Dar es Salaam/Dodoma.
Wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikihitimisha mjadala wa bajeti yake jana, baadhi ya wataalamu wamemkosoa Askofu Josephat Gwajima kwa msimamo wake kuhusu chanjo ya Corona.
Gwajima, ambaye ni Mbunge wa Kawe (CCM) alitoa angalizo hilo Mei 11, wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na kuzitaja aina tatu za chanjo ya ugonjwa huo alizosema hazijafanyiwa utafiti wa kina.
Pia, alisema chanjo hizo hazijapitishwa na taasisi zinazohusika na udhibiti wa magonjwa ambazo ni CDC (Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa) na FDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa) kwa Marekani na EMA (Wakala ya Dawa) kwa Ulaya.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Daniel Maeda alisema Askofu Gwajima anapotosha anaposema taasisi ya CDC inahusika na kuruhusu kutumika kwa chanjo au ubora wake.
“CDC haihusiki na upitishaji wa chanjo, bali inahusika na magonjwa ya binadamu kama ilivyo NIMR (Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu). FDA ndiyo inayoruhusu chanjo na ndiyo imeunda mfumo wa kuruhusu chanjo za dharura, siyo shirika jingine kama anavyosema Gwajima,” alisema Dk Maeda alipozungumza kwa simu.
Akifafanua zaidi, alisema chanjo hizo za corona zimeruhusiwa kwa dharura baada ya utafiti wa awali kuonyesha zina faida zaidi kuliko madhara katika kukabiliana na virusi hivyo vinavyoitesa dunia kiasi cha kuyumbisha uchumi.
“Wametoa ruhusa huku wakiendelea na utafiti mwingine kuona kama faida walizoziona zinaendelea kuwepo au kutaibuka madhara ambayo hawakuyaona awali,” alisema.
Kuhusu madhara ya kijenetiki, Dk Maeda alisema si kweli kwamba chanjo hizo zinaweza kuleta madhara.
“Chanjo hizi zinapoingia kwenye seli hazipenyi kwenye kiini (nucleus) bali zinaishia kwenye ganda la juu (cytoplasm). Kwanza hata virusi vya corona haviwezi kuingia kwenye kiini hicho. Kinachoweza kuingia ni virusi vya Ukimwi na ndiyo maana mpaka sasa hakuna chanjo yake,” alisema.
Kwa upande wake, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema hakuna haja ya kuwa na hofu kwa kuwa chanjo zote zimethibitishwa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linalosimamia tiba na afya za watu wote duniani.
Aliongeza kuwa matumizi ya chanjo duniani yamepunguza maambukizo nchi za Ulaya na Marekani.
Hoja za wabunge
Akihitimisha mjadala wa hotuba yake ya bajeti jana, Waziri wa Afya, Dk Doroth Gwajima alisema yeye na timu yake wamejipanga kushughulikia hoja hizo kwa masilahi ya Watanzania.
Akijibu hoja kuhusu janga la corona iliyoibuliwa na Askofu Gwajima juzi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema hadi sasa Serikali bado inatembea na kauli ya Hayati John Magufuli aliyoitoa mkoani Kagera aliposisitiza kuwa Tanzania haiwezi kupokea kila kitu kutoka nje bila kukifanyia uchunguzi wa kujiridhisha.
Alisema ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume ambayo imejaa wasomi na maprofesa.
“Tanzania haipingani na WHO (Shirika la Afya Duniani) wala siyo kisiwa cha kujifungia, hoja ya Mheshimiwa Gwajima tumeichukua na kumwambia kuwa Serikali inalitambua hilo na iko makini hivyo mtupe muda kamati aliyoiunda mheshimiwa Rais itakuja na majibu yote,” alisema Dk Mollel.
Alisema Serikali inajua kuhusu uchunguzi wa chanjo na hadi sasa kamati hiyo iliyojaa maprofesa imejichimbia kutafiti na itakuja na majibu ya moja kwa moja kumshauri Rais cha kufanya.
Kuhusu mtambo wa kuzalisha barakoa unaodaiwa kuzalisha chini ya matarajio, Waziri Gwajima alikiri kuwa ulianza kwa kusuasua, lakini baadaye walinunua na na kuboresha vifaa hivyo ukaanza kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa ambacho ni barakoa 48,000 kwa siku.
Akijibu hoja za jumla zilizotolewa na wabunge, Waziri Gwajima alisema suala la uhaba wa dawa bado lipo, ila linachangiwa na kupatikana kwa fedha.
Waziri alikiri kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya kununua dawa, vifaa na vitenganishi hazikutolewa kama ilivyotakiwa, lakini akaahidi kuwa Sh200 bilioni zilizopangwa mwaka wa fedha 2020/21 zitatolewa hadi mwishoni mwa Juni unapohitimishwa mwaka wa fedha.
Alisema kumekuwa na mwongozo ambao utawezesha kuwa na mzunguko mzuri wa upatikanaji wa dawa kutokana na mchango wa watu wanaochangia katika huduma ya afya kwenye dawa ambako alisema usimamizi wake utakuwa mkubwa zaidi.
Waziri pia alizungumzia bima ya afya kwa wote na aliwataka wabunge kuwa wavumilivu, kwani muswada uko mbioni kupelekwa mjengoni humo kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii wanayoiwakilisha.
Na kuhusu madeni yaliyopo ndani ya wizara hiyo na taasisi zake, alisema hadi Aprili 2021, Serikali ilishalipa Sh16.3 bilioni, lakini bado inadaiwa Sh260.7 bilioni na Bohari ya Dawa (MSD) ambazo zinajumuisha madeni ya vituo vya afya.
Askofu GwajimaSource: Mwananchi Digital
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇