Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo CP Liberatus Sabas akitoa Rpoti ya Jeshi la Polisi Nchini kwa mwaka huu wa 2020 unaomalizika.
Na CCM Blog
Licha ya ya watu 1158 kufa na 2089 kujeruhiwa kati ya Januari hadi Novemba mwaka huu, kutokana na ajali za barabarani, Jeshi la Polisi nchini limesema kiwango cha ajali za barabarani kwa mwaka huu kimepungua kwa asilimia 33.9 ikilinganishwa na mwaka jana.
Akitoa ripoti ya Jeshi la Polisi Nchini kuhusu matukio mbalimbali yaliyojiri katika kipindi cha mwaka huu wa 2020, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo CP Liberatus Sabas amesema, kati ya Januari hadi Novemba 2019 matukio ya ajali yalikuwa 2722, ajali zilizosababisha vifo ni 1117, waliokufa ni 1329 huku majeruhi wakiwa 2717.
Alisema mwaka huu kuanzia Januari hadi Novemba 2020 matukio ya ajali ni 1800, ajali za vifo 935, waliokufa 1158 na majeruhi 2089, na kwamba kulingana na takwimu hizo mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana yamepungua matukio 922 ya ajali, sawa na 33.9%, ajali za vifo 182 sawa na 16.3%, waliokufa 171 sawa na 12.9% na waliojeruhiwa 628 sawa na 23.1%.
Kamanda Sabas amesema, wakati matukio mbalimbali yameonyesha kupungua lakini miongoni mwa matukio yalioshika kasi na nafasi kubwa mwaka huu ni kuungua kwa majengo ya shule na sababu za matukio hayo ya zikiwa ni migogoro mashuleni, hitilafu za Umeme na uzembe, huku shule za watu Binafsi/Taasisi za Kidini zikiwa jumla 20 na za Kiserikali zikiwa ni 11 na kufnya idadi ya jumla ya shule 31 zilizoungua toka Januari mpaka Novemba mwaka huu.
Kuhusu hali ya Ulinzi na Usalama wa Nchi, Kamishna Sabas amesema, hali imeendelea kuwa shwari kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, pia Jeshi limepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wapenda amani au raia wema ambao wamekuwa wakitoa taarifa za uhalifu pamoja wahalifu kwa Jeshi la Polisi nchini licha ya kuwa yapo matukio machache yamekuwa yakijitokeza ambayo ni tofauti na matukio ya kipindi cha nyuma.
Upande wa unyang’anyi wa kutumia silaha (Ujambazi), Kamishna Sabas amesema, Jeshi la Polisi kwa mwaka huu limefanikiwa kupunguza makosa ya ujambazi wa kutumia silaha kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma na mwaka jana.
Amesema, kuanzia mwezi Januari hadi Novemba (2019) kulikuwa na makosa 378 huku mwaka huu kuanzia Januari hadi Novemba (2020) yamepatikana makosa 273 ya kutumia silaha hii ikiwa ni tofauti ya makosa 105 sawa na asilimia 27.
Kuhusu mauaji, Kamishna Sabas amesema, kwa kiasi kikubwa mauaji yanayotokea kwa sasa nchini yanatokana na wivu wa mapenzi na wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Amesema, kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi kutokujichukulia sheria mkononi huku likiwataka viongozi wa dini kuingilia kati katika kutoa elimu ili kusaidia kupunguza mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi kwani wengi ni waumini wa madhebu yao na wanawasikiliza sana.
Kamishna Sabas amesema pia kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kuacha shule na kwenda kujiunga na makundi ya kihalifu, miongoni mwa waalifu hao ni wale waliokuwa Kibiti na hatimae baada ya kupigwa na Jeshi la Polisi kwa kushilikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama walikimbilia nchi jirani ya Msumbiji.
Kamishna Sabas amesema hadi sasa wapo wanafunzi waliokuwa wameacha shule na kujiunga na vikundi vya kihalifu ambao wamekamatwa wakiwa wanavuka kuelekea nchini Msumbiji na wengine tayari wameishafanikiwa kuvuka kuingia nchini humo.
Aidha Kamishna Sabas amesema, licha ya Jeshi la Polisi kuwataka wazazi kuwalinda na kufuatilia mienendo ya watoto wao amewataka wananchi kuchukua tahadhali wakati huu wa kuelekea Sikukuu za mwisho wa mwaka kwani Jeshi la Polisi kwa kushilikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamejipanga kikamilifu kukabiliana na uhalifu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇