Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiweka udongo kwenye
kaburi la Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa
katika Mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lupaso Masasi Mkoani
Mtwara
……………………………………………………….
Na.Majid Abdulkarim, Lupaso – Masasi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa eneo lililotengwa kwa
ajili ya mazishi ya Viongozi Dodoma litumike kwa mambo mengine kwa
ajili ya wananchi na viongozi hao watazikwa katika maeneo yao
walipozaliwa.
Kauli hiyo ameitoa leo katika
mazishi ya Hayati Benjamini Mkapa aliyekuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya
Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kijijini cha Lupaso
wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara .
“Kuna wakati tulipanga sehemu ya
kuzika Viongozi Dodoma, Mzee Mkapa akasema nizikeni Lupaso,
nilipomuuliza Mzee Kikwete akasema Msoga, nikaogopa kumuuliza Mzee
Mwinyi maana ana miaka mingi isije kutokea kitu nikaonekana nimemletea
uchuro, mimi pia nikawaza nikifariki nizikwe Chato”ameeleza Rais
Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema kuwa
Watu wa Lupaso wana bahati sana kumpa Mzee Mkapa ambaye ni Mzalendo
aliyependa nyumbani kwao ndio maana hata akachagua akifariki azikwe
Lupaso.
Hivyo Rais Magufuli ametoa wito
kwa Jamii ya Watanzania kuwa inapaswa kujifunza kwa Mzee Mkapa kwa
upendo aliouonyesha kwa Wananchi wote, Kijiji cha Lupaso kimeacha alama
kubwa kwa Taifa la Tanzania kutokana na kutoa Kiongozi Mzalendo na
aliyependa Wananchi wake.
Rais Magufuli amehitimisha kwa
kuishukuru Kamati ya Maandalizi ya Mazishi iliyoongozwa na Waziri Mkuu
na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Viongozi
wote, Wananchi, Viongozi wa Dini zote sambamba na Waombolezaji
walioshiriki bega kwa bega kuhakikisha safari ya mwisho ya Hayati Mzee
Benjamin Mkapa katika makazi yake ya milele.
Naye Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali
Mohammed Shein akitoa salam za mwisho katika mazishi hayo amesema kuwa
leo tunamuaga mkapa kwa majonzi makubwa wananchi wa zanzibari wanaungana
na watanzania kumuombea mzee mkapa Mwenyezi mungu amsamehe huko
mbinguni.
Naye Rais Mstaafu wa awamu ya
Tatu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza kuwa kuna kipindi alipita
nyakati ngumu, nzito na katika nyakati zile mzee Mkapa alikuwa ni mmoja
wa nguzo zake za kuegemea katika kipindi kile kigumu, kwa hiyo ni mtu
aliyekuwa na msaada mkubwa kwake na kwa taifa .
“Wilaya hii ya Masasi ilikuwa na
tatizo la njaa wakati ule, nikiwa Katibu CCM Masasi na DC tukabuni mradi
wa kilimo cha muhogo hakikupendeza sana kwasababu Wamakuwa hawapendi
sana kula ugali wa mihogo kama Mashemeji zangu Wamakonde, ila Mzee Mkapa
alisimama nasi” ameweka wazi Dkt. Kikwete.
“Ni ngumu kupata maneno ya
kumuelezea Mzee Mkapa, nimemfahamu miaka mingi lakini nimemfahamu zaidi
nilipokuwa Katibu CCM Wilaya ya Masasi na yeye alikuwa Mbunge Nanyumbu,
alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ila pamoja na ubize aliwatumikia Wananchi
wake”, ameeleza Dkt. Kikwete.
Katika mazishi hayo baada ya
mwili wa hayati Mkapa kushushwa kaburini na taratibu za kidini
kukamilika, imepigwa mizinga 21 ikiwa ni ishara ya heshima kwa marehemu
Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu Benjamin William Mkapa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇