Na Lidya Lugakila, Bukoba
Watanzania wamehaswa kuyaendeleza mambo mbalimbali aliyoyafanya na kuyasimamia Rais wa awamu ya tatu hayati Benjamin William Mkapa wakati wa uongozi wake, ikiwemo kuweka utumishi wa umma katika weledi na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Kauli hiyo imetolewa na katibu tawala wa Mkoa wa Kagera Profesa Faustine Kamuzora (pichani) ambaye amemkumbuka hayati Benjamini Mkapa kwa mambo mengi yenye kulijenga taifa huku akisema kuwa enzi za utawala wake alifanya maboresho makubwa kwa watumishi wa umma na pia kuboresha uchumi wa nchi.
" katika Enzi za uongozi wake Mzee Benjamini Mkapa alifanya vitu vingi ambavyo tunavifahamu mfano sisi watumishi wa umma tunafahamu alifanya maboresho makubwa mpaka akaacha watumishi wa umma tuko katika weledi ambao umetusaidia mpaka leo hii katika utendaji kazi wetu" alisema.
Hata hivyo Profesa Kamuzora ameomba kitabu alichokiandika Rais Mkapa kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwezesha watanzania wengi kukisoma na kunufaika na masuala muhimu yanayohusu nchi yaliyomo katika kitabu hicho.
"Kwa Mtanzania yeyote anayetaka kuifahamu Tanzania asome kitabu hicho, kina masuala mengi na muhimu ambayo yanajenga umoja pia mshikamano" alisema Profesa Kamuzora.
Aidha kwa upande wao wakazi wa mkoa wa Kagera waliozungumzia msiba huo akiwamo Mkurugenzi wa kampuni ya Utalii ya Kiloyera Tours, Mary Kalikawe wamesema kuwa Rais Mkapa alikuwa mfano wa kuigwa hasa katika jitihada zake za kukabiliana na migogoro ya kisiasa ndani na nje ya nchi kwa kuitatua huku wakichukulia mfano wa nchi ya Burundi ambapo amesema kuwa aliukalia mgogoro huo na kuhakikisha amani imepatikana.
John Mutagwaba ni mkazi wa Kiziba wilayani Missenyi mkoani Kagera amesema kuwa Rais Mkapa alikuwa kiunganishi, na ambaye pia hakuwa na ubaguzi wa wa aina yoyote badala yake alifanya kazi iliyolenga kupatikana kwa maendeleo ya watanzania wote.
Ikumbukwe kuwa taarifa za kutokea kwa msiba huo zimetangazwa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli, ambapo pia Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassimu Majaliwa ameeleza kuwa Mzee Mkapa atazikwa kijijini kwao Rupaso Masasi Mkoani Mtwara mnamo julai 29 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇