Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema mashamba 6,315 yanayoshikiliwa na watu kinyume na sheria yamegunduliwa katika kisiwa cha Pemba.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Dk Soud Nahoda Hassan ameeleza hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe kisiwani Pemba Habib Ali Mohamed aliyetaka kujua ni mashamba mangapi yametambuliwa wakati wa kazi ya kuyatambua mashamba yanayomilikiwa kinyume na sheria, na lini yatakabidhiwa kwa wananchi kwa shughuli za kilimo.
Dk Hassan amesema, mashamba hayo yalitambuliwa baada ya serikali kuunda timu ya kutafuta mashamba yaliyofichwa na kumilikiwa na wananchi kinyume na sheria.
"Wizara imefanikiwa kuyatambua jumla ya mashamba 6,315 kati ya mashamba 8,215 yaliyopo na kazi ya kuyatafuta zaidi inaendelea", alisema.
Kwa mujibu wa waziri huyo wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar asilimia 90 ya mashamba yaliyotambuliwa ni ya kilimo cha zao la karafuu na minazi na kazi ya kugawa mashamba hayo kwa wilaya ya Micheweni huko kisiwanin Pemba imekamilika.
Amesema mashamba 732 yapo katika hatua za mwisho kukabidhiwa wamiliki wapya baada ya kufanya maombi ya kuyamiliki na kuyaendeleza kwa kazi za kilimo.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇