Na Maalum, Iramba
Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda ametoa zawadi kwa walimu wa shule ya Sekondari Lulumba wilayani hapa kuchagua mbuga ya wanyama kwenda kupumzika kwa siku 3 baada ya shule hiyo kufanya vizuri sana kwenye matokeo ya kidato cha 6 na kuongoza Kiwilaya na Kimkoa huku ikishika nafasi ya 24 Kitaifa kati ya shule 610.
Mwenda ametangaza zawadi hiyo juzi, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu wa shule hiyo waliofanya vizuri kwenye masomo yao na kuiwezesha shule yao kushika nafasi ya kwanza Kiwilaya na Kimkoa na nafasi ya 24 Kitaifa kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka huu.
Akisoma historia fupi ya shule mbele ya mgeni rasmi Mkuu huyo wa Wilaya, Mkuu wa shule ya Sekondari Lulumba Benjamin Kitiku amesema siri pekee ya mafanikio hayo ni kufanya kazi kwa ushirikiano.
Amesema shule ya Lulumba ilianza Mwezi Machi 1990 chini ya usimamizi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wakati huo Kapteni John Chiligati.
Mkuu wa Shule hiyo, alisema kwa sasa shule ina wanafunzi 971 kidato cha kwanza hadi kidato cha sita, wasichana 370 na wavulana 601 kwa jumla ya mikondo 15.
Pia shule ina walimu 35 kati ya hao walimu watatu ni wa muda, walimu wa kiume 21 na walimu wa kike 14 na Watumishi tisa ambao wasio walimu.
Kuhusu hali ya ufaulu, kidato cha nne kwa miaka mitatu mfululizo toka mwaka 2018 walifaulu wanafunzi 97 sawa na 95.9%, 2019 walifaulu wanafunzi 98 sawa na 100% na mwaka jana 2020 walifaulu wanafunzi 94 sawa na 98.9%.
Kwa upande wa kidato cha sita aliyaja matokeo kama ifuatavyo; 2018/2019 walifaulu wanafunzi 71 Sasa na 100%, 2019/20 walifaulu wanafunzi 151 sawa na asilimia 100%, 2020/21 walifaulu wanafunzi 130 sawa na asilimia 100% ambapo daraja la 1-96, daraja la 2-32, daraja la 3-3.
Kwa upande wa changamoto zinazoikabili shule, akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Kitiku alisema shule ina uhaba wa maji kea kuwa maji wanayotumia kutoka idara ya maji yana mgao wa kutoka mara mbili tu kwa wiki, uhaba wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa gari la shule, uhaba wa nyumba za walimu na samani za ofisini.
Mkuu wa shule alimuhakikishia Mkuu huyo wa Wilaya kuwa mikakati waliyo nayo ni kuhakikisha wanafanya maandalizi ya kutosha na wana uhakika matokeo yajayo ya kidato cha sita wataingia kwenye kumi bora kitaifa.
Mkuu huyo wa Wilaya, aliwapongeza walimu kwa kujitoa na kufundisha kwa bidii huku akiwahakikishia walimu atahakikisha anakuwa mstari wa mbele kuhakikisha anasimamia suala la elimu na amewaambia walimu wote wilaya ya Iramba kwa mwenye shida au changamoto basi ofisi yake ipo wazi anawakaribisha na kama anatoka maeneo ya mbali anaweza kupiga simu na atatatua changamoto inayomkabili.
"Mimi ni Mwalimu na nawapenda walimu wenzangu kwani mara baada ya kumaliza masomo yangu ya elimu ya juu nimefanya kazi ya ualimu kwa kujitolea kufundisha", alisema DC Mwenda
Kuhusu changamoto za shule DC Mwenda alimuagiza Mkurugenzi kwa kusema aangalie namna atakavyoweka kwenye mipango ya Halmashauri kuhakikisha anazitatua changamo za shule hiyo ya Lulumba.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akimkabidhi zawadi mmoja wa walimu wa shule ya Sekondari Lulumba iliyopo wilayani Iramba wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu na uongozi wa shule hiyo baada ya kufanya kazi kubwa ya kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya kwanza mkoa wa Singida na nafasi ya 24 Kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita.Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akiwa kwenye picha ya pamoja ya watumishi, walimu na uongozi wa shule ya sekondari Lulumba baada ya kumalizika kwa hafla ya kuwapongeza walimu na uongozi wa shule hiyo baada ya kuifanya kushika nafasi ya kwanza Kimkoa wa Singida na nafasi ya 24 Kitaifa katika matokeo ya kidato cha 6. (Picha na Ofisi ya DC Iramba).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇