Na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma, leo
Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa leo amefanya kikao kwa njia ya Video na Wakuu wa Mikoa yote na Kamati zao za Ulinzi na Usalama, akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma na kuwataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia vilivyo miradi ya maendeleo na uzalishaji wa mazao kulingana na jiografia ya maeneo husika.
“Asilimia 75 ya wananchi kwenye mikoa yenu, wanajishughulisha na kilimo. Lazima Ma-RC tusimamie kilimo huko tuliko. Kwa kawaida tunalima kwa kutegemea mvua lakini kwenye mikoa ambayo ina mito, ni vema tugeukie kilimo cha umwagiliaji maji kwa kutumia gharama kidogo.
Kule wilayani, maafisa kilimo wahusishwe kwenye miradi ya umwagiliaji, ingawa tumeunda Tume ya Umwagiliaji pekee, lakini tunahitaji maafisa kilimo wasimamie miradi yote na wahakikishe inafanya kazi", amesema Waziri Mkuu katika mazungu,zo hayo.
Kuhusu mazao ya kimkakati, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kusimamia mazao kama alizeti, chikichi, parachichi na sasa inaimarisha mazao ya ufuta, kokoa na fiwi. Amewataka wakuu hao wa mikoa wasimamie mazao hata kama kuna changamoto ya bei.
“Ni lazima tulime hata kama kuna changamoto ya bei, msimu ukianza kila mmoja lazima ajihusishe na kilimo. Ukichukulia zao la alizeti, utabaini kuwa lina uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya viwanda. Iweje sasa, viwanda vinafungwa kwa kukosa malighafi?
Kuna viwanda vya kusindika alizeti kule Singida vimepunguza uzalishaji. Vingine viko kule Bunda, Morogoro na Shinyanga lakini sasa vimefungwa kwa kukosa malighafi wakati hali ya hewa ni nzuri. Kwa hiyo, Wakuu wa Mikoa tusimamie mfumo wa mauzo kupitia ushirika,” Waziri Mkuu alisema na kuhoji kisha akaongeza;
“Waelewesheni wananchi kuhusu ushirika, waelezeni faida za ushirika na jinsi wanaweza kunufaika kupitia ushirika wao. Ushirika ni muhimu sana, mnaweza kuanza na vyama vya msingi na kisha kuendelea hadi ngazi nyingine.”
Ameyataja maeneo mengine ambayo yanahitaji usimamizi wa karibu kuwa ni miradi ya ujenzi wa barabara, umeme vijijini, elimu, maji, afya na ulinzi na usalama. “Miradi ya barabara iwe ni ya TANROADS au TARURA, isimamieni, mjue iko mingapi, imekamilika au la na kama imekwama tafuteni kujua sababu zilizofanya ikwame. Ni wajibu wenu kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” amesisitiza.
Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka ifikapo Disemba, 2021 iwe imemaliza kupeleka umeme kwenye vijiji 1,900 vilivyobakia na ianze kupeleka kwenye vitongoji.
Amewataka wakuu hao wasimamie wakandarasi walioko kwenye mikoa yao na kujiridhisha ujenzi wa miradi hiyo umefikia hatua zipi. “Hatuwezi kuwaacha wawe wanajenga kwa spidi wanayotaka wao kwani tunataka ifikapo mwaka 2025 nchi nzima iwe inawaka taa,” amesema.
Kuhusu elimu, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa wasimamie fedha zinazotumwa kutoka TAMISEMI na Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi katika muda uliopangwa. “Fedha ikija haipaswi kukaa zaidi ya wiki, ni lazima ziende kwenye maeneo ya utekelezaji,” amesisitiza.
Kuhusu afya, amewataka wakafuatilie ujenzi wa hospitali za wilaya na za halmashauri vikiwemo na vituo vya afya. “Ni lazima tujiridhishe kuwa value for money inapatikana kwenye majengo yetu.”
Kuhusu maji, amesema: “Muwasimamie wahandisi wa maji kupitia RUWASA ambao wako katika kila Halmashauri ili wafanye tafiti za kubainisha wapi pa kupata maji baridi, na hapo yanapopatikana je yapo ya kutosha?” Amesema hiyo itasaidia kuepuka kuwa na miradi ya maji ambayo ikichimbwa baada ya muda mfupi inakauka kutokana na uhaba wa maji.
Upande wa ulinzi na usalama, Waziri Mkuu amesema viongozi wanapaswa kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa kutosha nchini ili watu waweze kufanya kazi kwa amani. “Pakiwepo usalama baina koo na koo, kijiji na kijiji, itasaidia kufanya kazi na kuongeza uzalishaji.”
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewataka wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanajiandaa kwa ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwakani.
“Ni vema Ma-RC mjue idadi ya wanafunzi wa darasa la saba mlionao, mtafute uwiano wa ufaulu na kuhakikisha madarasa yanajengwa mapema ili kuepuka tabia ya kukimbizana dakika za mwisho.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu akinukuu mambo mbalimbali wakati wa Mkutano huo kwa njia ya Video. Kulia ni Waziri Mkuu akisikiliza maelezo kutoka miongoni mwa wakuu wa mikoa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇