Mbunge agaragara ardhini kwa furaha mbele ya Lubinga
Na Jacqueline Liana, Nyasa
MBUNGE wa Nyasa, Injinia Stella Manyanya, amegaragara ardhini, akitekeleza mila na desturi za Wanyasa, akimshukuru Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga kwa kufanya ziara ya kikazi wilayani humo, Septemba 19-20, 2021.
Katika ziara hiyo, Kanali mstaafu Lubinga, alikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nyasa na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Nambila.
Pia, alishiriki vikao vya shina, katika shina namba nne, tawi la Kilosa na shina namba tatu, katika tawi la Liuli.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa CCM, viongozi na watumishi wa serikali, Kanali Lubinga alipongeza jitihada za wananchi kujiletea maendeleo.
Alisema Nyasa ya leo siyo ya miaka ya nyuma, na kutoa mfano kwamba zamani kulikuwa na nyumba duni zilizoezekwa kwa nyasi, lakini sasa zimejengwa kwa matofali imara na kuezekwa kwa mabati.
"Hongereni sana wana-Nyasa, nimefurahi kwa kazi nzuri mnazofanya za kujiletea maendeleo, nimepita kote huko sijaona nyumba ya nyasi, na mbili nilizoziona nimeambiwa ni za kutambikia," alisema Kanali mstaafu Lubinga na kusababisha kicheko.
Kuhusu utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2020-2025, kongozi huyo wa chama alisema mabilioni ya fedha yanayopelekwa wilayani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zisipofanyiwa ubadhirifu, maendeleo makubwa yatapatikana nchini kwa kipindi kifupi.
Kanali mstaafu Lubinga, alionyesha kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji katika utumishi wa umma, kukwapua fedha za umma kwa masilahi binafsi, huku wananchi wakitaabika kwa kukosa huduma nzuri; zikiwemo za afya, maji na elimu.
Alitaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa mara moja dhidi ya mtumishi yoyote wa umma atakayebainika kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
"Mkuu wa wilaya, TAKUKURU, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatoa fedha nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maendeleo, nawaagiza kuzisimamia ili zilete matokeo yanayotarajiwa," alibainisha Kanali mstaafu Lubinga.
Alisema kwamba kwa waumini wa dini, mtumishi wa umma kutokuwajibika kulingana na vigezo vya ajira yake ni dhambi.
"Wewe usidhani dhambi ni kutamani tu mke wa mtu, tena hiyo inaweza kuwa na madhara kwa wachache, hebu fikiria daktari asipowajika, mwalimu asipowajibika, nesi asipowajibika, ndege ipo angani halafu hawajibiki, si watu watakufa!," alisema Lubinga na kuongeza;
"Watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo ni lazima na siyo ombi, si wewe mwenyewe uliandika barua ya maombi ya kazi na kuandika wako mtiifu, sasa wajibika."
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, akiwasalimu wananchi wa Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, alipowasili wilayani humo, Septemba 19, mwaka huu, kwa ziara ya kikazi ya kukagua uhai wa CCM ngazi ya shina, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 na kuhamasisha wananchi kushiriki katika sensa itakayofanyika mwakani. (Picha na Jacqueline Liana).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇