Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Milton Lupa kuhakikisha chakula kinachonunuliwa Kanda ya Arusha kinahifadhiwa kwenye vihenge vipya.
Maagizo hayo ameyatoa wilayani Babati, Manyara alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa maghala mapya na vihenge vya kisasa ambavyo vimekamilika kwa asilimia 94.
Waziri Hasunga ameiagiza NFRA kuhakikisha inanunua mazao mchanganyiko katika msimu huu na siyo kununua mahindi na maharage pekee.
" Nataka kuona NFRA inabadilika siyo kama zamani mlikua mnanunua mahindi na maharage peke yake kana kwamba hakuna vyakula vingine vinavyopatikana, msimu huu nataka kuona mnanunua mazao mchanganyiko ili kama kuna dharura inatokea msaada wa chakula mtakaotoa uwe ni kamili kwa wenye uhitaji," Amesema Hasunga.
Amesema Ujenzi wa vihenge vya kisasa pamoja na maghala mawili ya kisasa wilayani Babati utaifanya NFRA Kanda ya Arusha inayohudumia mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro kuongeza akiba ya Taifa ya chakula kutoka tani 39,000 hadi 79,000.
Akisoma taarifa yake mbele ya Waziri Hasunga, Mtendaji Mkuu wa NFRA, Milton Lupa amesema ujenzi wa mradi wa vihenge hivyo unatekelezwa kwenye viwanja vya NFRA eneo la Maisaka ambapo ulianza rasmi Desemba 2018 na unatekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya Poland.
Lupa amesema mradi huu unatekelezwa katika mikoa nane ya Tanzania bara ikiwemo Mkoa wa Manyara ambapo kanda ya Arusha kupitia mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula unaendelea na ujenzi mpya wa vihenge nane vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 25,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 15,000.
Mahenge ya Kisasa yanayojengwa wilayani Babati, Manyara na NFRA ikiwa ni jitihada za kuongeza uhifadhi wa Chakula Kanda ya Arusha inayohudumia Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza na watumishi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Arusha alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala mapya wilayani Babati, Manyara.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akimsikiliza Mhandisi wa NFRA, Imani Nzobonaliba wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vihenge vipya vinavyojengwa wilayani Babati, Manyara. Wa kwanza kulia ni Mhandisi Radoslaw Osowiesk kutoka Kampuni ya ARAJ ya Nchini Poland.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇