Viongozi na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamesisitizwa kutotoka katika utaratibu hususani wakati chama kikielekea katika uchaguzi wa ndani nchini, huku kikisisitiza kuwa utulivu na uimara wa CCM ni matokeo ya kuimarika kwa demokrasia ya ndani ya CCM.
Kimesema sababu nyingine inayoongeza imani ya CCM na kukubalika kwake na umma ni hali ya demokrasia ndani ya chama hicho kuimarika zaidi, kutoweka kwa makundi pamoja na uadilifu na uwajibikaji kupewa msukumo wa kipekee ndani na nje ya CCM.
Akihutubia mamia ya viongozi na watendaji mbalimbali wa chama na serikali katika kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani Mbeya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema ni matokeo ya chama hicho kuwaletea maendeleo wananchi, kuwa wasikivu kwao na kuheshimu misingi ya haki, amani, umoja na utulivu.
"CCM ndio tumepewa dhamana ya kutoa uongozi wa nchi yetu na kuunda serikali hivyo tusikubali mambo ya hovyo yakafanyika chini ya dhamana hii tuliyopewa." Alisema Chongolo
Chongolo amefahamisha kuwa Katika kuendelea kuhimiza umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ni lazima wanachama wapewe nafasi ya kusikilizwa badala ya wanapotoa maoni yasiyowapendeza viongozi wakaonekana wasaliti na kutengenezewa mizengwe.
"Chama lazima kiwe kinafanya vikao na kuhakikisha vinakuwa vyenye agenda za maendeleo na sio kujadili watu, majungu au kuendeleza siasa za makundi, wakati huo huo tukumbuke wanachi wetu maana
sio uungwana wananchi kupata majibu ya kero zinazowakabili pale tu viongozi wa kitaifa wanapowatembelea bali ni haki yao na wajibu wa lazima kwa waliopewa dhamana kufanya hivyo" alisema Chongolo
Hata hivyo alisema wakati chama hicho kikielekea katika uchaguzi wa ndani Maana si vyema wanachama kutengenezewa tuhuma za kupika ili wakose sifa za kuomba uongozi ndani ya chama jambo ambalo sio sawa na chama kitakuwa makini kuhakikisha wanachama hawaonewi na haki inatendeka.
"CCM imeendelea kubaki kuwa tumaini pekee la watanzania ikiwa ni matokeo ya chama chetu kujisahihisha na kurejesha imani kubwa kwa wananchi kwa kuisimamia serikali kwa ufanisi mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii, upatikanaji wa haki, kudhibiti vitendo vya wizi, rushwa, ufisadi, kukemea vikali matumizi mabaya ya madaraka, ulinzi wa rasilimali za nchi, kuukabili utendaji kazi wa mazoea na matumizi yenye tija kwa mapato ya serikali" alisema chongolo
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo na Sekretarieti yake ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wamehitimisha ziara yao katika mikoa ya Rukwa, Songwe na Mbeya.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka akiandika jambo wakati wa kikao hicho.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho cha Majumuisho.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho cha Majumuisho.
Wajumbe na waalikwa wakiwa kwenye kikao hicho cha Majumuisho.
Chongolo akiwashukuru wajumbe wakati akitoka ukumbini baada ya kikao hicho cha Majumuisho.
©CCM Blog/Uenezi CCM/Julai 14, 2021
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇