LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 22, 2021

HOTUBA YA MAKAMU WA RAIS DK. MPANGO KATIKA UZINDUZI RASMI WA MAONYESHO YA TATU YA SIDO, KASULU MKOANI KIGOMA, LEO


JAMHURIYA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA MAKAMU WA RAIS


HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP ISDOR MPANGO, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI UFUNGUZI WA MAONESHO YA TATU YA SHIRIKA LA KUHUDUMIA VIWANDA

VIDOGO (SIDO) KITAIFA YANAYOFANYIKA KATIKA UWANJA

WA UMOJA, WILAYA YA KASULU MKOANI KIGOMA

 

TAREHE 22 SEPTEMBA, 2021

Mheshimiwa Dkt. Kitila A. Mkumbo, (Mb.), Waziri wa Viwanda na Biashara;

Mheshimiwa Kamishna wa Polisi Thobias E. M. Andengenye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na Mwenyeji wa Maonesho ya Mwaka huu;

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira;

Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Kigoma na Waheshimiwa Wabunge wengine wote mliopo;

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa mbalimbali;

Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya mliopo;

Makatibu Tawala wa Mikoa mliopo;

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SIDO;

Mkurugenzi Mkuu wa SIDO;

Viongozi wa Vyama vya Siasa;

Viongozi wetu wa Dini;

Viongozi wa Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi;

Ndugu Washiriki wa Maonesho;

Wageni Waalikwa;

Wanahabari;

Wananchi wote wa Kasulu mliofika;

Mabibi na Mabwana;

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

 

1.            Napenda nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na fadhili kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kushiriki kwenye ufunguzi wa maonesho haya ya Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) yanayofanyika Kitaifa hapa Kasulu, katika Mkoa wetu wa Kigoma.

2.            Pili, nichukukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Uongozi wa SIDO kwa kunialika katika ufunguzi wa maonesho haya. Pia, napenda kuwapongeza waandaaji wote wa maonesho haya, hususan Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na timu yako, kwa kuratibu maandalizi haya. Napenda niwapongeze pia SIDO kwa kubuni na kuanzisha utaratibu huu wa kuwa na maonesho ya SIDO Kitaifa.  Vilevile, na kwa umuhimu wa pekee nawashukuru washiriki wote, Wajasiriamali, Makampuni, Taasisi Binafsi na za Serikali kwa kushiriki kwenye maonesho haya yaliyosheheni bidhaa za viwanda vyetu zinazozalishwa na Watanzania. Ninawashukuru pia wadhamini wote wa maonesho haya kwa jinsi walivyojitoa kuwezesha kufanikiwa kwa tukio hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.  Asante sana! kwa kutuunga mkono.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

3.            Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kujenga uchumi shindani wa viwanda na kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati cha juu.  Azma hii ya Uchumi wa Viwanda, imeelezwa vizuri katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26), ambapo Serikali imeazimia kuwa takribani asilimia 9 ya pato la Taifa litokane na viwanda ifikapo mwaka 2025/26 ukilinganisha na asilimia 8.2 kwa mwaka 2020/21. Kwa upande wa ajira, Serikali imeweka lengo la asilimia 13 ya ajira yote itokane na viwanda ifikapo 2025/26 ukilinganisha na asilimia 6.7 kwa mwaka 2020/21. Mchango wa sekta ya viwanda katika mauzo ya nje (exports) unakusudiwa ufikie asilimia 19 ukilinganisha na asilimia 17.1 ya sasa.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

4.            Nimefurahishwa na Kaulimbiu ya Maonesho haya ya SIDO ya mwaka huu inayosema Pamoja Tujenge Viwanda Kwa Uchumi na Ajira Endelevu  Kaulimbiu hii, inalenga kutambua mchango wa Sekta ya Viwanda hususan viwanda vidogo na vya kati katika kuchochea uzalishaji kwenye Sekta mbalimbali za Kiuchumi ili kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.  Ni ukweli kuwa, ili tuweze kujenga uchumi shindani, ni lazima tuwekeze katika ujenzi wa Viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini. Pia, kufanya uwekezaji kwenye Sekta zinazochangia upatikanaji wa malighafi hizo ikiwemo Sekta ya Kilimo. Tumekuwa na maneno mazuri sana katika kupamba maonesho/maadhimisho mbalimbali lakini kiuhalisia utekelezaji wake hauendani na yale tunayoyapanga ama kuyazungumza. Hivyo, natoa rai kuwa kila maonesho  yanapofanyika ni vema itolewe tathmini ya utekelezaji wa kaulimbiu husika ya kipindi/mwaka uliotangulia.

 

Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana; 

5.            Maonesho ya viwanda vidogo na vya kati yana faida na umuhimu wa pekee. Maonesho haya yanawawezesha wenye viwanda kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao na hivyo kuongeza uzalishaji na kupelekea viwanda kukua. Maonesho haya yanatoa fursa kwa wenye viwanda kubadilishana ujuzi na uzoefu na hatimaye kuboresha bidhaa kulingana na mahitaji ya walaji na soko.  Lakini pia maonesho ni fursa kwa wajasiriamali na wananchi kujionea wenyewe mashine mbalimbali, vipuri na bidhaa ambazo zinatengenezwa hapa nchini, wapi zinapatikana na kwa bei gani. Kwa sababu hizo nimefarijika kuona mmefika kwa wingi katika maonesho haya. Hii inaashiria wazi kuwa mna nia ya dhati ya kukuza masoko ya bidhaa zenu na kujifunza mambo mbalimbali kutoka miongoni mwenu na kutoka kwa wataalamu wa Taasisi zilizoshiriki. Maonesho haya yametudhihirishia kuwa si kweli kwamba kila kilicho bora lazima kiwe kimetoka nje ya nchi yetu.  Ni imani yangu kuwa wajasiriamali wetu mtatumia fursa hii ya maonesho kuzielewa na hatimaye kufanya juhudi kujipatia mashine/bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

6.            Mara tu nilipofika nimepata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda katika maonesho haya. Nimefurahia sana kujionea wabunifu mbalimbali wa teknolojia zinazoweza kutumika kwa uzalishaji viwandani.  Mathalani, nimeona wabunifu wanaojishughulisha na uzalishaji katika mnyororo wa thamani wa mazao mbalimbali ya kilimo. Napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali kuwatia moyo katika jitihada zenu. Ni matarajio yangu, kuwa SIDO mtazidi kuwahamasisha na kutoa mafunzo kwa wananchi wengi zaidi ili kuwaongezea uthubutu wa kuingia katika shughuli zinazotumia teknolojia rahisi na nafuu hususan katika uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao na bidhaa mbalimbali. Hata hivyo,  napenda kuwasisitiza mhakikishe kuwa mashine, vipuri na bidhaa mnazozizalisha, ziwe zinakidhi viwango na hata kushindana na zile zinazotoka nje lakini muhimu ziwe za gharama nafuu ili wale ambao wanaoagiza mashine, vipuri na bidhaa za kutoka nje hivi sasa wavutiwe kununua zinazozalishwa hapa hapa nchini.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

7.            Nimefurahi pia kuona bidhaa za mafuta ya kula zikiwemo za mawese, alizeti na karanga pamoja na Asali kushamiri katika maonesho haya. Kama nilivyosema hapo awali, nchi yetu inatumia fedha nyingi kuagiza bidhaa kutoka nje. Kwa mfano, kutokana na upungufu wa uzalishaji wa mafuta ya kula, nchi hutumia takribani shilingi bilioni 470 kwa mwaka kuagiza mafuta ghafi. Natoa wito kwa wananchi kuungana na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha tunaondokana na upungufu wa mafuta ya kula nchini haraka iwezekanavyo kwa kuongeza uwekezaji katika kilimo na uchakataji wa mbegu za mafuta. Nichukue fursa hii pia kuipongeza TARI na Uongozi wa Mkoa kwa ujumla kwa uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa zao la mchikichi. Natambua jitihada za TARI kuwezesha kuzalisha mbegu za kisasa za michikichi 6,645,000 na tayari mbegu 4,410,000 zimeoteshwa na ekari 6,019 zimepandwa. Na katika hili, ninampongeza sana Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha kilimo cha michikichi katika mkoa wetu wa Kigoma.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

8.            Madhumuni ya kuanzishwa kwa SIDO kama yalivyopitishwa kwa sheria namba 28 ya Bunge ya mwaka 1973 bado yana umuhimu wa pekee kwa maendeleo ya nchi.  Niwakumbushe tu, madhumuni hayo ni pamoja na:

(i)       Kushawishi, Kuhamasisha na Kusimamia uanzishwaji wa Viwanda Vidogo nchini;

(ii)     Kuongeza thamani ya rasilimali zilizoko nchini;

(iii)    Kuwezesha kutengeneza bidhaa za kutosheleza mahitaji ya wananchi;

(iv)   Kuendeleza na kutumia teknolojia rahisi inayopatikana nchini;

(v)     Kutoa kipaumbele kwa miradi ya uzalishaji inayotumia zaidi nguvukazi; na

(vi)   Kutoa huduma kwa viwanda vidogo nchini.

 

9.            Pamoja na mafanikio kadhaa yaliyoelezwa hapa ambayo SIDO wameyapata tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 48 sasa, kwa maoni yangu mchango wa viwanda vidogo katika uchumi wa Taifa bado ni mdogo! Bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vidogo hazikidhi mahitaji ya wananchi na baadhi kutokidhi viwango vya soko! Bado tunaagiza mashine ndogondogo, vipuri na bidhaa nyingi kutoka nje ambapo kama SIDO wangejipanga vizuri naamini bidhaa hizo zingekuwa zinatengenezwa hapa nchini na kukidhi mahitaji ya soko la ndani. Napata shida sana ninapoona hata panga tunaagiza kutoka nje ya nchi! SIDO mnakwama wapi? Tunazo taasisi nyingi za ufundi, utafiti na teknolojia kama DIT, TEMDO, KMT nk mnakwama wapi? Hata vifungashio jamani kwa nini tunaendelea kuagiza kutoka nje? Kwa nini tuendelee kuwatengenezea ajira nchi nyingine wakati sisi tunazihitaji?

 

10.         Nimewakumbusha hapa madhumuni ya kuanzishwa kwa SIDO, na nina hakika watanzania wangependa wajue madhumuni ya kuanzishwa kwa SIDO yametekelezwa kwa kiwango gani na tuko wapi tangu kuanzishwa kwa SIDO miaka 48 iliyopita na mwelekeo ni upi?. Kuna jitihada gani za kuinua viwanda vidogo na kuviwezesha kuzalisha bidhaa zenye kiwango kinachokidhi mahitaji ya soko la ndani na la nje?. Hivyo, ninaitaka Wizara ya Viwanda na Biashara ifanye tathmini ya kweli (candid assessment) kuhusu SIDO imefanikiwa ama imeshindwa kiasi gani katika kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake ili kuja na mapendekezo ya mikakati mipya itakayopelekea Tanzania kuweza kukidhi mahitaji ya uchumi wa kati ya mashine ndogo/za kati, vipuri, bidhaa, huduma n.k katika karne ya 21. Waziri wa Viwanda na Biashara uhakikishe na usimamie utekelezaji wa zoezi hilo na unipatie mrejesho kupitia kwa Waziri Mkuu.

 

11.         Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Uchumi wa Taifa letu unategemea na utaendelea kutegemea kilimo kwa miaka mingi ijayo.  Hivyo, SIDO na Taasisi nyingine zote (za Umma na Binafsi) zinazojihusisha na maendeleo ya viwanda na teknolojia ya viwandani, ninazitaka zifikirie na kuchukua hatua za dhati kuanzia sasa na kujiwekea malengo ya kulinyanyua Taifa katika uchakataji wa mazao ya kilimo na kuongeza thamani (agro-processing) kwa kutumia teknolojia rahisi, zikiwemo:

·        Mashine za bei nafuu za kukamua na kutakasa mafuta ya alizeti, mawese, ufuta, pamba, karanga, parachichi n.k;

·        Mashine za kusaga nafaka na kuweka kwenye mifuko, kutengeneza chakula cha samaki/mifugo/kuku n.k;

·        Mashine za mkono za kuvuna nafaka/mazao au kukamua maziwa hata chikichi na kuhifadhi maziwa/mazao;

·        Mashine za kukata na kufunga majani/kukausha chakula bora cha mifugo; na

·        Mashine za kutengeneza vifungashio, mizani nk.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

12.         Nafahamu kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo. Wakati natembelea mabanda nimeelezwa baadhi ya vikwazo vinavyopelekea wajasiliamali hawa kushindwa kupata mikopo. Vikwazo hivyo ni pamoja na kukosa dhamana zinazokubalika ambazo zimeandikishwa rasmi na kuwa na Hati. Vilevile, baadhi ya taasisi za fedha zinakopesha lakini kwa riba kubwa mno ya asilimia 18 na hata zaidi. Ni ukweli ulio wazi kuwa hatuwezi kushinda vita dhidi ya umaskini kama wajasiriamali wadogo wanaendelea kukosa mitaji ya kukuza shughuli zao. Utegemezi kwenye akiba zao wenyewe pekee hauwezi kuwawezesha kukuza uzalishaji kwa kasi itakayo waongezea motisha ya faida kukua na hivyo kupanua biashara zao zaidi na hata kuajiri wengine! Hali ilivyo sasa inawafanya wajasiliamali hawa kubaki kwenye mzingo wa umaskini. “Biashara inakuwa ndogo kwa vile mtaji ni mdogo, na mtaji ni mdogo kwa vile faida ni ndogo na akiba ni ndogo pia”!

 

13.         Napenda kutumia jukwaa hili kuzitaka Benki na Taasisi nyingine za Kifedha kubuni namna bora zaidi ya kuwawezesha wananchi wetu hawa. Aidha, ni muhimu pia huduma hizo ziende sambamba na kutoa elimu kwa Wateja hasa kuhusu ubora wa miradi, usimamizi wa miradi na matumizi adili ya Mikopo inayotolewa. Taasisi za Fedha mkiweka utaratibu mzuri wa kutoa Mikopo kwa wajasiriamali wadogo na kwa riba nafuu wanaweza kabisa kuongeza uzalishaji, ajira na Kupunguza Umaskini. Na kwa upande wa wajasiliamali wetu, hakikisheni kuwa fedha zote mnazokopeshwa zinarejeshwa kwa wakati na kwa viwango mlivyokubaliana na mabenki ili ziende tena kwenye mzunguko wa kukopa zaidi na kukopesha wengine.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

14.         Nafahamu kuwa SIDO ina Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) na pia natambua uwepo wa SANVN Viwanda Scheme ambao ni mpango wa kuwezesha wananchi kiuchumi ili wajasiriamali wadogo na wa kati kufikia wajasiriamali wakubwa kwa kuwasaidia kupata elimu, ujuzi, taarifa, mtaji na kuibua wajasiriamali wabunifu, kuwalea na kuwakuza wengine na kubwa zaidi kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu. Pamoja na jitihada hizo za kuwa na mifuko hiyo, bado kuna kazi ya kufanya kwa SIDO na hasa kutangaza fursa hizi kwa wananchi na kuhakikisha mnailea na kuikuza mifuko hiyo ili kuweza kikidhi mahitaji yaliyopo. Ongezeni wigo wa vyanzo vya fedha ili kutunisha mfuko wa NEDF.

 

15.         Nimefurahishwa sana na taarifa kuwa, SIDO inashirikiana na Benki ya CRDB kutoa mikopo kwa viwanda vinavyochakata mazao na pia Mfuko wa NSSF kupitia SANVN Viwanda scheme nao wanatoa huduma mbalimbali za kuwawezesha wajasiliamali wetu. Huu ni mfano mzuri na wa kuigwa kwa Taasisi zetu za fedha kushiriki moja kwa moja kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza ajira na kupunguza umaskini kwa wanachi wetu. Nitumie fursa hii kuziomba taasisi nyingine za fedha kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha wajasiliamali wadogo.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

16.         Ninapokaribia kuhitimisha hotuba yangu, napenda kuwaelekeza Wizara ya Viwanda na Biashara na SIDO watumie Balozi zetu nje ya nchi katika kupata teknolojia rafiki, mitaji na fursa ya kujifunza namna wenzetu wanavyosimamia taasisi inayofanana na SIDO yetu pamoja na kutafuta masoko. Zipo nchi nyingi sana ambazo wameweza kutumia vizuri viwanda vidogo katika kukuza ajira na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi. Tujifunze kutoka huko wamewezaje! Mfano nchi ya China asilimia 90 ya viwanda vyake ni viwanda vidogo na vya kati ambavyo kwa wastani vinachangia asilimia 60 kwenye Pato la Taifa (GDP) na asimia 80 ya ajira. Kwa upande wa India, Viwanda vidogo na vya kati vinachangia asilimia 95 ya pato la Taifa na asilimia 45 ya mauzo nje;  na kwa upande wa Balozi zetu, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ninawaelekeza kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi una lenga pia katika kukuza na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati hapa nchini kwa kutoa  kipaumbele katika:

 

(i)    Kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati;

 

(ii)    Kuratibu upatikanaji wa teknolojia zinazofaa katika mazingira ya nchi yetu na masoko ya bidhaa za Viwanda vidogo;

 

(iii)  Kuratibu upatikanaji wa mitaji kutoka kweye mifuko au taasisi zinazofanya hivyo katika maeneo yenu ya uwakilishi hususan taasisi zinazotoa mikopo nafuu kwa SMEs;

 

(iv) Kuiunganisha Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SMEs) na zile za nje kwa madhumuni ya kubadilishana uzoefu na taarifa za masoko pamoja na kuziwezesha kuingia makubaliano ya ushirikiano (MOU) katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na teknoligia na ubunifu; na

 

(v)   Kuiunganisha Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na taasisi zinazotoa elimu na kujenga uwezo kwa ajili ya SMEs zetu kuuza katika masoko ya kimataifa kwa kujua taratibu na kanuni za masoko hayo.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

17.         Kwa upande wa Serikali napenda niwahakikishie kuwa tutaendelea kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji ili bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo nchini ziweze kuwa na bei nafuu na kupanua soko lake ili kukuza viwanda vya ndani. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kusimamia agizo la utengaji maeneo ya viwanda katika kila Halmashauri ya Wilaya ili kuongeza ufanisi wa viwanda vyetu kuzalisha katika mazingira bora.  Serikali imeweka kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuhakikisha tunakuwa na nishati ya uhakika ikiwa ni pamoja na Mradi wa Bwawa la kufua umeme wa maji la Mwalimu Nyerere mto Rufiji, mradi wa kuunganisha mikoa yote na Grid ya Taifa na mradi wa kuvipatia vijiji vyote umeme ifikapo 2025. Ninawaagiza wakuu wote wa mikoa kupitia Kamati za Maendeleo za mikoa kujiwekea malengo ya kuongeza viwanda vidogo kila Wilaya hususan vinavyochakata mazao ya kilimo. Aidha, ninazitaka Wizara za Kilimo, Viwanda na Biashara, Elimu, Teknolojia & Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa kipaumbele kwa utafiti na maendeleo (R & D) katika sekta hii muhimu.

 

Ndugu Wananchi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

18.         Nimalizie hotuba yangu kwa kuwapongeza tena Viongozi, Washiriki, Wafadhili mbalimbali na wenyeji wetu wananchi wa Mkoa wa Kigoma na hususan wa hapa Kasulu waliotukaribisha na wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha maonesho haya. Aidha, niwasihi watanzania wenzangu kuwa tuthamini na kupenda bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwani zina ubora na viwango vinavyostahili.  Waswahili wanasema “Kipende chako”.

 

19.         Baada ya kusema hayo,  kwa heshima na taadhima, natamka kuwa maonesho haya ya Tatu ya SIDO Kitaifa hapa Kasulu, Mkoani Kigoma yenye kaulimbiu “Pamoja Tujenge Viwanda kwa Uchumi na Ajira Endelevu” yamefunguliwa rasmi leo tarehe 22/09/2021”

 

KIGOMA OYEE! KASULU OYEE! JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KAZI IENDELEE

 

MUNGU AWABARIKI, ASANTENI KWA KUNISIKILIZA 

 

Makamu wa Rais wa Dk. Philip Mpango akikata utepe kufungua rasmi Maonyesho ya tatu ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika Viwanja vya Umoja Wilayani Kasulu mkoani Kigoma, leo Septemba 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages