LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 2, 2021

WIZARA YA KILIMO YAANISHA MAFANIKIO SIKU 100 ZA RAIS SAMIA

 

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda anasema wakati akilihutubia bunge kwa mara ya kwanza Rais wa Awamu ya sita Samia Suluhu Hassan alitumia takribani asilimia 14 ya mambo yote aliyozungumza kwenye masuala ya kilimo.

Hayo aliyabainisha hivi karibuni wakati akitoa maelezo kuhusu siku 100 za Rais Samia akiwa madarakani tangu kifo cha Rais wa awamu ya tano, Hayati Rais John Magufuli kitokee.

Waziri huyo anasema jambo moja ambalo Rais, alilitamka ni umuhimu wa kuongeza tija katika kilimo kwakuwa bila kufanya hivyo nchi inaweza isiende vizuri kwenye sekta hiyo.

Alitolea mfano kuwa sasa hivi kwenye kahawa uzalishaji unaweza kuongezwa tija mara tatu ya kahawa inayozalishwa kwa sasa licha ya kuwa kwa sasa tija ni ndogo hivyo kupatikana theluthi tuu ya uzalishaji.

Amesema kwa upande wa Pamba kwenye hekari moja unapata takribani kilo 200 mpaka 350 lakini kwa nchi nyingine za Afrika Magharibi wanapata mpaka kilo 1000 hivyo tija bado ni ndogo.

”Bila hata kuongeza eneo la kulima tunaweza tukaongeza uzalishaji hivyo ukienda zao moja hadi jingine unakuta kwamba tija ni ndogo sana” Amesema

Anasema Rais Samia alielekeza nguvu kubwa ielekezwe katika kuongeza tija hivyo bajeti ya wizara ya Kilimo iliyosomwa bungeni imeanisha mikakati ya kuongeza tija na fedha katika maeneo ya kupaumbele.

Anaeleza waliona cha muhimu katika yote ni suala la utafiti wa mbegu bora ambazo zinaongeza tija, na kilimo bora.

Amesema hayo ni mafanikio makubwa kwa sababu alitembelea baadhi ya vituo vya utafiti ambavyo watu wameanza kukata tamaa na kuhisi kwamba serikali ilikuwa ikipuuza suala hilokwa sababu hautoi matokeo mara moja hali inayosababisha watu kutafuta vitu vyenye matokeo ya haraka.

Alisema suala la pili ni kuzalisha mbegu bora zaidi kutokana na uhaba wake kuwa ni kikwazo kikubwa cha uzalishaji wa tija huku akitolea mfano zao la alizeti ambalo kwa sasa serikali imekusudia kuongeza wazalishaji nchini licha ya kutokuwepo mbegu.

”Tumeamua mashamba yote ya mawakala wa mbegu Tanzania 13 tutayafufua, kuyamawagilia ili yaanze kuzalisha mbegu ziwafikie wakulima na tumeongeza bajeti kubwa kwenye suala la uzalishaji wa mbegu,” Alisema.

Alifafanua kuwa bajeti imeongezwa kwenye huduma ya ugani ambayo ilikuwa milioni 603 tuu hadi bilioni 11.5 licha ya kuwa hazitoshi hivyo nguvu itawekwa mikoa mitatu ya Dodoma, Singida na Simiyu kuonyesha namna huduma hiyo inatakiwa ifanyike ili kuongeza tija.

Pia, alisema utaanzishwa mfuko wa umwagiliaji kwa ajili ya kuhakikisha kwamba uzalishaji wa ekari unaongezeka.

Alieleza pamoja na mambo hayo kuna masuala ya masoko ili kuhakikisha kwamba mkulima anapolima anaweza kuuza huku akieleza tatizo lipo la aina mbili ambapo ni uzalishaji ambao wakulima hawajui wauze wapi bidhaa zao.

”Sasa hivi tuna mchele mwingi, mahindi lakini hatuna wananunuzi wakutosha na ukiongea na wakulima mengine wanaona hii haitaleta hamasa ya kuendelea na kilimo huko mbele ya safari,”alisema.

Alieleza kwenye hilo wanafanya mazungumzo na nchi mbalimbali na mwisho wa mwezi Julai hatimaye inawezekana Sudani Kusini wamekubali kwamba wanaweza kutupokea mwisho wa wiki ambapo wataenda na wafanyabiashara kwa ajili ya kuangalia masoko ya huko jinsi tunavyoweza kuuza mchele, mtama, mahindi.

Aidha, alibainisha kwa nchi za DRC, Zimbabwe wataangalia vilevile masoko ya mchele, kwa maana umeanza kuuzwa katika nchi ya Swaziland na wanaangalia uwezekano wa kuuza Afrika Kusini.

Alieleza hayo yote yanahitaji wajasiriamali kuchangamka kwa kuwezeshwa kujenga mazingira bora ili wachangamkie fursa ikiwa ni pamoja na kuchakata mazao kabla ya kuyauza maana ukitaka kuuza mchele vizuri ni lazima uchakatwe na kupelekewa kwenye masoko ya Afrika nzima.

Alibinisha katika suala hilo la masoko ambapo wakulima wanakosa mahali pa kuuza moja ya changamoto ilikuwa ni ndani ya nchi kwamba wafanyabishara wa mazao walikuwa wakati mwingine wanapata usumbufu mkubwa kwa kusimamishwa na kukamatwa hivyo kuwa kama wanafanya biashara haramu.

Alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwamba kwa sasa wanasaidia biashara iende na kwamba kauli ya Rais Samia kuboresha mazingira ya biashara inaweza kuwa imesaidia kwa namna moja ama nyingine.

”Sisi tunasema mazao sio bidhaa haramu kwahiyo acha ziuzwe na sisi kwa kilimo tunasema acha bidhaa hizi ziuzwe popote na kwa namna yoyote ile ili kuongeza tija na masoko,”alisema.

Alifafanua aina nyingine ya changamoto ya masoko ni pale ambapo sisi tunahitaji mafuta ya kula lakini hatuzalishi bidhaa hiyo japo kuwa tungeweza kulima alizeti lakini hatulimi ya kutosha na wakulima wanahitaji fedha hivyo wangefanya hivyo wangepata fedha za kutosha.

Alieleza tunatumia nusu trilioni za fedha za nchi yetu kwenda kununua mafuta nje ya nchi sasa hapa tumeshindwa kuzalisha kile ambacho kinahitajika ndani ya nchi, tatizo hilo pia lipo kwenye ngano, Shayiri, hivyo hilo nalo watapambana nalo katika mkakati wa bajeti ili kuongeza tija.

Kuhusu suala la kuwekeza mitaji na kufanyia kazi katika kilimo na kilimo anga, alisema nzige kwa wakati fulani lilikuwa kama tatizo kubwa ikabidi ahamie eneo la tukio ’site’ kuhakikisha kuwa suala hilo linaisha.

Alibainisha wakati wa kupambana na nzige aligundua kuwa tatizo moja wapo ni kwamba mitaji iliyopo zinamilikiwa pamoja na nchi nyingi huku akitolea mfano ndege za kupambana na nzige ambazo zinamilikiwa chini ya umoja wa kupambana na nzige wa jangwani nchi ambazo zinaunganisha Tanzania, Uganda, Kenya, Somalia, Elitrea, na Sudani Kusini.

Alisema inabidi kupeleka kule taarifa ya kutaka kuletewa ndege hali iliyosababisha ufanisi kuwa mbaya kwa sababu ilikuwepo ndege moja ambayo ipo Moshi lakini rubani yupo Nairobi hivyo wakaanza kuhisi kwamba kama hali ingekuwa kubwa na tishio lingekuwa kubwa katika nchi nyingi ingekuwa ni vigumu kugombana nao.

”Wakati wa kupambana na nzige ilikuwa changamoto kubwa hadi uangize ndege kule inakuwa ngumu ndio maana tukaamua kujenga uwezo wa ndani kwa kurudisha kilimo anga kwa sababu uharibifu wa mazao vilevile unapunguza tija,”.

Alisema hayo ni masuala ambayo yamejitokeza kipindi hiki cha siku 100 za Rais Samia ambaye anawapa watanzania matumaini makubwa katika kilimo ndio maana fedha zimeongezwa kwa ajili ya kusukuma vipaumbele vitakavyoongeza tija kwenye sekta hiyo.

Akizungumzia juhudi ambazo zimefanywa na Rais katika kuimarisha mazingira ya biashara, alisema hiyo ni pamoja na nchi kuwa na amani na utulivu, uchumi mpana ulitengamaa, kuwa na miundombinu wezesha na huduma za kiuchumi ikiwemo nishati.

Aidha, kuwa na mfumo mzuri wa masuala ya kanuni na usimamizi wa shughuli za kiuchumi maeneo mbayo mara nyingi yamekuwa yakitolewa malalamiko.

Alisema nchi imeimarisha mifumo ya biashara ambapo awamu ya tano iliwekeza zaidi kwenye miundombinu lakini Rais Samia amekuwa akitoa matamko ya kuongeza imani ya watu ambao walikuwa wanahisi kwamba pengine dola halitabiriki sana katika shughuli zake za uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages