Ukonga, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, amewaomba watanzania wasifanye majaribio ya uongozi wa nchi kama baadhi ya vyama vinavyoendelea kuwalaghai kwa kuomba kujaribiwa.
Dk. Bashiru ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa kampeni za CCM, uliofanyika jana, katika jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam.
“Hakuna Chama kingine mpaka sasa tunapozungumza chenye uzoefu na uwezo wa kulinda umoja, upendo na mshikamano wa Taifa hili isipokuwa CCM.
Ndugu zangu, ninawaomba tusiwajaribu watu wasio na uzoefu, CCM inao uzoefu, inaweza kuwa na mapungufu fulani kwa kuwa ni Chama cha watu sio cha malaika, lakini katika eneo la kulinda uhuru, Usalama, amani, umoja, mshikamano wa kitaifa na muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Hakuna Chama kingine cha kukupa uhakika katika hayo isipokuwa CCM.” alisema Dk. Bashiru.
Katibu Mkuu amewataka pia wananchi kuwa makini na kuepuka vitendo vyoyote vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wakati huu wa kampeni, wakati na baada ya kupiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu kwa kuwa vitendo hivyo havitawanufaisha badala ya kuangamiza maisha yao.
Alisema Chuki, ghasia na vurugu vikishamiri hazichagui Chama, zitaathiri kila mmoja, hivyo ni muhimu wananchi wakati huu wa kampeni na watakapokwenda kupiga kura na baada ya kupiga kura kutazama kwa makini ni Chama kipi kinaweza kuwahakikishia usalama wao, na mpaka sasa CCM imedhihirisha inao uwezo huo kwa vitendo.
Pia Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza msimamo wa Chama na Mgombea Urais wa CCM Dk. John Magufuli wa kuendelea kuwajibu kwa hoja wapinzani licha ya wao kutumia matusi na kejeli, na kwamba dawa yao ni kutokuwapa wapinzania kura za Udiwani, Ubunge na Urais.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇