Na Jacqueline Liana
KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM}, Daniel Chongolo, amesema uongozi
siyo ukubwa wa kutaka utukufu, bali ni wajibu unaoambatana na dhamana.
Amekemea tabia aliyoita ya hovyo ya baadhi ya wana-CCM ya kupanga safu za uongozi kinapofika kipindi cha uchaguzi wa viongozi.
Ameyasema
hayo leo Julai 7,2021 katika wilaya ya Sumbawanga Vijijini, mkoa wa
Rukwa, ambako yuko kwa ziara ya kikazi katika mikoa ya Rukwa, Mbeya na
Songwe, akiwa amefuatana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM taifa,
Komredi Ngemela Lubinga, Komredi Shaka Hamdu Shaka na Komredi Kenani
Kihongosi.
Chongolo
alikuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa CCM wa mkoa wa Rukwa
katika kikao kilichofanyika Sumbawanga Vijijini, na kufafanua kwamba,
lazima kila kiongozi ajiulize amewafanyia nini wale anaowaongoza.
"Ukiwa
kiongozi lazima ujiulize nini umekitendea chama na wanachama, ukiitwa
mwenyekiti siyo kwa sababu ya shati ulilovaa au viatu ulivyopiga kiwi au
mtindo wa nywele ulionyoa," alionya Chongolo.
"Uongozi
ni wajibu wa kujua ni kipi chenye masilahi kwa chama," alisema na
kunukuu kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba "uongozi ni
mzigo".
Alisema kwamba
mwaka 2022 ni mwaka wa uchaguzi ndani ya CCM na ni wakati wa kuwapata
viongozi bora na siyo wale wanaopangwa kwa masilahi binafsi.
Chongolo
alisema kwamba miongoni mwa wana-CCM kuna wanaofaa kuwa viongozi lakini
hawana kimbelembele kama wale wanaondekeza upangaji wa safu.
Alisema wanachama wenye sifa za kuwa viongozi hapana budi washawishiwe wagombee nafasi za uongozi katika chama.
Akimnukuu tena Mwalimu Nyerere, Chongolo alitaka wanaokimbilia uongozi kuogopwa kama ukoma.
"Eti
kuna mwingine anajipanga kuwa kiongozi...niwaombeni mhakikishe
hamruhusu watu wanaopanga safu. Watu wazuri hawana tabia ya kimbelembele
kutaka madaraka," alisema.
Aliitaja kazi nyingine na viongozi ni kuwaandaa viongozi wa baada yao, kwa sababu uongozi ni kupokezana vijiti.
"Mtu huwezi kuwa kiongozi milele," alisema na kuhoji kwanini mtu ang'ang'anie madaraka?
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇