LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 29, 2021

MABALOZI WA TANZANIA DUNIANI KOTE, WATAKIWA KUTAFUTA MASOKO YA UHAKIKA YA BIDHAA ZA HAPA NCHINI HUKO WALIKO

Na Mwandishi Maalum

Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Nchi za nje, wameagizwa kujipanga, kushiriki na kutafuta fursa zitakazowezesha bidhaa mbalimbali za Tanzania kupata masoko ya uhakika katika nchi walizopo


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi wakati akizungumza na Mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje leo jijini Dodoma.


Prof. Kabudi amesema hilo ni jukumu la lazima kwa mabalozi hao kwa kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambayo inaelekeza juu ya Diplomasia ya Uchumi pamoja na kuimarisha sauti ya Tanzania na taswira yake katika medani ya uhusiano wa Kikanda na Kimataifa.


Amesema, ili kufanikisha hilo Balozi zinapaswa kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya nyingine za Kimataifa zikiwemo, Indian Ocean Rim Association, Indian Ocean Tuna Commission, South South Commission na South West Indian Ocean Fisheries Commission.


Prof kabudi amewataka Mabalozi hao kuzingatia maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyoyatoa wakati akizindua Baraza la Wawakilishi ya kutaka kuhakikisha kuwa Uchumi wa Buluu kupitia uvuvi wa Bahari Kuu unakuwa na manufaa kwa Wananchi hususani katika kuongeza mapato, ajira na kukuza uchumi kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni ya Muungano.


Pia amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) katika maendeleo ya Taifa na kuzielekeza Balozi zianze na ziboreshe kanzi data ya Diapora ikiwa ni pamoja na kuwahimiza kuanzisha Jumuiya zao.


“Natambua kazi hiyo inaendelea na kwa sasa tuna data za Diaspora takriban 98,658 na kuna Jumuiya 77 za Diaspora. Nachukua fursa kusisitiza umuhimu wa Balozi zetu kuboresha na kuharakisha kazi hii kwa kubuni njia mbalimbali za kuwaandikisha," amesema Prof. Kabudi.


Mkutano huo wa Prof. Kabudi na Mabalozi hao umehudhuriwa pia na Naibu Waziri, William Tate Ole Nasha, Katibu Mkuu Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palagamba Kabudi akisisitiza jambo kwenye Kikao kazi na Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sehemu mbalimbali Duniani pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo kilichofanyika jijini Dodoma, leo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. William Tate Olenasha (Mb) akizungumza na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoiwakilisha nchi sehemu mbalimbali Duniani pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo kwenye kikoa kazi kilichofanyika jijini Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Brigedia Jenerali Wilbert A. Ibuge akisisitiza jambo katika Kikao kazi katika ya Mhe. Prof Kabudi na Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sehemu mbalimbali Duniani pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo kilichofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Mabalozi na Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palagamba John Kabudi (Mb) kwenye Kikao Kazi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palagamba John Kabudi (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sehemu mbalimbali Duniani mara baada ya Kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages