Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani baada ya basi la abiria kupinduka katika mteremko wa Kumnyange uliopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.
Ajali hiyo ambayo imetokea tarehe 24 Oktoba, 2020 pia imesababisha watu 18 kujeruhiwa.
Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig. Jen Marco Gaguti na amemtaka kufikisha salamu za pole kwa familia za Marehemu, ndugu, jamaa na wote walioguswa na vifo hivyo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kuungana na familia zao.
“Nimesikitishwa na vifo vya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, nawapa pole wafiwa wote na nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majozi” Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva wa magari kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Pia amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kuchukua hatua dhidi ya watumiaji barabara wanaokiuka sheria za barabarani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇