Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais Hayati Dk. John Magufuli
Na Bashir Nkoromo
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeitisha Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wake na Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole amesema kwamba Kikao hicho kinafanyika siku ya Jumamosi Machi 20, 2021, saa 8 mchana, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
"Kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipenzi chetu Dk. John Joseph Pombe Magufuli, Wazee wetu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Philip Mangula na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein wameshauriana na kukubaliana kifanyike kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM....", amesema Polepole.
" Aidha taarifa inatolewa kwamba Chama kitakuwa katika maombolezo ya siku 21sambamba na siku 14 zilizotangazwa na Serikali na bendera zote za CCM zitapepea nusu mlingoti", ameongeza Polepole aliyekuwa akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma, leo.
Amesema, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli, vitabu vya salam za maombolezo vitawekwa Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
Pia Polepole amtangaza kusimama kwa muda shughuli zote za uchaguzi ndani hadi taarifa itakapotolewa baadaye.
"Uongozi wa CCM unawaomba sana wanachama wote wa CCM, watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi, kuwa na moyo mkuu, kuendelea kuwa watulivu kusimama imara na kuendelea kutafakari mchango wa kipekee na wa kihistoria kwa taifa letu wa ndugu yetu na mpendwa wetu Dk. Johnh Magufuli", amesema Polepole, huku akimuomba Mungu kuiweka roho ya marehemu Dk. Magufuli kuiweka roho yake mahala pema peponi.
Shughuli za chama zihusianazo na uchaguzi ndani ya chama zinasimama kwa muda hadi taarifa itakapotolewa baadaye.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇