Na Mwandishi Maalumu
MZEE wetu, Ally Hassan Mwinyi, alipata kusema haya: "Maisha ni hadithi tu, ewe mwanadamu kuwa hadithi nzuri.”
Hayati John Magufuli (JPM), Rais wetu wa Awamu ya Tano, ameondoka duniani akiwa tayari ameandika hadithi kubwa sana. Si jambo rahisi kuifuta labda ubomoe kila kitu alichowaza, alichofanya na alichojenga.
Vitu ni vingi sana alivyofanya kwa kipindi kifupi na hapa nitaorodhesha vichache tu vinavyojenga hadithi ya JPM
Katika kuvunja hadithi yake, anza na kuvunja zahanati takribani 400 alizojenga.
Mtetezi huyu wa wanyonge ameandika hadithi ya kujenga hospitali kwa wilaya zote ambazo hazikuwa na hospitali za wilaya na vituo vya afya zaidi ya 300 nchini baada ya kuvikuta vituo 67 tu!
Alipandisha bajeti ya dawa maradufu na sasa zinapatikana katika hospitali zote kulinganisha na zamani huku akisaidia kumaliza tatizo la dawa kupotelea hospitali binafsi.
Tanzania sasa ilikuwa inaelekea kwenye utalii wa kimatibabu kutokana na namna JPM alivyoendeleza kazi nzuri iliyoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete ya kuhakikisha tiba za Kibingwa zinapatikana nchini.
Kuondokana na hadithi ya Magufuli, ingia kwenye shule zote za sekondari za zamani alizozikarabati na kuzivunja. Usipofanya hivyo, kila tukiziona tumakumbuka.
Hayati Magufuli ameandika hadithi ya kutoa ruzuku kwenye elimu ili watoto wa maskini na matajiri wasome kwa shule za misingi na sekondari. Hivi sasa hakuna mtoto anayeshindwa kwenda shule kutokana na mzazi wake kutomudu gharama za elimu.
JPM amelala akiwa ameandika hadithi ya kujenga hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwapunguzia wanafunzi adha ya malazi.
Kuiharibu hadithi ya Hayati Rais John ni pale utakapofanikiwa kuvunja meli tisa kubwa mpya alizojenga ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Ziwa Victoria. Nenda uvunje na kutupilia mbali daraja la Busisi la Ziwa Victoria la kilomita tatu na nusu na daraja linalojengwa baharini la kilomita moja, pale Salender.
Kuharibu hadithi ya Hayati Magufuli labda uvunje madaraja mtambuko ya Ubungo na Tazara, kisha uvunje stendi za mabasi mpya na za kisasa alizojenga kila mikoa takribani yote 30.
Futa hadithi ya Magufuli kwa kuvunja masoko makubwa mapya ya kisasa aliyojenga katika mikoa yote 30 ya Tanzania, uvunje ndege 11 alizonunua, ubomoe reli ya kisasa ya umeme na reli ya kwenda Moshi na Arusha.
Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi ya kujenga mradi wa umeme mkubwa katika Bwawa la Mwalimu Nyerere unaozidi uwezo wa umeme wote unaozalishwa tangu mkoloni, Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete.
Mradi huu ambao Mbunge wa Msoma Vijijini anataka tuuvunje, utalihakikishia taifa kutokuwa tena na upungufu wa umeme wakati tunapoendelea kuita wawekezaji zaidi.
Akina Muhongo wamesahau haraka sana mambo yaliyolitesa taifa letu katika sekta ya umeme kupitia ‘madude’ mumiani kama Richmond, IPTL, Dowans mtoto wao Escrow!
Sambamba na hilo, JPM wakati anaingia madarakani ni vijiji 2018 tu ndivyo vilikuwa na umeme lakini hadi anaondoka duniani tayari vijiji 9750 vilikuwa na umeme, tena ukisambazwa kwa gharama ndogo ya shilingi 27,000 tu. Kabla yake gharama za mtu kuwekewa umeme kijijini ilikuwa Sh 450,000.
Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi ya kujenga reli ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kwenda kwa haraka na kubeba mzigo mkubwa kuliko reli zote nchini. Tutakuwa na treni ambayo itatumia saa moja na nusu kutoka Dar hadi Morogoro na saa takribani tisa tu toka Dar es Salaam hadi Mwanza. Kwa vipimo vyovyote vile treni hii itaharakisha sana maendeleo yetu.
Hivi unapata picha gani sehemu ambayo mtu alitumia saa 17 (Mwanza- Dar) sasa atatumia saa tisa tu? Ngoja ikamilike muone namna ambavyo itakuwa nguvu kuvunja hadithi ya JPM, labda mkiamua kutoiendeleza na kuicha kama gofu.
Kinachovutia ni kwamba Rais wetu mpendwa, Samia Suluhu Hassan, kasema miradi hiyo ni urithi alioachiwa, lazima ataiendeleza. Hongera mama yetu kwani wanaotaka kuvunja hadithi ya JPM hawatafanikiwa.
Hayati Magufuli ameandika hadithi ya kujenga maghala ya kutunzia vyakula kwa mikoayote inayozalisha vyakula kwa hifadhi za taifa letu. Sasa Taifa litakuwa na hifadhi ya kutosha ya mazao ya chakula.
Ameandika hadithi ya kufufua shirika la ndege ili taifa letu liwe na kitu kinachobeba bendera yetu na kututangaza hata kama tutachelewa kupata faida.
Sasa tunashuhudia watalii wakitua nchini licha ya corona na ndege hizi zinasaidia sana kwa usafiri wa ndani na baadaye tutatoka nje. Lakini kuna watu ambao walibeza ununuzi wa hizi ndege, sasa wanataka kufuta hii hadithi!
Magufuli ameandika hadithi ya kumalizia miradi iliyoanzishwa na watangulizi wake ambayo ilikwama kuendelea baada ya pesa ‘kupigwa’ ama ujenzi usioridhisha kuanzia barabara, madaraja, viwanja vya ndege vya zamani na vipya na mengine kibao.
Magufuli ametoa somo kubwa kwa marais wa Afrika kuhusu kusimamia raslimali zetu kama waafrika na kwamba inawezekana, lakini ni hadithi ambayo kuna watu inawakera, wanataka kuivunja.
Ameandika hadithi ya kudhibiti raslimali zetu na kielelezo ni ujenzi wa ukuta wa Mererani na maduka ya madini yaliyojazana nchi nzima. Ukitaka kumaliza hadithi yake, kavunje hayo maduka na ukuta wa Mererani.
Ameandika hadithi ya kutekeleza wazo la Baba wa Taifa la kuhamia Dodoma, tena katika kipindi ambacho hakikuzidi miaka mitano. Amesababisha Dodoma imepanuka bila kuathiri maendeleo ya jiji la Biashara la Dar es Salaam.
Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi ya kuwa mzalendo wa kweli kwa nchi yake, kwamba lazima tujivunie nchi yetu.
Mara tu baada ya kuapishwa, Magufulia aliandika hadithi ya kutumbua viongozi waliokuwa wakifiriki kwa matumbo yao na siyo kwa akili zao, akasafisha uozo katika sekta ya umma, akarejesha uadilifu serikalini na kusafisha kwa kiwango kikubwa ufisadi.
Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi ya kukomesha watumishi hewa serikalini na watumishi wenye vyeti feki na kuokoa mabilioni ya fedha yaliyokuwa ‘yakipigwa’.
Alikuwa mkali sana katika hilo na ukitaka kujua muulize Anne Kilango Malecela alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuutangazia umma kwamba mkoani kwake hakukuwa na wenye vyeti feki wakati si kweli.
Hayati Magufuli ameandika hadithi ya usimamizi madhubuti wa mapato ya Serikali, sasa taasisi za serikali zinajiendesha kibiashara na si kihasara kama ilivyokuwa awali ilipokuwa ni ulaji tu wa pesa, upigaji dili, taasisi zinakufa, hakuna gawio kwa serikali lakini sasa zinatoa gawio.
Ameacha somo kwamba kila kitu ni usimamizi imara, ukicheka na kima utavuna mabua.
Hayati Rais Magufuli ameandika hadithi ya kutuondolea kile kilichoaminika kwamba mwenye pesa anaweza kufanya chochote. Anaweza kukudhulumu lakini wewe ndiye ukaonekana mkosaji, badala yake akapindua meza kwamba mwenye pesa anaweza kufanywa chochote. Hayakuwa maneno matupu bali tumeshuhudia!
Ndani ya miaka mitano tu aliandika hadithi ya kutandaza miradi mingi nchi nzima inayoonekana kwa macho na sio miradi hewa ama ya kitapeli kama miradi tuliyowahi kuisikia siku za nyuma. Mingi nimeshaitaja hapo juu.
Ameandika haditi za kujenga hosteli za Askari Magereza na kota za Magomeni takribani ghorofa 30 zenye ghorofa 10 kwenda juu.
Hayati Magufuli ameandika hadithi ya uwezeshaji ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga na sasa, siku chache baada ya kifo chake, Rais Samia Suluhu Hassan amesaini kuanza rasmi kwa ujenzi wa bomba hilo baada taratibu zote kukamilika.
Miaka yote maeneo ya Mbezi na Kimara walikuwa hawapati maji japo yanapita njia hiyo hiyo lakini sasa maji yamefika Mbezi. Zote hizo ni hadithi za Magufuli. Awali waliokuwa wanakula hela za wananchi ni wenye miradi ya kuuza maji kwa magari.
Yaani, Magufuli kaandika hadithi nyingi sana ambazo wanaotaka kuzifuta, watapata shida sana. Kimsingi hawataweza. Na hapo sijataja namna alivyoiingiza nchi kwenye uchumi wa kati katika kipindi kifupi sana.
Kama alivyosema mwenyewe, wengi tutaendelea kumkumbuka kwa mazuri na wachache kwa mabaya.
Makala haya yalianza kuonekana kwa mara ya kwanza yakiwa hayako katika mtiririko huu kwenye mtandao wa Jamii Forum.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇