhe, Mizengo Pinda, akiwapokea wanachama wa  vyama vya upinzani waliohamia CCM, kushoto ni Charles Shigino aliyekuwa Katibu wa Siasa na Uenezi kutoka NCCR Mageuzi, akifuatiwa na Emmanuel Aluta aliyekuwa Afisa utawala na fedha kutoka TLP, pamoja na aliyekuwa Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti Renatus Nzemo.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe, Mizengo Pinda akipanda mti nje ya uwanja wa CCM Kambarange mkoani Shinyanga kabla ya ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa mashindano ya kitaifa ya mpira wa miguu ya UVCCM GREEN CUP 2021 yaliyozinduliwa kitaifa mkoani Shinyanga.


Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Waziri mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati Kuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Mizengo Pinda, ameivunja ngome ya vyama vya upinzani mkoani Shinyanga baada ya vigogo watatu wa  vyama vya CHADEMA,TLP na NCCR MAGEUZI kuhamia CCM na kuusifu uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassani.

Wanachama hao waliohamia CCM ni   pamoja   na Renatus Nzemo, aliyekuwa katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti,   Emmanuel Alute,  aliyekuwa Afisa Utawala na Fedha wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na Charles Shigino, aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi NCCR Mageuzi.

Akizungumza jana mkoani humo katika hafla maalumu ya kuwapokea viongozi hao Pinda alisema kuwa uamuzi waliouchukua kujiunga na CCM ni wakizalendo na hawatojutia maamuzi yao kutokana na chama hicho kuwa na sera nzuri zenye mrengo wa kuwaletea wananchi maendeleo.

“Wenzetu wameona kukaa upinzani hakuna tija  wameamua wao wenyewe kujiunga CCM,hatuna budi kuwapokea ili tuendelee kufanya kazi ya kulijenga taifa letu kwa pamoja,wapeni ushirikiano wa kutosha,”alisema Pinda.

Awali akizungumza katika hafla hiyo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa alisema kuwa  wanachama hao wapya wamefuata taratibu zote zinazohitajika ndani ya chama hicho ikiwa ni Pamoja na kurejesha kadi za vyama vyao vya awali na kupatiwa kadi mpya.

“Wenzetu hawa baada ya kusikia ujio wako katika mkoa wetu waliomba wewe kurudi CCM na mzee Pinda uwezekuwapokea baada ya kuridhika na uongozi wa awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani,”alisema Mlolwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, aliyekuwa katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti, Renatus Nzemo alisema kuwa uamuzi wake wa kurudi CCM umechagizwa na uongozi wa mama Samia,kwa kutatua hoja walizokuwa wanazipigania kipidi kile wakiwa upinzani.

“Nimeamua kurudi nyumbani kwa sababu kumenoga,nimekuwa upinzani kwa muda mrefu,nimetafakari kwa kina mimi na familia yangu nikaona nibora nihamie CCM kwani sisi hoja tulizokuwa tunazipambania zote Rais Samia ameshazitekeleza,”alisema Nzemo.

Nae Charles Shigino, aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi NCCR Mageuzi,alisema kuwa vyama vya upinzani kwa sasa vimekosa hoja na badala yake vimekuwa vikihimiza wananchi kutotekeleza maagizo ya serikali ikiwa ni Pamoja na kuhamasisha maandamano yasiyokuwa na tija kwa taifa.

“Nimeamua kuacha siasa zisizo na tija kwa nchi yangu,nimerudi nyumbani kumuungamkono Rais wangu katika ujenzi wa nchi yangu,huwezi kupata dola kwa kuendelea kubedha mazuri yanayotekelezwa na mtangulizi wako,”alisema Shigino.

Kwa Upande wake Emmanuel Alute,  aliyekuwa Afisa Utawala na Fedha wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) alisema kuwa Rais Samia ametatua kero mbalimbali katika sekta za afya,elimu,maji,umeme na miundombunu ya barabara hali ambayo imeudhoofisha upinzani na kubakia na siasa za chuki ambazo hana tija kwa taifa letu.

“Rai Samia amepandisha madaraja watumishi wa umma,amefuta tozo kandamizi zaidi ya 200 kwa wafanyabiashara,gharama za kuunganisha umeme zimepungua,machinga wametengewa maeneo ya kufanyia biashara na wawekezaji wa nje ya nchi wanaendelea kuja nchini ,sasa mimi kama kijana kwanini nisimuunge mkono kwa kuhamia CCM,”alisema Alute.

Hafla hiyo ilienda sambamba na ufunguzi wa mashindano ya UVCCM GREEN CUP 2021 yaliyozinduliwa kitaifa mkoani shinyanga.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages