Baadhi ya wananchi waliofika katika shule ya Mchepuo wa Kingereza ya Byamungu Islamic baada ya wanafunzi 10 katika shule hiyo kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo.
Alodia Babara, Kyerwa
Wanafunzi kumi (10) wa Shule Msingi ya Byamungu Islamic iliyopo katika Kijiji cha Itera Wilayani Kyerwa mkoani Kagera, wamefariki dunia na wengine 6 kujeruhiwa, baada ya bweni wa wavulana katika shule hiyo kuteketea kwa moto katika shule hiyo, wanafunzi wakiwa wamelala, usiku wa kuamkia leo.
Mkuu wa Shule hiyo, Selemani Abdu amesema bweni lililoungua lilikuwa na wanafunzi wa kiume 74 wenye umri kati ya miaka 6 hadi 13 katika shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 127 ambao ni mchanganyiko wa watoto wa kike na wa kiume.
Alisema baada ya kutokea moto huo mlezi wa wanafunzi hao anayelala nao bwenini alishtuka na kuona moto mkubwa ukiwaka ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada wakati akijitahidi kuwasaidia wanafunzi hao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyakahanga ya Wilayani Karagwe, Dk. Furaha Kahindo amesema hospitali hiyo imepokea maiti 10 na majeruhi sita na kati ya majeruhi hao, wawili hali zao siyo nzuri hivyo wanawapa rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera (Bukoba) au hospitali ya Rufaa Kanda (Bugando).
"Majeruhi wawili kati ya sita waliofikishwa katika hospitali hii hatuwezi kuwamudu katika matibabu hivyo wanapewa rufaa ya kwenda katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera (Bukoba) au hospitali ya Rufaa ya Kanda (Bugando)," alisema Dr Furaha.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Hamis Dawa alisema jeshi hilo halina kituo cha Zimamoto katika Wilaya ya Kyerwa hivyo Wilaya hiyo inategemea huduma ya Jeshi hilo kutoka kituo cha Wilaya jirani ya Karagwe.
"Baada ya kupata taarifa la tukio hili askari wangu kutoka kituo cha Wilaya ya Karagwe wamejitahidi kuwahi kwenye tukio na kushirikiana na wananchi kuzima moto huo.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema miili ya wanafunzi walifariki katika ajali hiyo ya moto imeharibika vibaya hivyo wazazi hawawezi kuwatambua watoto wao kwa kuwatazama.
"Utaratibu wa kawaida wa kuwatambua wanafunzi hao hauwezekani kwa sababu miili imeharibika vibaya hivyo utatumika utambuzi wa kitabibu (DNA) ili kuweza kutambua miili ya wanafunzi hao," alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Mwaimu alisema kwa sasa hawezi kumlaumu mtu hadi pale watakapopata majibu kutoka kwa tume iliyoundwa.
"Ninawashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushirikiana na Kamati ya ulinzi ya Wilaya kuzima moto huo lakini wakiendelea kuwa watulivu wakati tukisubiri taratibu za kitabibu zikamilike," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti ameifunga shule hiyo kwa wiki moja kuanzia leo (jana) ili kupisha tume ya uchunguzi yenye watu sita kufanya uchunguzi wa nini chanzo cha ajali hiyo.
"Shule hii haina wanafunzi wa darasa la saba ambao wana mtihani wa Taifa hivyo naifunga kwa wiki moja kuanzia sasa ili uchunguzi wa kina kuhusu ajali hii uweze kufanyika lakini pia wanafunzi waweze kuungana na familia zao kwa ajili ya kupewa faraja ili waweze kusahau tukio lililotokea.
Pia Gaguti alisema amesitisha huduma ya malazi katika shule hiyo hadi maelekezo yatakapotolewa baada ya uchunguzi kufanyika.
Gaguti amevitaka vyombo vya ulinzi na Usalama Mkoa wa Kagera kufanya mapitio upya ya shule za bweni zote za mkoani humo ili kuhakiki kama zina vibali halali vya Serikali vya kuruhusu malazi katika mabweni au hosteli hizo.
Na kuhakiki ubora wa majengo na mfumo wa umeme, mifumo ya kujihami, milango na madirisha ya kujiokoa linapotokea tatizo.
Alisema hatua zitachukuliwa haraka kwa shule ambazo hazina vigezo vya kutoa huduma ya malazi na viongozi wa shule watakuwa chini ya uangalizi kutoa ushirikiano wa tukio lililojitokeza.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇