Mwili wa Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Marehemu Benjamini Mkapa, utaagwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia keshokutwa Jumapili Julai 26 hadi Jumanne Julai 28, 2020, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kabla ya kupelekwa kuzikwa katika Kijiji cha Lupaso, Wilayani Masasi mkoani Mtwara
Akitangaza ratiba ya mazishi leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema siku ya Jumapili mwili wa Mzee Mkapa utaanza kuagwa saa 4, 00 asubuhi katika Uwanja huo wa Uhuru na Ibada itataongozwa na Kanisa Katoliki kabla ya waombolezaji kuanza kuaga.
Amesema, shughuli ya kuaga itaendelea hadi Jumanne, Julai 28, 2020 ambayo ndiyo siku mwili utaagwa Kitaifa kuanzia asubuhi hadi saa 6.00 mchana na itakapofika saa 8.00 mchana mwili utasafirishwa kwa ndege hadi Uwanja wa Ndege wa Nachingwea kisha kupelekwa Masasi kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatano, Julai 29, 2020.
Waziri Mkuu amewasihi wanafamilia na Watanzania wote kwa ujumla waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Mapema, Waziri Mkuu alikwenda nyumbani kwa Marehemu Mzee Mkapa Masaki jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa Mjane wa Marehemu Mama Anna Mkapa pamoja na familia, kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli na Serikali.
“Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dk. Magufuli,” amesema Waziri Mkuu.
Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Dk. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Akitangaza kifo hicho kupitia vyombo vya habari usiku wa kuamkia leo, Rais Dk. Magufuli kwa masikitiko makubwa alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee Mkapa amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Rais Dk. Magufuli amewataka Watanzania wote wawe watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mzee Mkapa. “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia.”
Aliongeza kuwa “ Amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki.”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇