Kibaha, Pwani
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema Tanzania ni nchi huru na haipaswi kuingiliwa mambo yake na nchi nyingine yoyote Duniani, yakiwamo ya uchaguzi.
Dk. Bashiru amehusianisha kauli yake na historia iliyoandikwa Desemba 14, mwaka 1960, kufuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), kupitisha azimio la kuzipatia uhuru nchi na watu walioko kwenye ukoloni.
Mwanazuoni huyo alitoa msimamo huo mjini Kibaha katika mkoa wa Pwani, jana na kufafanua kuwa uamuzi huo uliofikiwa kwa nchi 89 kusema ndiyo na nchi tisa kupinga bila kuweka bayana kupitia kikao cha 15 cha baraza hilo, ndiyo msingi wa uhuru wa kisiasa wa nchi za Bara la Afrika unaoonekana leo.
Katibu mkuu huyo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza baada ya kukagua mradi wa kisasa wa Ujenzi wa Chuo cha Uongozi na Itikadi cha Mwalimu Julius Nyerere, kilichojengwa wilayani Kibaha, eneo la Kwa Mfipa.
"Bila kupitishwa kwa azimio hili, lililopewa Namba 1,514, tusingekuwa na haki hata ya kupiga kura, kwa sababu nchi haziwezi kuendesha uchaguzi wa kidemokrasia chini ya ukoloni," alisema.
CHUO CHA UONGOZI
Alisema kutokana na ukweli huo, vijana wa Kiafrika na wa Kitanzania hawana budi kujifunza historia, kazi inayokwenda kufanywa kwa ufanisi mkubwa na Chuo cha Uongozi na Itikadi cha Mwalimu Julius Nyerere, kikiwalenga watumishi wa umma na wanasiasa.
Dk. Bashiru alisema chuo hiko ambacho tayari ujenzi wake umekamilika, kitakuwa nyenzo ya kujifunza barabara historia, misukosuko, vikwazo na changamoto zinazotokana na mfumo wa kibeberu na taratibu za ubaguzi wa rangi.
"Hata kauli mbiu ya Chuo hiki, imeandikwa pale nje, kwamba: Someni barabara historia, ukiielewa barabara historia utaepuka vikwazo na dhambi za ubeberu na ubaguzi wa rangi' imeandikwa kwa Kiingereza ambapo ni maneno ya Mwalimu Nyerere, mwaka 1972," alisema.
Alisema huo ni urithi na falsafa muhimu kwa kizazi cha sasa na kwamba hata jina la Chuo hicho, halijaitwa kwa bahati mbaya, bali ni makubaliano ya vyama vyote sita vilivyoshirikiana kukianzisha hapa nchini.
Dk. Bashiru alivitaja vyama hivyo na nchi vinakopatikana kwenye mabano kuwa ni SWAPO (Namibia), FRELIMO (Msumbiji), ZANU-PF (Zimbabwe), MPLA (Angola), ANC (Afrika Kusini) na mwenyeji CCM.
"Vyama hivi viliafikiana kuita chuo hiki jina la Mwalimu kwa kuwa Mwalimu (Nyerere), alikuwa mwana historia mzuri, mwana falsafa mzuri, mwalimu mzuri, kiongozi mzuri na mwanasiasa bora katika Afrika na Dunia," alisema.
Aliongeza: "Kwahiyo kuja kwetu hapa ni kielelezo kwamba Chama Cha Mapinduzi na wanaCCM na vyama vya ukombozi vinavyoshirikiana katika mradi huu, vitaendelea kuenzi fikra, mchango na falsafa ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere," alisema.
Katibu Mkuu alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya China ambayo imekuwa mstari wa mbele kwenye kuhakikisha chuo hiko kimejengwa kupitia chama tawala cha CPC na kusema CCM itaendelea kuwa rafiki wa kweli wa chama hicho kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Alisema furaha ya CCM imeongezeka dhidi ya China kwa kuwa sasa ni mjumbe mmojawapo wa baraza la usalama la UN, mwenye uwezo wa kura ya turufu, ikiwa ni miaka mingi kupita, tangu Mtanzania, Dk. Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Umoja wa Mataifa, kupigania China na nchi zingine kwa hoja kupata nafasi iliyonayo sasa.
"Tangu China ilipoingia kwenye Umoja wa Mataifa, haijawahi kutuangusha, tunawashukuru sana wenzetu wa China; pia niwapongeze kampuni ya CRJE kutoka China na kampuni zingine zilizoshiriki kwenye ujenzi huu," alisema.
Dk. Bashiru alisema kampuni hiyo imetekeleza miradi minne ya kihistoria hapa nchini tangu kuasisiwa kwa mataifa haya mawili, ukiwemo mradi wa reli ya TAZARA (Uhuru), daraja la Nyerere, Kigamboni na Nyerere Square, yote ikiwa na uhusiano na kazi za Baba wa Taifa.
AWASHUKURU JK, KINANA
Katibu Mkuu Bashiru, pia alitumia hatuba yake kuwashukuru Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa maono yao ya kuanzishwa kwa chuo hicho cha itikadi na uongozi.
"Viongozi hawa ndiyo walioanzisha majadiliano na kufikia muafaka wa ujenzi wa chuo hiki katika vikao cha Chama na pia kujadiliana na vyama sita nilivyovitaja awali, kwahiyo wakati mimi nakabidhiwa ofisi, ndugu yangu Kinana alinikabidhi nyaraka zilizokuwa na muafaka wote, tayari kwa utekelezaji," aliongeza.
Alisisitiza: "Kwa hiyo, kupitia kwenu ndugu waandhishi wa habari niwashukuru sana viongozi wetu hawa na wote wa vyama tunavyoshirikiana navyo kutekeleza mradi huu ambao ni wazo zuri."
Alisema wazo hilo linakwenda kutekeleza nia ya Chama kuwa na vyuo vya aina hiyo, ambavyo awali vilikuwepo eneo la Kivukoni, Dar es Salaam, Lushoto mkoani Tanga na maeneo mengine kabla ya kutetereka na kurudishwa Serikalini.
"Sasa hivi tunatekeleza maelekezo ya Chama ya kuanzisha vyuo vya itikadi na uongozi vya Chama na hiki kitakuwa chuo kikuu cha ushirikiano wa vyama sita vya ukombozi, kwahiyo hapa tutawaandaa pia wakufunzi wa vyuo vingine ambavyo vitaanzishwa.
"Tayari kile cha Ihemi, kule Iringa na Tunguu kule Zanzibar vinafanya kazi hapa patakuwa sehemu ya kuimarisha vyuo hivyo na umuhimu wa kuwepo kwa vyuo hivi kunatokana na ukweli kuwa siasa ni msingi wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Dk. Bashiru, ziara yake ya jana chuoni hapo ni sehemu ya mwendelezo wa matukio ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 21 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ambaye alifariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999.
"Tarehe 14, hatutakuwa na tukio kubwa mbali na kampeni zenyewe, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi hii, hivyo leo (jana), nimetembelea chuo hiki kama mfululizo wa matukio yanayoendelea kufanyika maeneo mbalimbali, katika kuiadhimisha siku hiyo muhimu," alisema.
KAULI YA BALOZI WA CHINA
Naye Balozi wa China hapa nchini Wang Ke, akizungumza kwenye ziara hiyo, alisema Ubalozi wa China umefurahishwa na uamuzi wa kujumuishwa kwenye ziara hiyo kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 21 ya kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere.
Alisema kwa kumbukumbu zake, Julai mwaka 2018, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria shehere ya kuwekwa kwa jiwe la msingi ujenzi huo, iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais, Dk. John Magufuli, akishirikiana na makatibu wakuu wa vyama vingine vitano vya ukombozi.
"Katika tukio lile, nakumbuka pia Rais wa China, Xi Jinping, alitoa salamu zake na pia Waziri wetu wa Mambo ya Nje, alishiriki tukio lile la kuanza ujenzi wa chuo hiki muhimu," alisema.
Alisema CPC na CCM ni vyama rafiki vyenye historia ndefu na kwamba Ubalozi wa China, ambao umekuwa sehemu ya kufanikisha kukamilika kwa ujenzi huo, unaupongeza uongozi wa CCM kwa kusimamia vizuri mradi huo uliokamilika kwa ubora na wakati.
Balozi Wang, alisema wakati huu ambao Tanzania inaelekea kufanya Uchaguzi Mkuu, Ubalozi wa China unalitakia taifa kila la kheri na kwamba China ina iamini Tanzania kwenye kufanya uchaguzi huru, haki na unaotawaliwa na amani.
"Tangu Agosti, tumeshuhudia kampeni zenye amani, huru na usawa, tunawatakia Watanzania uchaguzi mzuri huru na haki na ubalozi wetu hauna shaka na uzoefu wa Tanzania kwenye kufanya chaguzi zake kwa msingi inayotakiwa," alisema.
Aliongeza kuwa urafiki wa China na Tanzania, ambao umejengwa kwenye msingi minne ya uhuru, usawa, heshima na kutoingiliana masuala ya ndani, utaendelea kudumu kwa miaka mingi ijayo kwenye masuala mbalimbali.
MRATIBU WA UJENZI
Kwa pande wake, Mratibu wa Mradi, Emmanuela Kaganda, alisema ujenzi ulianza Julai 17, mwaka 2018 na ulitarajiwa kukamilika Julai, mwaka huu, lakini umechelewa kwa miezi miwili kutokana na changamoto ya kunyesha kwa mvua nyingi zilizokuwa nje ya makisio na janga la corona lililoyakumba mataifa mengi duniani.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ulifanikisha upatikanaji ajira kwa Watanzania zaidi ya 3,000 na kwamba pia umekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwenye Wilaya ya Kibaha kutokana na ufikishwaji wa huduma muhimu za kijamii kwenye eneo la mradi, hivyo kuwanufaisha wakazi wengi wa Kibaha kwa Mfipa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇