Na Jacqueline Liana, Sumbawanga
KATIBU
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Kanali mstaafu Ngemela
Lubinga, amewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuepuka majungu.
Lubinga
alisema hayo Julai 7, 2021 alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM
katika ngazi za mashina wilayani Sumbawanga Mjini, katika mkoa wa Rukwa.
Alisema
kwamba CCM ina utaratibu mzuri wa kushughulikia changamoto za viongozi
na watendaji wake, hivyo hakuna haja ya kupigana majungu.
Kiongozi
huyo aliwataka wana-CCM kuonyeshana upendo na iwapo atatokea mwenye
kwenda kinyume na maadili ya chama, arekebishwe kwa staha kupitia vikao
vya chama.
Kuhusu masuala
yanayozungumzwa na kujadiliwa katika vikao hivyo, alisema wajumbe
wanapaswa kuwa na vifua vya kutunza siri kwani ni kinyume cha maadili
kutoa siri za vikao.
Alisema moja ya sifa ya kiongozi bora ni uwezo wa kutunza siri kwa masilahi ya CCM.
Kuhusu
uchaguzi wa viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali utakaofanyika
mwakani, Kanali mstaafu Lubinga aliwataka wanachama wa CCM kuwachagua
wagombea watakaokuwa watumishi wazuri wa CCM.
Alisema wapo viongozi na watendaji wa chama 'huwabeba' wagombea na kusababisha mitafaruku isiyo na tija kwa chama.
Kiongozi
huyo alifafanua kwamba, tabia hiyo ni miongoni mwa sababu za uwepo wa
makundi yasiyo na masilahi kwa chama na wanachama, hivyo hapana budi
ikome.
"Viongozi tusibebe wagombea, ukibeba mgombea umepoteza sifa ya kuwa kiongozi na mtendaji wa chama chetu," alionya.
Kuhusu
changamoto zinazowakabili wanachama na wananchi kwa jumla, aliwataka
viongozi na watendaji wa CCM kutenga muda wa kusikiliza kero na
kuzitafutia majawabu.
Alisema,
ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, imelenga kuondoa kero mbalimbali
katika jamii, hivyo utekelezaji wake unapaswa kusimamiwa kwa makini.
Alisema
ilani hiyo ina ahadi za maendeleo zinazotekelezwa nchini kote, hivyo ni
wajibu wa viongozi na watendaji wa CCM, kuanzia ngazi za mashina,
kuhakikisha zinatekelezwa kwa ufanisi.
Alifafanua kwamba serikali inatoa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima zitumike kwa kusudi hilo.
Pamoja
na kuzungumza na wanachama wa CCM katika ngazi za mashina, pia kiongozi
huyo alikagua na kushiriki katika ujenzi wa madarasa katika shule za
msingi za Isale na Manga za Sumbawanga Mjini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇