Mbunge wa Jimbo la Madaba mkoani Ruvuma Joseph Mhagama akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lilondo jana kwa ajili ya kuwashukuru kutokana na kukipa kura nyingi chama cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba,pia alitumia mkutano huo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha awamu ya tano ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli
……………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Madaba
MBUNGE wa jimbo la Madaba Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma Joseph Mhagama,ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya na jitihada inazofanya za kuimarisha huduma za afya katika jimbo hilo.
Mhagama ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti, wakati wa mikutano yake ya kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba pamoja na kuhimiza shughuli za maendeleo katika vijiji na kata mbalimbali .
Amesema, kimsingi fedha hizo zinakwenda kuimarisha na kuboresha huduma za afya hasa ikizingatia kuwa katika jimbo hilo hakuna hospitali kubwa ya wilaya, badala yake wananchi wanategemea kupata matibabu katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo.
Amesema, wananchi wa Madaba hawana budi kumshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kazi kubwa aliyowafanyia ya kupeleka maendeleo na kusisitiza kuwa,heshima pekee wanayoweza kumpa Rais Magufuli ni kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi inayobuniwa na kutekelezwa na serikali ili kuleta tija.
Amesema mbali na fedha za ujenzi wa Hospitali ya wilaya, awali serikali ilishatoa shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Madaba na Mtyangimbole ambavyo vimeshakamilika na sasa wananchi wameanza kupata huduma za matibabu.
Pia amesema, serikali kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini Tarura imeanza ukarabati wa barabara ya Madaba kwenda Ifinga kata ya Matumbi yenye urefu wa km 48 ambayo wakati wa masika ilikuwa haipitiki kwa urahisi na hivyo wananchi kukosa huduma ya usafiri na kushindwa kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.
Mhagama, amewataka wananchi wa jimbo la Madaba kuwa wazalendo na kuiga mfano wa Rais Dkt Magufuri ya kufanya kazi kwa kujituma ili kuondokana na hali ya umaskini, badala ya kuwa vibarua na kufanya kazi katika mashamba ya watu kutoka nje, jambo linaloweza kuchangia umaskini na hatari kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Aidha amewatahadharisha, kuepukana na tamaa ya fedha kwa kuuza ardhi yao kwa wageni ambapo amewahimiza vijana kutumia fursa ya ardhi iliyokuwepo kupanda miti na kulima mazao mbalimbali ya biashara na chakula ikiwemo zao maarufu la Parachichi ambalo lina soko kubwa hapa nchini.
Amesema, vijana kama nguvu kazi ya Taifa ni lazima watumie rasilimali ardhi kujikwamua na umaskini na kuacha tabia iliyozoeleka kulalamika na wengine kutumia muda wakazi vijiweni kucheza pool huku jukumu la uzalishaji mali wakiachiwa wazee, jambo linalopaswa kukemewa vikali.
“uchaguzi umekwisha, kwa hiyo ni lazima watu hasa vijana wajikite katika uzalishaji mali badala ya kuendelea kukaa vijiweni kupiga porojo zilizokuwepo wakati wa uchaguzi mkuu katika jimbo letu hatutaki kuona watu wakilalamika kwa kukosa ela kwani kuna fursa kubwa ya ardhi inayostawi mazao mbalimbali”alisema.
Mhagama ,amewataka vijana kutambua thamani ya maisha yao ni juu yao wenyewe na hakuna mtu anayeweza kutoka mbali kuja kuwasaidia fedha, bali juhudi zao ndizo zitakazo wainua kimaisha na kupata fedha kwa ajili ya kuhudumia familia zao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba Theophanes Mlelwa alisema, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, kazi iliyobaki ni madiwani na watendaji wa serikali kuhakikisha wanashirikiana kutatua kero na changamoto za wananchi ili kuharakisha maendeleo.
Mlelwa ambaye ni diwani wa kata ya Wino, amewataka wananchi wa kata ya Wino na jimbo la Madaba kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa uchaguzi wa mwezi Oktoba na kuungana pamoja kuijenga Madaba yao ambayo inahitaji ushirikiano na umoja wa wananchi wote na sio kuiachia serikali.
Alisema, licha ya kuwa diwani wa kata hiyo, katika uongozi wake atahakikisha ana tenda haki kwa watu na kata zote na kuwataka wakazi wa kata ya Wino kutumia nguvu na maarifa kumaliza baadhi ya changamoto zilizokuwepo na pale watakapo shindwa basi halmashauri yao itaangalia namna ya kuwasaidia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Songea Nelly Duwe amesema, chama kina imani kubwa na Mbunge mteule Joseph Mhagama na diwani wa kata ya Wino Theophanes Mlelwa kutokana na uchapakazi wao,hivyo kuwataka kutobweteka na mafanikio baada ya kupita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu.
Amesema, hatua ya kupita bila kupingwa kwa viongozi hao wawili ni ishara kwamba wanakubalika kwa wananchi,kwa hiyo ili kudhihirisha hilo ni lazima wahakikishe wanashirikiana na wananchi wao kumaliza kero ambazo zinahitaji umoja wa pande zote mbili.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇