NA TIGANYA VINCENT
HALMASHAURI ambazo zinazotegemea sehemu ya mapato kutoka kwenye zao la tumbaku zimetakiwa kuandaa mkakati mpya ambao utawawezesha kulima mazao mengine ili kuwa na msingi wa vyanzo vipya vya mapato ya ndani.
Hatua hiyo inafuatia Kampuni zinazonunua tumbaku Mkoani Tabora kuendelea kushusha makisio ya uzalishaji kwa wakulima wa tumbaku.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Urambo.
Alisema Kampuni za Tumbaku zimekuja ya staili mpya ya kudai kuwa zitanunua tumbaku kilo chache lakini badala yake zimekuwa zikinunua tumbaku nyingi iliyolimwa nje ya mkataba kwa bei inamuumiza mkulima na kusababisha Halmashauri kupata mapato kidogo.
Aidha Makungu alisema ni vema Halmashauri zikaanzisha kilimo kikubwa cha maembe kwa kuwa Mfanyabiashara Bakharesa ameshaonyesha nia ya kununua embe zote zinazozalishwa Mkoani Tabora.
Alisema cha msingi kuwaelimisha wakulima kulima kitaalamu na kutoa huduma za ugani kwao ili waweze kuzalisha maembe bora.
Makungu aliongeza ni vema Halmashauri zikasisitiza kilimo cha korosho na Alizeti kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kuwa na vyanzo vingi vya kujipatia kipato.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇