LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 24, 2020

KWA MARA YA KWANZA TANZANIA INAFANYA UCHAGUZI BILA KUTEGEMEA MSAADA WA NJE


Kituo cha kupigia kura
Maelezo ya picha,

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba 28

Bajeti ya uchaguzi ni moja kati ya masuala ya msingi zaidi ambayo huenda yakachangia shughuli za uchaguzi kwenda kwa uafinisi ama kusuasua.

Katika uchaguzi wa nchi nyingi zinazoendelea hasa Barani Afrika, fedha za kuendesha shughuli nzima ya uchaguzi huegemea zaidi michango na misaada kutoka nchi zilizoendelea ama mashirika makubwa duniani kama benki ya dunia na mashirika ya kimataifa.

Na kiasi kingine cha fedha hutolewa na serikali ya nchi husika.

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi huu Oktoba 28. Na tofauti na miaka iliyopita, bajeti ya uchaguzi ya mwaka huu inatolewa yote na serikali ya Tanzania.

Bila kusubiri msaada wa mashirika wa nchi za nje, Tanzania ilitangaza kuwa uchaguzi utagharamiwa na serikali ya nchi hiyo kwa asilimia 100.

Kwa mujibu wa tume ya taifa ya uchaguzi NEC Serikali ya Tanzania imetenga kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 331 wakati wa uchaguzi, na maandalizi ya uchaguzi yakigharimu shilingi za kitanzania bilioni 157.

Mkurugenzi wa uchaguzi kutoka Tume ya taifa ya uchaguzi Dr Wilson Mahera amesema kuwa tayari serikali imetoa fedha zote za kuendesha uchaguzi huu.

''Hadi sasa tumepewa fedha kwa asilimia kubwa, hatujaenda kuomba nje na mataifa ya nje yanasema vipi mbona hamuji kuomba?''

Kwa upande wa Zanzibar, Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Thabit Idarous Faina amebainisha kuwa kwa mara ya Kwanza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetumia bajeti yote ya Uchaguzi kwa ukamilifu bila kutumia fedha zozote kutoka kwa wafadhili.

Uchaguzi

Hali ilikuaje chaguzi zilizopita?

Uchaguzi wa mwaka 1995 uligharamiwa na serikali pamoja na wafadhili. Lakini kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya taifa ya uchaguzi NEC kwa uchaguzi wa mwaka 1995, bajeti ilisuasua kutokana na kubadilika kwa sharia hivyo NEC walipaswa kutoa zaidi ya matarajio yao. Na pia masuala ya kifedha na bajeti ya uchaguzi ilipangwa mwaka 1994 hivyo ilivyofika wakati wa uchaguzi machache yaliweza kubadilika.

Changamoto nyingine iliyokumba uchaguzi wa mwaka 1995, ni serikali ya Tanzania kusuasua kupeleka fedha kwa wakati kwa tume ya taifa ya uchaguzi.

Kwa Mujibu wa ripoti ya NEC 2001, katika uchaguzi wa mwaka 2000 Tume ya taifa ya uchaguzi ilijipanga vizuri kutokana na mafunzo waliyoyapata kupitia matatizo yalitokea katika uchaguzi wa mwaka 1995.

NEC iliandaa bajeti mwaka 1998 na kupata fedha kutoka serikali na nyingine ikitoka kwa wafadhili waliokusanya kupitia shirika la Kidanishi.

Kwa miaka mingine ya uchaguzi wa Tanzania, 2005,2010 na 2015 fedha za bajeti ya uchaguzi ilitolewa kwa kiasi kikubwa na serikali lakini pia wafadhili na mashirika ya kimataifa.

Wapigakura

Kwa upande wa uchaguzi wa serikali ya mapinduzi Zanzibar na kwa mujibu ripoti ya uchaguzi ya ZEC mwaka 1995, zaidi ya nusu ya gharama ya uchaguzi wa mwaka 1995 ilitolewa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na wafadhili wakachangia kupitia shirika la Kidanishi (DANIDA) na fedha nyingine ikiwa na kiasi cha dola za Kimarekani 13,500 zikitoka serikali ya Uingereza na kukabidhiwa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Hivyo hivyo kwa uchaguzi wa mwaka 2005, 2010 fedha zilitoka kwa wafadhili, mashirika ya kimataifa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.

Ina maana gani kujitegemea kifedha?

Suala kuu la kujitegemea katika uchaguzi linaonekana kuwa ni kupunguza msukumo kutoka kwa wafadhili wa kufanya maamuzi kutokana na kulipa fadhila ya gharama za uchaguzi.

'' Tunataka kuwa huru ili tuweze kusimamia uchaguzi wetu bila masharti, na hizi zote tumezipokea kutoka serikali ya awamu ya tano'' anasema mkurugenzi wa uchaguzi kutoka tume ya taifa ya uchaguzi Dkt.Wilson Mahera.

Kama ilivyo kwa Tanzania kuna baadhi ya nchi za Afrika kwa mara ya kwanza wamejigharamia bajeti za uchaguzi.

Katika uchaguzi uliopita wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo nayo Serikali ilitanganza kujitegemea kwa asilimia 100.

Msemaji wa serikali Lambert Mende aliiambia Reuters kuwa hakuna nchi duniani inataka kuingiliwa katika kufanikisha zoezi la uhuru.

Aidha Mende aliongeza kuwa hawataki kuigiliwa katika masuala ya demokrasia, kama wanataka kutoa msaada basi wapeleke katika sekta nyingine kama Afya na elimu.

Kwa upande wa Burundi, hadi mwaka 2015 walikua wakitegemea wafadhili kugharamia uchaguzi , baada ya Rais Nkurunzinza kushinda muhula wa tatu na kutokea kwa machafuko nchini humo, wafadhili wakasitisha kutoa misaada.

Aliyekua waziri wa mambo ya ndani Pascal Barandagiye, serikali itakusanya michango nyumba kwa nyumba hadi fedha ya uchaguzi ipatikane.

Katika harakati za kuchangia fedha hizo haki za binadamu zilikiukwa nchini Burundi. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la haki za binadamu la Human rights watch vikosi vya usalama vilikua vikilazimisha watu kulipa mchango huo kwa kutumia nguvu na kuchangia zaidi ya mara moja.

Kwa nchi hizi za Afrika, mara nyingi hutemegemea misaada kutoka kwa wafadhili na mikopo kutoka mashirika makubwa duniani.Swali kubwa linabaki, Je Kuanza kujitegemea katika suala la msingi kama uchaguzi hutasaidia nchi hizi kuacha utegemezi wa kiuchumi?

Maelezo ya sauti,

Je tume ya uchaguzi iko tayari kwa mchakato huu muhimu wa Demokrasia?


Imeandikwa 

Na Munira Hussein

  • BBC Swahili Dar es salaam

 


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages