*******************************
Tanzania imesema itatumia kipindi
chake cha uenyeketi wa nchi za Afrika,Caribbean na Pacific na Umoja wa
nchi za Ulaya katika kusisitiza juu ya urejeshwaji wa rasilimali
zilizoporwa katika nchi hizo nyakati za ukoloni,kuheshimu mamlaka ya
nchi husika na urejeshwaji wa wahamiaji haramu kwa kuzingatia utu na
haki za binadamu.
Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. damas Ndumbaro
ameyasema hayo wakati akishiriki mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo
ya Nje wa jumuiya ya nchi za Afrika,Caribbean na Pacific (OACPS) ambapo
Tanzania inapata heshima ya kukabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa
ngazi ya Balozi na Waziri katika nchi 79 za jumuiya hiyo.
Ameongeza
kuwa mbali na masuala hayo pia Tanzania katika kipindi chake cha
uenyekiti itatilia mkazo zaidi suala la mashirikiano ya kiuchumi ili
kuziwezesha nchi zote za Jumuiya ya Afrika,Caribbean na Pacific kuingia
katika uchumi wa kati ili kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi wake
jambo litakalosaidia kupunguza uhamiaji haramu na kupunguza uhalifu wa
kimataifa miongoni mwa nchi hizo.
Aidha amesema
kuwa hoja nyingine ni kuhusu majadiliano yanayoendelea hivi sasa kati
ya Nchi za Afrika,Caribbean na Pacific na Jumuiya ya Ulaya ya kupata
mkataba mpya baada ya kumalizika kwa mkataba wa Kotonu uwe ni mkataba
wenye manufaa kwa pande zote mbili utakaokuwa na msukumo katika suala la
maendeleo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇