*Asema anayetaka fedha, ataipata shambani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana
wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi waache kukaa vijiweni na badala yake
waanzishe bustani ili kujiongezea kipato.
“Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote
anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime,
twende shambani. Shamba siyo lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama muhogo.
Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana.”
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi,
Julai 18, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda
kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu
unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.
Amesema Serikali imetoa sh. milioni 600
ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji huko Mpumbe, Mnindu, Chiepo na Chikalala.
“Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime wakati wote, iwe masika au kiangazi.
Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia
kipato zaidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kamati ya ujenzi ya
mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu
wa ujenzi wa majengo ya Serikali kwenye soko hilo.
Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Bw.
Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe
ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji
wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya
kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch)
badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba
vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka
mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.
“Nimetoa maagizo manne. Kwanza, toboa
milango, pili weka vizimba ili wananchi wauze bidhaa zao mahali pasafi, usiruhusu
watu wauze bidhaa zao chini, siyo sawa kiafya. Tatu, chimba visima, weka mnara,
tanki na mipira ya kumwagilia ya kutosha ili wakulima wasipate taabu ya kusomba
maji. Weka mashine ya kusukumia maji ili uweze kuyasambaza katika eneo kubwa.
Nne, tenga eneo la kuuza bidhaa kwa rejereja ili wananchi wa hapa jirani wanufaike
na mradi huu,” amesema.
Pia alimwagiza Afisa Kilimo wa Wilaya
hiyo, Bw. Harun Ibrahim Kiara ahakikishe wanatoa elimu ya kilimo cha bustani
kwa vijana ili waanze na matuta machache. “Pia anzisheni programu ya kukutana
na vijana na akinamama na muwaeleze bonde la Mnindu linatumikaje kwa kilimo
hicho,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Bw. Selemani Mrope alisema mradi huo
unatarajiwa kutumia sh. milioni 127 hadi kukamilika kwake na mpaka sasa
wamekwishapokea sh. milioni 50.8 ambazo ni sawa na asilimia 40.
Alisema ujenzi wa soko ambao ulianza Mei
25, 2020 ulikadiriwa kugharimu sh. milioni 25 na mpaka sasa wameshatumia sh.
milioni 18.2 ambapo ujenzi umefikia hatua ya uinuaji wa nguzo. Mradi huo unatarajia
kukamilika Agosti 30, mwaka huu.
Alisema Chuo cha Ufundi Stadi Mkowe
kinatekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo wa
mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA) kupitia mfuko wa kuongeza na kuboresha elimu (SDF).
“Mradi huu umelenga kuwezesha kuwepo kwa soko
la uhakika, ongezeko la ajira na uzalishaji, ongezeko la kipato kwa jamii,
upatikanaji wa uhakika wa chakula lishe na uboreshiji wa miundombinu ya kilimo
cha umwagiliaji kwa mazao ya bustani,” alisema Bw. Mrope.
Alisema hadi sasa wamekamilisha kazi ya kuandaa
mitala na miongozo ya kufundishia wakulima wote wa bustani kwa gharama ya sh. milioni
nne na kwamba wanaendelea na ukarabati wa darasa moja litakalotumika kutoa
elimu kwa wakulima wote wa bustani
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 18, 2020.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇