Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kulia) moja ya zao la kazi za mikono za wanufaika wa huduma zinazotolewa na Hospitali hiyo waliowezeshwa kutengeza bidhaa mbalimbali wakati wa ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kulia ni Msajili wa Mashirika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao.
Msajili wa Mashirika
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao ameeleza kuridhishwa na
ubora na viwango vya huduma zinazotolewa na Hospitali ya CCBRT za kuwahudumia
Watanzania wanaokabiiliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.
Mayao ameyasema hayo
jijini Dar Es Salaam alipofanya ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya
ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali sambamba na uhakiki
wa matumizi ya fedha ndani ya Mashirika hayo ili kuendana na mwongozo wa
Mashirika unayosisitiza uhalisia wa fedha na matumizi yake.
“Hii ni ziara ya
kujiridhisha na fedha zinazotumiwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili
kuhakikisha fedha zinazoingia kwa jina la Tanzania, zikilenga kuwanufaisha
Watanzania zisitumike kinyume” alisisitiza
Aliongeza kuwa
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatakiwa kuhakikisha fedha zinazotolewa na
wafadhili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali zinatumika kulingana na
malengo yake na hivyo kuwanufaisha walengwa waliokusudiwa.
“Hapa nieleze tu
kwamba CCBRT wanafanya kazi nzuri sana katika huduma zao kwa walengwa na hata
katika miradi wanayoitekeleza, Mfano ni Jengo hili hapa kweli tunaona kwamba
wamefanya vizuri sana” alisema.
Aidha, amesema kuwa
baadhi ya Mashirika yaliyokaguliwa pamoja na kutekeleza majukumu yake,
hayatekelezi miradi kwa ukamilifu wake na hivyo kusababisha maswali na hoja katika
matumizi ya fedha zinazotolewa na wafadhili.
Akizungumzia ziara
hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dkt.
Richard Sambaiga amesema CCBRT imekuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa miradi
ya maendeleo na huduma hasa za afya kwa watu ambao wengi wana kipato cha chini.
“Niseme ukweli, Kazi
hii kubwa inayofanywa na CCBRT ilitakiwa kufanywa na Serikali, Lakini kwa kuwa
Serikali imekasimu kazi hii kwa NGOs kwa utaratibu unaokubalika hivyo ni lazima
lazima kazi hizo kufanyika kwa viwango vikubwa kama inavyofanya
CCBRT”alisisitiza.
Pia amefafanua kuwa mwongozo
wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliotolewa na Serikali hivi
karibuni hauna kusudio la kuyabana Mashirika hayo kama inavyodhaniwa na baadhi wadau
bali umelenga kuweka uwazi katika matumizi ya fedha za miradi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi amesema Hospitali hiyo
inafanya kazi ya kuwa kubwa ya kuwarejesha watu wenye matatizo mbalimbali ya
kiafya katika mfumo wa kawaida ili waweze kufurahia maisha kama walivyo watu
wengine.
Brenda amesema kuwa Hospitali
ya CCBRT inatoa huduma mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na upasuaji kwa watu
wenye miguu pinde na kuwapatia vifaa saidizi, upasuaji na urejeshaji wa katika
hali ya kawaida kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na midomo sungura, utoaji wa
huduma kwa wanawake wenye ugonjwa wa fistula pamoja na kutoa huduma nyingine za
Matibabu.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇