WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akimpa maelekezo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, SAP Onesmo Lyanga (kulia),
wakati alipofanya ziara Ofisi ya Kamanda huyo, Mjini Ikwiriri, Wilaya ya
Rufiji, leo. Kushoto ni Mkuu wa Utawala wa Mkoa huo, ACP Richard Ngole.
Amelitaka Jeshi hilo kudhibiti vurugu zozote au uvunjifu wa sheria hasa
katika kipindi hiki nchi inapoelekea katika uchaguzi mkuu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto),
akiangalia ramani ya ujenzi wa Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kipolisi Rufiji, ambayo inahitajika shilingi milioni mia tatu ili iweze
kujengwa. Waziri huyo aliahidi kuzitafuta fedha hizo ili kufanikisha
ofisi hiyo iweze kujengwa. Kulia ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, SAP
Onesmo Lyanga. Simbachawene alifanya ziara katika ofisi hizo zilizopo
Ikwiriri, Wilayani Rufiji, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati),
akimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, SAP Onesmo
Lyanga (kulia), wakati akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama
katika Mkoa wake. Waziri huyo alifanya ziara Ofisi ya Kamanda huyo,
Mjini Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, leo, na kuwataka Polisi kudhibiti
vurugu zozote au uvunjifu wa sheria katika kipindi hiki cha uchaguzi
mkuu. Kushoto ni Mkuu wa Utawala wa Mkoa huo, ACP Richard Ngole. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akisalimiana
na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, SAP Onesmo Lyanga, wakati
alipokua anawasili Ofisi ya Kamanda huyo, Mjini Ikwiriri, Wilayani
Rufiji, leo. Kulia ni Mkuu wa Utawala wa Mkoa huo, ACP Richard Ngole. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*********************************
Na Mwandishi Wetu, MOHA, Rufiji.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene amelitaka Jeshi la Polisi kudhibiti vurugu zozote au
uvunjifu wa sheria hasa katika kipindi hiki nchi inapoelekea katika
uchaguzi mkuu.
Amewataka muda wote wawe
tayari kwa kujipange vizuri na pia intelejensia wahakikishe kila
kinachotekea katika jamii wanakijua ili kuhakikisha nchi inakua salama
na uchaguzi umalizike salama.
Akizungumza na Viongozi Wakuu
wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Mjini Ikwiriri leo, wakati alipokuwa
safarini akitokea Mkoani Mtwara kuelekea Jijini Dar es Salaam,
Simbachawene amewataka Polisi wasije kujisahau na kudhani kuwa wapo
salama sana bali muda wote wawe macho kujilinda, kulinda raia na mali
zao.
“Msije mkajisahau mkadhani mpo
salama sana, hawa watu uvamia pale mnapojisahau ndipo wanafanya hayo
mambo. Tunapoelekea kipindi hiki cha uchaguzi ni vizuri mkawa katika
tahadhali, intelejensia ikae vizuri kuhakikisha kila kinachotokea kwenye
jamii mnakijua,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Mshirikiane
na vyombo vingine kudhibiti uhalifu, Serikali ni moja, dola ni moja,
Mamlaka ni moja na Amiri Jeshi Mkuu ni mmoja, kwahiyo pale
mnapopungukiwa tumia taarifa kutoka kwa wenzenu.”
Pia Simbachawene alilitaka
Jeshi hilo lithibiti matukio ya uhalifu kuanzia chini na pia wasilipuuze
kwa kuwa tukio likidharauliwa ndipo baadaye linbakuja kuwa kubwa na
kuleta matatizo makubwa katika jamii.
“Mdhibiti matukio kuanzia
chini, utakuta tukio lina cheni fulani lakini halishughulikiwi, hivyo
linazaa lingine na matokeo yake linakua kubwa zaidi, matukio yanayotokea
yathibitiwe kwa kiasi cha kutosha ili yasije kuleta madhara makubwa
hapo baadaye,” alisema Simbachawene.
Aidha, Waziri huyo aliahidi
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ofisi ya
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, ambapo atahakikisha
anamfikishia ombi Rais Dkt. John Pombe Magufuli aweze kusaidia kuanza
kwa ujenzi wa ofisi hiyo.
“Nitamuomba mheshimiwa Rais
aone uharaka wa kutupa fedha ya ujenzi wa ofisi, ambayo ni shilingi
milioni mia tatu, bila ofisi mnawezaje kufanya kazi, hatuwezi kuwaacha
watu kwenye vijumba vyenye joto, itakua ni mateso, tutajitahidi tuweze
kufanikisha hili kwa kulifanyia kazi kwa uharaka zaidi,” alisema
Simbachawene.
Waziri huyo pia alimpongeza
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo wa kipolisi pamoja na wasaidizi wake,
kuhakikisha wanadhibiti uhalifu kwa kiasi kikubwa na sasa eneo hilo lina
amani na wananchi wanaendelea na shughuli zao za maendeleo.
Kwa upande wake Kamanda wa
Polisi wa Mkoa huo wa Kipolisi, SACP Onesmo Lyanga alisema Mkoa wa
Kipolisi Rufiji hali ya usalama imeimarika na Wilaya zote nne za
Kiserikali ambazo ni Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Mafia zipo salama.
“Mkoa huu wa Kipolisi
ulianzishwa mwaka 2017, na mpaka sasa, hali ya uhalifu ni shwari,
tunaendelea kufanya misako na doria kupambana na uhalifu mdogo na mkubwa
unaofanyika katika Mkoa wa Kipolisi Rufiji,” alisema Lyanga.
Pia Lyanga alimshukuru Waziri
huyo kwa kuwatembelea, na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote
aliyowapa, na wataendelea kufanya kazi kwa weledi muda wote kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇