Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran imetangaza kuwa: Hadi leo Jumanne mchana watu 14,656 miongoni mwa walioambukizwa kirusi cha corona wamepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitali.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran Kianoush Jahanpour, amewaeleza waandishi wa habari kuwa, jumla ya watu 44,606 wameambukizwa virusi vya covid-19 nchini Iran; na kwa masikitiko, watu 141 wamefariki dunia katika muda wa saa 24 zilizopita kutokana na ugonjwa huo na kuifanya idadi ya watu waliopoteza maisha hadi sasa kufikia 2,898.
Aidha, Dokta Jahanpour amesema: Idadi ya wananchi walioshiriki katika mpango wa upimaji virusi vya corona vya covid-19 nchini Iran imepindukia milioni 65.
Sambamba na hatua zinazochukuliwa na serikali kwa msaada wa vikosi vya ulinzi, mchakato wa kuwagundua mapema na kuwafuatilia watu waliochanganyika na waathirika sambamba na kuwawekea karantini na kuwapatia huduma za tiba waathriika hao wa covid-19 unaendelea kufanyika kwa kasi kwa nchini kote kwa kushirikisha wananchi wa matabaka yote.
Kirusi cha corona, kinachojulikana rasmi kama COVID-19, kiligunduliwa mwishoni mwa mwezi Desemba 2019 katika mji wa Wuhan nchini China.
Mbali na China, kirusi hicho hivi sasa kimeshasambaa katika nchi karibu zote duniani.
Kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa, hadi sasa zaidi ya watu laki nane wameambukizwa covid-19, zaidi ya 172,000 miongoni mwao wamepata nafuu na wengine zaidi ya 38,000 wamefariki dunia kutokana na maambukizi ya kirusi hicho angamizi.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇