Katika uchaguzi mkuu wa Uganda unaotarajiwa kufanyika Januari 14 mwakani una wagombea 11 wa nafasi ya Urais, 10 kati yao wakitaka kuchukua nafasi ya Yoweri Museveni wa chama tawala cha NRM anayetaka kutetea nafasi yake kwa muhula wa sita.
Orodha ya wagombea katika uchaguzi huo inajumuisha watu wa aina tofauti, kada tofauti na vizazi tofauti; wakileta mchanyato wa kipekee katika uchaguzi huo unaovuta hisia za wengi katika eneo la Afrika Mashariki na kwingineko duniani.
Rais Museveni aliyekaa madarakani tangu mwaka 1986 alipoingia madarakani kwa njia ya mapigano ya msituni, ni miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Afrika na mwangwi wa uchaguzi huu umevuka jiografia ya bara hili.
Ingawa Robert Kyagulanyi Ssentamu ndiye mgombea anayetajwa zaidi katika vyombo vya habari kutoka miongoni mwa wanaotaka nafasi hiyo kutoka vyama vya upinzani, wapo wagombea wengine wenye ushawishi miongoni mwa Waganda katika uchaguzi huo.
Ni kina nani hao wanaotaka kumshinda Museveni na kuchukua madaraka ya kuongoza taifa hilo lenye wananchi zaidi ya milioni 40?
Tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambazo haziruhusu wagombea binafsi, Uganda inaruhusu mfumo huo na katika kuangalia wasifu na ushawishi wa wagombea hao.
Wagombea wa vyama ni kina nani?
Norbert Mao (Democratic Party)
Mao ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Uganda, akiwa ameanza kupata umaarufu tangu angali mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere - akijulikana kwa uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja na kuongoza migomo ya wanafunzi.
Wakati alipochukua Uenyekiti wa DP; chama kikongwe zaidi cha siasa nchini Uganda, mnamo mwaka 2010, wapo waliodhani kwamba mwanasiasa huyo anayetoka Kaskazini mwa Uganda, angeweza kuja kuwa Rais wa taifa hilo katika miaka ya mbele.
Hata hivyo, nyota ya kisiasa ya mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 53 imepungua sana na sasa hadi wanachama wa chama chake wameanza kampeni ya kutaka kumng'oa katika cheo chake hicho.
Wakati anapewa wadhifa wake, matumaini ya DP chenye wafuasi wengi katikati ya Uganda yalikuwa kwamba ataongeza kura kutoka Kaskazini anakotoka na uwezo wake wa kuzungumza utavutia watu wengi zaidi kujiunga nao.
Ujio wa Kizza Besigye, kwanza na sasa Bobi Wine, kumemfanya awekwe nyuma kwenye mstari wa watu wanaoweza kuchukua nafasi anayoshikilia Museveni.
Pengine ndiye mwanasiasa mwenye ulimi mtamu zaidi katika siasa za Uganda na anazungumza lugha nne; Kiingereza, Kijaluo, Kiganda na Kinyankore kwa ufasaha.
Gregory Mugisha Muntuyera (Alliance for National Transformation)
Katika siasa za Uganda, hakuna mwanasiasa anayeheshimika kwa uadilifu na siasa za kiungwana kumzidi mwanajeshi huyu mstaafu aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).
Maarufu zaidi kwa jina la Mugisha Muntu, mwanasiasa huyu ni Jenerali wa nyota tano aliyejiunga na jeshi la msituni la NRA mara tu baada ya kumaliza Shahada ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Makerere.
Katika miaka ya nyuma, Muntu alikuwa kipenzi cha Museveni kiasi kwamba hata walipotofautiana wakati Rais huyo alipotaka kuondoa ukomo wa kikatiba wa kubaki madarakani, Museveni alimwondoa jeshini na kumpa uwaziri. Muntu alikataa cheo hicho cha Uwaziri.
Muntu ana sifa za kuwa Rais wa Uganda lakini tatizo lake kubwa ni kwamba Waganda wanamwona mpole mno na mtu ambaye kwa tabia hiyo hawezi kumshinda Museveni.
Mgogoro wake na wenzake katika chama alichokuwa awali cha FDC kiasi cha kuamua kuanzisha chama kipya pia kumempunguzia wafuasi.
Kugombea kwake ni muhimu kwa sababu ana wafuasi wengi Magharibi mwa Uganda ambako ndiko nyumbani kwa Rais Museveni.
Kama atapata kura nyingi katika eneo hilo, anaweza kusaidia kupunguza pengo kati ya Bobi Wine na mgombea huyo wa NRM.
Patrick Oboi Amuriat (Forum for Democratic Change-FDC)
Kabla ya ujio wa chama cha Bobi Wine cha NUP, FDC ndicho kilichokuwa kikichukuliwa kama chama kikuu cha upinzani kikiongozwa na Kizza Besigye.
Amuriat ambaye pia wafuasi wake humwita kwa jina la POA ikiwa ni ufupisho wa majina yake matatu, amejijengea jina kutokana na siasa zake za kuzungumzia matatizo ya wananchi na utatuzi wake badala ya kupiga porojo.
Ingawa ni mzaliwa wa Soroti, Mashariki mwa Uganda, Amuriat anafahamika sana miongoni mwa wananchi wa taifa hilo kwa sababu yeye ndiye alikuwa mkalimani wa mgombea urais wa chama cha upinzani cha DP, Paul Ssemogerere, katika mikoa ya Kaskazini mwa Uganda wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini humo mwaka 1996.
Tatizo lake kubwa katika uchaguzi huu ni kwamba anaingia katika mchuano huu baada ya mgogoro wa FDC uliosababisha kuondoka kwa Jenerali Muntu ambako kumefifisha nguvu za chama hicho. Ni wazi kwamba yeye na mwanajeshi huyo mstaafu watagawana kura.
Robert Kyagulanyi Ssentamu 'Bobi Wine' (National Unity Party -NUP)
Katika uchaguzi huu wa Uganda, huyu ndiye mgombea anayemnyima usingizi Rais Museveni kuliko wengine wote.
Umaarufu wake, umri wake na uungwaji wake mkono miongoni mwa vijana, ndiyo mambo yanayomtofautisha na wagombea wengine wote.
Mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 38, alijipatia umaarufu kwanza kama mwanamuziki - kwa kuimba nyimbo zilizokuwa zikipendwa na wengi wa wananchi wa kipato cha chini na sasa kama mpinzani jasiri wa Museveni.
Bobi Wine alisomea masuala ya muziki katika Chuo Kikuu cha Makerere na baadaye akajiunga na masomo ya sheria.
Kuondoa Rais Museveni, pengine yeye ndiye mgombea anayefahamika zaidi kwa Waganda kuliko mwingine miongoni mwa waliosalia.
Bobi ana bahati ya kutoka katika kabila lenye watu wengi zaidi (Baganda), dhehebu lenye waumini wengi zaidi (Wakatoliki) na kuwa katika rika lenye watu wengi zaidi miongoni mwa wapiga kura (miaka 18 -40) - ambalo linakusanya asilimia 80 ya wapiga kura wote wa Uganda.
Kama Mao ataweza kupata kura nyingi Kaskazini, Amuriat akapata kura za kutosha Mashariki mwa Uganda huku Muntu na Tumukunde wakiweza kupunguza kura za Museveni Magharibi mwa Uganda, Wine anaweza kuweka rekodi ya kupata kura nyingi kuliko mgombea mwingine yeyote wa upinzani katika historia ya Uganda.
Au, kinyume cha matarajio ya wengi, kuibuka mshindi katika uchaguzi huu.
Yoweri Museveni (National Resistance Movement - NRM)
Katika historia ya Uganda, hakuna Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko Museveni , amekuwa madarakani kwa takribani miongo minne.
Museveni mwenye miaka 76 ana nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huu kwa sababu ya muunganiko wa vitu vingi ikiwamo muundo wa tume ya uchaguzi, upendeleo wa vyombo vya dola kwake na ukweli kwamba chama chake pengine ndicho pekee kilichosambaa nchi nzima ya Uganda.
Rais huyo na chama chake pia kina rasilimali ya kutosha kuweza kununua matangazo kwenye vituo vya redio na luninga kufanya kampeni; katika uchaguzi ambao mikutano ya hadhara imezuiwa kwa sababu ya tishio la ugonjwa wa Corona.
Kwa sababu ya rekodi yake ya kuiongoza Uganda kwa amani kwa muda wote huo, kuna wanaoamini kwamba amani ya nchi hiyo inatokana na utawala wake na kwamba endapo ataondoka, nchi hiyo inaweza kujikuta ikirudi nyuma katika nyakati za kutawaliwa na madikteta wakatili kama Idi Amin.
Baada ya kutazama wagombea hao watano ambao wanaingia katika kinyangányiro hicho kwa kutumia vyama vyao, sasa tumulike wagombea binafsi. Katika mabano ni umri ambao kila mgombea binafsi anao.
John Katumba
Huyu ndiye mgombea mwenye umri mdogo kuliko wote katika uchaguzi huu wa Uganda, Katumba ana umri wa miaka 24. Ajenda yake kubwa katika uchaguzi huu ni kupambana na tatizo la ajira linaloathiri vijana wengi.
Tatizo kubwa alilonalo kijana huyu ni kwamba mambo yake mengi yanaonekana kama hadithi za kutunga tu na hayana ukweli. Kwa mfano, Waganda bado wanajadili ni kwa vipi mtu ambaye hana ajira ya uhakika ameweza kupata shilingi milioni 20 za nchi hiyo kwa ajili ya kuchukua fomu ya urais.
Ingawa mwenyewe amekuwa akidai kwamba alikuwa na "kibubu" cha kuhifadhia fedha nyumbani kwake, jambo hilo limeshindwa kuaminika na wengi. Tatizo lingine ni kwamba haijulikani mahali anapoishi na hata wazazi wake hawajulikani - mwenyewe akidai kuwa walifariki wakati akiwa na umri wa miaka miwili tu.
Si mgombea makini zaidi ya kuchangamsha tu uchaguzi huu.
Nancy Kalembe (40)
Huyu ndiye mgombea urais pekee mwenye jinsia ya kike katika uchaguzi huu. Alijulikana na Waganda wengi wakati akiwa mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Taifa (UBC) katika miaka ya nyuma na aliwahi kushiriki mashindano ya urembo ya Miss Uganda ambako aliingia katika tano bora.
Sera yake kubwa katika uchaguzi huu ni inahusu kupambana na rushwa na kutoa uongozi usio na upendeleo kwa kabila moja au watu kutoka katika eneo moja la taifa lao.
Tatizo lake kubwa katika uchaguzi ni kuwapo kwa wagombea wengine wanaokubalika kuliko yeye na pia ukosefu wa fedha.
Tangu kuanza kwa kampeni, mikutano yake kadhaa imeahirishwa kwa yeye kushindwa kufika. Pia, nusura aondolewe na Tume ya Uchaguzi ya Uganda kwenye uchaguzi baada ya kushindwa kupata shilingi milioni 20 za nchi hiyo alizotakiwa kuweka kama dhamana ya wagombea wote.
Jenerali Henry Tumukunde (61)
Miongoni mwa wagombea binafsi katika uchaguzi wa Januari 14, 2021, mwanajeshi huyu mstaafu ana historia ya peke yake. Alikuwa katika vita ya msituni pamoja na Museveni wakitaka kumpindua Obote na baadaye Tito Okello.
Baada ya kuingia madarakani, Tumukunde alikuwa Mkuu wa Usalama wa Jeshi la Uganda - huku mmoja wa maofisa wa chini yake akiwa Paul Kagame; Rais wa sasa wa Rwanda.
Alipanda vyeo kiasi cha kuwa Waziri wa Usalama na Mkuu wa Idara ya Usalama wa Ndani (ISO) wa Uganda.
Kama ilivyokuwa kwa Muntu, Tumukunde alikorofishana na Museveni baada ya kumpinga Rais huyo wa Uganda wakati alipokuwa akitaka kubadili Katiba ya Uganda ili aendelee kubaki madarakani.
Msimamo wa Tumukunde ulikuwa kwamba kufanya hivyo ni kusaliti misingi ya kilichowafanya waende msituni kupambana na serikali zilizokuwa madarakani takribani miaka 40 iliyopita.
Misimamo hiyo ya mwanajeshi huyo ilisababisha afunguliwe mashitaka mbalimbali na kuwekwa kizuizini kabla ya kuachiwa na kupewa uwaziri na Museveni tena. Hata hivyo, walikorofishana tena mwaka juzi na sasa askari huyu anataka kuchukua wadhifa wa swahiba wake huyo wa zamani.
Uwezekano wa yeye kushinda ni mdogo kwa sababu Bobi Wine anaonekana kuungwa mkono zaidi yake. Umuhimu wake katika uchaguzi huu ni kwamba kwa kuwa anatoka katika eneo analotaka Museveni, anaweza kupunguza kura za rais huyo na hivyo kumsaidia Wine.
Joseph Kabuleta (48)
Nchini Uganda, mgombea huyu alijipatia umaarufu mkubwa kama mmoja wa waandishi na wachambuzi wa masuala ya michezo - akifikia kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo wa Uganda miaka michache iliyopita.
Hii ni mara yake ya kwanza kujitokeza kuwania nafasi hii na ajenda yake kubwa ni kuhakikisha sekta ya kilimo nchini humo inakuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo.
Hata hivyo, si watu wengi wanamchukulia kwa umakini mkubwa kwa sababu ya kudaiwa kuwa na tabia za ushaufu na aliwashangaza Waganda baada ya kukubali kupigwa picha akiwa anabusu viatu vya mmoja wa wachungaji wa makanisa mapya ya Kiinjilisti nchini humo.
Mchungaji Fred Mwesigye (38)
Miezi michache iliyopita, hakuna mtu aliyekuwa amewahi kusikia jina la mgombea huyu lakini hatua yake ya kujitokeza kuwania urais imemfanya awe maarufu ghafla.
Ajenda zake kubwa ni kufanya Uganda kuwa taifa linaloendeshwa kidini, kuongeza mishahara ya askari na kupunguza gharama za matumizi ya serikali ili kuongeza uwekezaji kwenye kutatua kero za wananchi.
Hapewi nafasi ya kushinda.
Willy Mayambala (33)
Mgombea huyu ni mhandisi kitaaluma. Baba yake alikuwa mmoja wa watu waliokwenda msituni kujiunga na majeshi ya NRA ya Yoweri Museveni yaliyokuwa yakipambana dhidi ya Obote.
Hapewi nafasi kubwa ya kushinda na tayari ametangaza kwamba kwa sababu ya ukata, ataweza kufanya kampeni kwa siku 43 tu badala ya 65 zilizowekwa kikatiba kwa ajili ya kampeni.
Hapewi nafasi kushinda na hana ushawishi miongoni mwa wananchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇