Na Dismas Lyassa, Kibaha
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) wameendelea kutoa raha kwa wananchi wa Mtaa wa Mkombozi, Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kuweka makaravati katika baadhi ya maeneo korofi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu katika Serikali ya Mtaa wa Mkombozi, Hassan Kuliganya maarufu Mwendokasi anasema azma ni kuhakikisha maeneo korofi yanashughulikiwa ili kuwawezesha wananchi kupita bila karaha.
“Wameanza na makaravati matatu, lakini tunaamini wataendelea zaidi,” anasema Kuliganya.
Hivi karibuni TARURA walitengeneza baadhi ya barabara za mitaa katika mtaa huo ambao kimsingi ni mtaa mpya uliopatikana baada ya kugawanywa kwa Mtaa wa Kidimu. Mtaa wa Mkombozi unasumbuliwa na changamoto nyingi ikiwamo barabara zake nyingi kutofunguliwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu, hivyo kuwa kero kwa wananchi hasa wakati wa mvua.
Wananchi wa Mtaa wa Mkombozi pia wanasumbuliwa na maji, kiasi kwamba wengine wao wanatumia maji ya mto mpiji kunywa ingawa sio salama kwa matumizi.
“Tunafurahishwa na umeme unasambaa vizuri, japo wengine bado hawajapa, lakini tunaomba wenzetu wa DAWASCO watuangalie kwa jicho la tofauti kwani kwa kweli maji ni shida kubwa mno kwetu, watuwekee hata sehemu za kuuzia kama haiwezekani kupata bajeti ya kusambaza mabomba kila nyumba,” anasema mwananchi mmoja wa mtaa huo.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇