………………………………………………………………………………….
Na Tito Mselem Dodoma,
Imeelezwa kuwa Sekta ya Madini Imezidi kuimarika miaka ya hivi karibuni kutokana na juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kusimamia masoko na vituo vya kuuzia madini katika maeneo yote yanapopatikana madini nchini.
Hayo, yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko Machi 28, 2021 alipokuwa akijibu hoja kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Utawala Annex uliopo Bungeni jijini Dodoma.
Akizungumza katika Kamati hiyo, Waziri Biteko amesema kuwa, juhudi za kuanzisha na kusimamia masoko na vituo vya madini imesaidia kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ambapo mapato yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Pia, Waziri Biteko amesema kwamba, kasi ya ukusanyaji na mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka ambapo katika kipindi cha Julai 2020 mpaka Februari 2021 Serikali ilikusanya jumla ya shilingi bilioni 399.09 sawa na asilimia 113.73 ya lengo ya makusanyo kwa kipindi husika.
Aidha, Waziri Biteko amesema katika kipindi cha Robo Tatu ya Mwaka 2020 mchango wa Sekta ya Madini umekuwa kwa asilimia 6.4 na nimatumaini ya wizara kwamba lengo la kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 linafikiwa.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kuimarisha utendaji wa Sekta ya Madini na kuifanya sekta kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Sambamba na hilo, Prof. Msanjila ameishukuru Kamati hiyo kwa ushauri wake makini ambao imekuwa ikiutoa mara kwa mara katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kukuza mchango wake katika Pato la Taifa na ustawi wa Watanzania.
Pia, Prof. Msanjila amesema, Wizara ya Madini imeshaandaa timu ili kuanza kuandaa utekelezaji wa Kituo cha Utalii wa Madini ambapo madini yapatikanayo nchini yataoneshwa hapo ili yaweze kuongeza mapato yatokanayo na Rasilimali Madini.
Akijibu Swali la Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula, Prof. Msanjila amesema, katika kudhibiti utoroshaji wa madini ya dhahabu Wizara imesajili mialo yote ili kuhakikisha kiasi kinachozalishwa katika kila mwalo kinapelekwa kuuzwa katika masoko ya Madini yaliopo nchini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇