LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 11, 2021

CCM YAMLILIA TEDDY MAPUNDA, SHAKA AMWAKILISHA CHONGOLO KUAGA MWILI, DAR

Mbezi Beach, Dar es salaam
Chama Cha Mapinduzi (CCM  ) kimemtaja marehemu Magdalena Theresia (Teddy) Hollo Mapunda kuwa alikuwa ni mdau muhimu na mshirika kinara wa shughuli za maendeleo ya Taifa, ambapo wakati wa uhai wake alishirikiana vyema na Chama na Serikali kupitia tasnia ya habari, hivyo Taifa  limempoteza Mtanzania makini aliyejengeka vyema katika misingi ya uzalendo na utaifa.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka wakati akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kabla ya mazishi kufanyika ya Teddy,  nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

 Shaka ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwenye tukio hilo la kuaga mwili amemtaja Teddy kuwa  alikuwa Mtanzania aliyependa sana tasnia ya habari na kuhakikisha habari muhimu zinawafikia wananchi wanaoishi vijijini na mijini  kwa haraka na usahihi.

"Marehemu Teddy atakumbukwa kwa tabia yake ya kupenda ucheshi, huruma na upendo akiwa si mwenye majivuno , asiyedharau wenzake lakini pia hakupenda kujikweza na kuwakoga watu. 

Teddy alikuwa na kiu na mbinu za uwezeshaji wa kutosha ili habari ziweze kuwafikia wananchi na kuitangaza nchi yake hasa alipokuwa akifanyakazi  katika mbuga ya wanyama ya Taifa Serengeti", akasema Shaka Hamdu Shaka na kuongeza;

"Hayati Teddy sifa yake  kubwa ilikuwa ni unyenyekevu, ucheshi na  moyo wenye Haruna. Alikuwa ni mtanzania mzalendo, mtaifa na mchapakazi aliyependa kuona umoja wa kitaifa ukidumu nchini".

Shaka akasema, Teddy  atakumbukwa sana kwa tabia yake na mwenendo bora na adilifu  kwani hakuwa mtu mbabaishaji na asiyevunja wala kutotimiza miadi mnapowekeana  ahadi kwani aliheshimu wakati.  

"Tuige maisha  aliyoishi mwenzetu hapa duniani kwani hakuwa mtu wa majivuno. Hakuwa akivunja miadi pia hakupendelea wala kuwa na roho ya korosho. Mikono yake haikuwa kama ile ya birika, badala yake alipenda kuwasaidia wenzake kila alipoweza na kuitazama jamii" Alieleza.

Aidha shaka alisema ni watu wachache mno duniani pale wanaopata nafasi hujikuta wakizitumia vibaya kuwakomoa wenzao, kuwanyanyasa na kuwapuuza wengine jambo ambalo katika maisha ya Teddy ilikuwa ni kinyume  na hivyo. 

Shaka amewahimiza watu wengine kutambua kuwa wanadamu katika dunia wana  safari fupi  hivyo  isiwaghilibu badala yake kila mmoja ajijue  iko siku ataondoka duniani na kurudi kwenye vumbi.

"Chama Cha Mapinduzi kinatuma  salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kumuomba Mwenyezi Mungu awape familia, Ndugu, jamaa na marafiki wa Teddy, subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwao cha  msiba na maombolezo na tunaungana na wafiwa wote kumuomba Mungu amuweke mahali pema peponi", akamalizia Shaka.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka akitoa heshima kwa mwili wa aliyekuwa Mdau wa Maendeleo, Teddy Mapunda, wakati wa kuagwa mwili wa marehemu, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, jana. Shaka alimuwakilisha Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka akimpa pole aliyekuwa Mume wa Marehemu Teddy Mapunda, Nestory Mapunda, wakati wa kuagwa mwili wa marehemu jijini Dar es Salaam, jana
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka akiwa na waombolezaji wengine wakati wa kuagwa mwili wa marehemu Teddy Mapunda, jijini Dar es Salaam, jana
Padre akiendesha misa ya wafu, wakati wa kuagwa mwili wa marehemu Teddy Mapunda jijini Dar es Salaam.
Mtoto wa Marehem Teddy Mapunda akizungumza kwa niamba ya familia, wakati wa kuaga mwili wa marehemu mama yake, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye tukio la kuaga mwili wa marehemu Teddy Mapunda jijini Dar es Salaam.  

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages