Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu Zanzibar, Mheshimiwa Zena Said (pichani) amepongeza kazi zinazofanywa na Kampuni ya Global Education Link (GEL) katika sekta ya elimu nchini na kushirikiana katika kusaidia kuzalisha wataalam.
Pongezi hizo zimetolewa wakati alipotembelea mabanda ya kampuni ya GEL katika maonyesho ya vyuo vikuu yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kwenye maonyesho hayo yanayoshirikisha vyuo vikuu mbalimbali nchini, GEL imefanikiwa kuleta vyuo vikuu 10 ambavyo ni washirika wake nje ya nchi kwa ajili ya kuja kuelezea fani wanazotoa na namna Watanzania wanavyoweza kujiunga na vyuo vyao.
Vyuo hivyo ni Chandigarh, Lovely Professional University,
CT, Maharish Makandeshwar, Pandeet Deendayal Energy, Sharda, Rayat Bahra vya
India na V.N. Karazin Kharkiv na Sumy State vya Ukraine.
Katibu mkuu huyo kiongozi alisema ni kweli kutokana na uhaba
wa fani mbalimbali hapa nchini, baadhi ya wanafunzi wanalazimika kwenda nje ya
nchi kusoma elimu ya juu hivyo kuwa na kiunganishi ni jambo la msingi katika
kurahisisha upatikanaji wa vyuo hivyo.
“Ni kweli vyuo vyetu haviwezi kuchukua wanafunzi wote kwa sasa, nawapongeza kwa kazi hii ya kuwaunganisha wanafunzi wetu na vyuo vya nje,” alisema katibu mkuu kiongozi huyo huku akishangiliwa na umati wa wazazi na vijana waliofurika katika mabanda 21 yanayotumiwa na GEL pamoja na washirika wake kufanya maonyesho.
Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalick Mollel alimweleza katibu mkuu
kiongozi huyo kuwa kampuni yake imekuwa ikishirikiana na vyuo vya nje kuwapeleka
wanafunzi wa Tanzania kwa kozi mbalimbali ikiwemo kuzungumza na vyuo vya ndani
ili viweze kubadilishana wanafunzi (exchange program).
Mollel alisema wakati nchi nyingi duniani zina kozi nyingi za
afya, kwa Tanzania bado hazijawa za kutosha hivyo wanafunzi wanaotaka kozi hizo
na nyinginezo nyingi ambazo bado hazipatikani nchini, wamekuwa wakiwaunganisha
kwenda kusoma kwenye nchi hizo.
“Tumezungumza na vyuo vingi vya nje ya nchi kwamba sisi tuna
wanafunzi wengi na wamekubali kuwachukua wanafunzi wa Kitanzania kwa gharama nafuu;
zinazofanana na za hapa ndani ya nchi yetu,” alisema Mollel na kuongeza kuwa
baadhi ya vyuo vimeahidi kufungua matawi nchini baada ya kuona mahitaji makubwa
ya kozi wanazofundisha ambazo wanafunzi wa Tanzania wamekuwa wakizifuata katika
mataifa yao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇