LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 29, 2025

CCM YATANGAZA ILIOWATEUA KWENDA KURA ZA MAONI UBUNGE

Dodoma, Julai 29, 2025
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza majina ya Wanachama wake kiliowateua kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025.

Majina hayo yametangazwa leo mjini Dodoma, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM CPA Amos Makalla, ikiwa ni baada ya kukamilika michakato ya kuyapata majina hayo miongoni mwa walioomba uteuzi wa kugombea, mchakato ambao ni pamoja na vikao vya juu vya chama, ikiwemo Kamati ya Usalama na Maadili, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), vilivyoketi hadi usiku wa manane Julai 28.

Miongoni mwa waliokosa kurejea ni aliyewahi kuwa mgombea urais mwaka 2015, Januari Makamba ambaye halikurudi katika Jimbo la Bumbuli na aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Mjini na Naibu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Stephen Byabato.

Wengine ni Waziri wa zamani wa ardhi, Anjelina Mabula jimbo la Ilemela, Naibu Waziri wa zamani wa Michezo, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul- Babati mjini, na wabunge maarufu Christopher Olesendeka jimbo la Simanjiro na Seif Gulamali wa jimbo la Manonga.

Pia katika Jimbo la Arusha Mjini, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mrisho Gambo naye ametemwa, huku Ole Sabaya, Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Hai, jina lake likiondolewa kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi. Waziri Mkuu wa sasa, Kassim Majaliwa, alitangaza mwenyewe kuwa hatawania tena ubunge katika Jimbo la Ruangwa.

Halikadhalika Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, ambaye alikuwa akitazamiwa kugombea Jimbo la Kigamboni, jina lake halikurudi na badala yake watu sita wamepitishwa kuwania nafasi hiyo. Majina hayo ni Ponela Mtei, Habib Mchange, Allan Sanga, Ally Mandai, Francis Elias, na Henjelewe.

Katika Jimbo la Kisesa, Simiyu, kama ilivyotarajiwa na wengi, aliyekuwa mbunge Luhaga Mpina ameondolewa, huku majina saba yakipitishwa kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya majina makubwa yamerudi wakiwemo wanamichezo na wanahabari. Jerry Muro, mwanahabari, msemaji wa zamani wa Yanga na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya, amepitishwa kugombea Jimbo la Hai. Mtangazaji maarufu wa michezo, Shaffih Dauda, jina lake limepita katika Jimbo la Temeke, na Jemedari Said ametajwa kugombea Jimbo la Mtama.

Hashim Ibwe atapeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Mwanga, Mtangazaji wa zamani wa BBC, Salim Kikeke, amepitishwa kugombea Jimbo la Moshi Vijijini. Katika Jimbo la Kigoma Mjini, Baruani Muhuza na Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, wamepitishwa kuwania nafasi hiyo.

Mkuwe Issale "Mamybaby, Mtangazaji wa Clouds fm amepitishwa kuwania viti maalumu Tabora, kama ilivyo kwa Jesca Magufuli, mtoto wa rais wa awamu ya nne, John Pombe Magufuli aliyepitishwa kupitia Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa.

Mtoto wa Rais Samia, Wanu Hafidh Ameir amepitishwa jimbo la Makunduchi na Mkuu wa mkoa wa zamani mweye 'vituko', Agrey Mwanri amerejea tena kupitia Jimbo la Siha.

Familia ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete imeendelea kuwa na ushawishi ndani ya CCM. Mke wake, Mama Salma Kikwete, amekuwa mgombea pekee katika Jimbo la Mchinga, Lindi, huku mtoto wao, Ridhiwani Kikwete, pia akipitishwa peke yake Jimbo la Chalinze.

Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko, naye hakuwa na mpinzani katika Jimbo la Bukombe. Katika visiwa vya Zanzibar, Hemed Abdulla ametajwa kama mgombea pekee Jimbo la Kiwani, huku Jimbo la Ole likiwa na majina mawili yaliyopitishwa – Ali Salim Ali na Amour Kassim.

Majina mengine yaliyovuta hisia ni la Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, na Deo Sanga waliopitishwa Jimbo la Makambako, ambapo Sanga anatetea nafasi yake. 

Aidha Wilson Mahera, aliyekuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, amepitishwa kugombea Jimbo la Butiama. William Vangimembe Lukuvi, mmoja wa wanasiasa wakongwe zaidi wa CCM, amerudishwa kugombea Jimbo la Isimani kwa mara ya saba mfululizo. Lukuvi ana rekodi ya kuwa bungeni kwa miaka 30 sasa. Job Ndugai, Spika wa zamani aliyejiuzulu baada ya kutofautiana na Rais Samia, amerejeshwa jimbo la Kongwa, Dodoma.

Kwa upande mwingine, waliokuwa wabunge wa CHADEMA na kurejea CCM, nao wamepita katika mchujo  Jesca Kiishoa, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA, ameteuliwa kugombea Jimbo la Iramba Mashariki. Ester Bulaya, mmoja wa wanasiasa waliokuwa maarufu CHADEMA, ametajwa miongoni mwa majina matano yaliyopitishwa kugombea Jimbo la Bunda Mjini. Viongozi wengine waliokuwa upinzani ni pamoja na Peter Msigwa, ambaye sasa jina lake limepita Jimbo la Iringa Mjini, na Ester Matiko aliyefukuzwa CHADEMA, sasa amepitishwa kugombea Jimbo la Tarime Mjini.

Mchakato wa uteuzi wa CCM mwaka huu umeonyesha mwelekeo mpya wa kisiasa ndani ya  chama. Wakati baadhi ya sura kongwe zikitemwa, wanasiasa wapya na wale waliorejea kutoka upinzani wamepewa nafasi, hali inayoweza kubadili ramani ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Mchakato wa kupata jina moja kila jimbo utafanyika mwezi ujao.


Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amos Makalla akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma, leo.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages