MKUU wangu wa Nchi, nimeamua kukushukuru kwa
uamuzi wako Mgumu wenye Busara wa
kuwataka Watanzania waache kutishana kuhusu ugonjwa wa Corona, bali waendelee
kuchapa kazi, lakini kwa tahadhari kubwa juu ya Ugonjwa huo hatari uliozikumba
nchi masikini na tajiri duniani.
Wakati unatoa uamuzi huo hukukurupuka kwa kuiga
marufuku zinazotolewa na viongozi wa nchi mbalimbali, za kuwataka wananchi wao
wasitoke nje kwa siku kadhaa wakidhani ndo njia mojawapo ya kuudhibiti ugonjwa huo , bali wewe ulitulia
na kufikiria mazingira ya nchi yako na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
JPM,ulijua kabisa kwamba ukikurupuka na kuwaiga
viongozi wenzako, licha ya uchumi kuyumba, bali kwa kiasi kikubwa ungewaumiza
wananchi wa hali ya chini walio wengi ambao bila kutoka kutafuta hawawezi kupata mlo wao wa siku.
Pia, hali ya nchi ingevurugika kama
tunavyoshuhudia kila kukicha vurugu
katika Nchi jirani na mataifa mengine makubwa, ambako wananchi wameshindwa
kuhimili/kuvumilia njaa na mateso wanayopata na familia zao baada ya kukosa mahitaji yao muhimu kwa
katazo la kutotoka majumbani.Lakini pamoja na amri hizo idadi ya wagonjwa
inazidi kuongezeka.
Tumekuwa tukishuhudia mapambano kati ya raia na
askari wakiwapiga viboko na mabomu ya machozi waliokiuka amri ya kukaa
majumbani, lakini si kwa kupenda bali wamelazimika kutoka kwenda kutafuta
riziki baada ya kukabwa na njaa kali. Je, hilo ndo suluhisho?
Rais wetu, uamuzi wako huo mgumu, umeliepusha
Taifa na mambo mengi mabaya ambayo
yangetokea endapo ungewaiga marais
wenzako. Kuna haja hata ya marais hao kukuiga wewe ili kuleta utulivu katika
nchi zao.
JPM,huwa nakaa na kufikiria endapo ungetoa amri
ya Watanzania kutotoka nje, hivi ingekuwaje? Kwanza hali hii tu ya tahadhari ya
korona, imeshatuvuruga na kuvuruga uchumi, ikiwemo ya kukosa watalii ambao
wanaliingizia taifa fedha nyingi za kigeni, baadhi ya mahoteli yamefungwa kwa kukosa wateja.
Hali hiyo, imesababisha wafanyakazi kupunguzwa na
hata wengine kuachishwa kazi. Kampuni zilizokuwa zinasambaza vyakula na huduma
zingine kwenye hoteli hizo zimekosa kazi. Ndege zimekosa abiria na biashara kwa
ujumla kuyumba.
Kampuni na wafanyabiashara waliokuwa wameingia
mikataba na shule/ vyuo ya kusambaza vyakula
na mahitaji mengine hivi sasa hawana kazi.
Orodha hiyo ni mifano michache tu, lakini watu
wengi wameathirika kwa katazo hilo dogo la kupunguza misongamano ambayo ni
hatari kwa maambukizi ya Korona ambayo hadi sasa haina kinga wala tiba.
Watanzania wangepigwa marufuku kutoka nje mambo
mengi mabaya yangetokea; Wengi wa walalahoi hasa walioko mijini wangeshindwa
kuvumilia, bila kupenda wangetoka kwenda kutafuta riziki bila kujali kupigwa na
askari.
Hali ingewazidia wangekwenda kuvamia maduka ya
vyakula kwa kupora kwani hata fedha za kununulia wangekuwa hawana. Baada ya
maduka kuishiwa vyakula wangeanza kuvamia nyumba za watu wenye ahueni kimaisha
na kupora chochote walicho nacho.
JPM, hali ingekuwa hatari zaidi, tungeanza
kuporana wenyewe kwa wenyewe mitaani. Sidhani kama majeshi yetu yangeweza
kutuliza ghasia hizo, kwani ni dhahiri idadi ya askari wa majeshi yetu ni
chache sana kuliko wingi wa wananchi, wangezidiwa tu.
Isitoshe ungezuka uhasama mkubwa kati ya wananchi
na askari. Hatari zaidi ingekuwa kwa askari wanaoishi na familia zao uraiani,
wangefanyiwa vurugu kulipiza kisasi. Nakushukru sana JPM kwa uamuzi wako huo
mgumu umeepusha mengi.
Na endapo raia wangetii amri ya kutotoka
majumbani, basi, walalahoi wasio na chochote wala akiba ya vyakula, wangekufa
wengi kwa njaa, vifo ambavyo vingekuwa vingi kuliko vifo vya korona
vinavyotokea kwa sasa Italia na Marekani. Nasema kinachotakiwa ni kumuunga
mkono JPM kwa hali na mali kkwa kuwa na tahadhari kubwa na ugonjwa huo.
Lakini vile vile tujiulize, hivi Serikali yetu ina uwezo wa kuwasambazia chakula na mahitaji mengine wananchi wakibaki majumbani?
Lakini vile vile tujiulize, hivi Serikali yetu ina uwezo wa kuwasambazia chakula na mahitaji mengine wananchi wakibaki majumbani?
JPM, kwa uamuzi huo mgumu. Umeepusha kundi kubwa
la raia wasio kuwa na ajira kama vile; waendesha Bodaboda, mama/baba lishe, machinga, vibarua na baadhi ya wakulima wadogo wadogo
wanaotegemea kuuza mazao yao ndiyo wapate mlo wa siku. Hivi kundi hilo na
familia zao lingeingia barabarani kutafuta riziki ya mlo wa siku, askari wetu
wangeweza kulizuia?!!!
Pia, nawachukiana kupingana nao baadhi ya Watanzania
walioko nje ya nchi na ndani ya nchi ambao wanaubeza uamuzi wako, wakitaka uige
uamuzi wa unaotolewa na baadhi ya marais katika nchi zao wa kupiga marufuku
wananchi kutoka majumbani kwa siku kadhaa kwamba ndiyo njia muafaka ya
kupambana na Korona.
Naamini,wengi hawajui mazingira ya nchi yetu,
wanayafananisha na huko waliko. Na waliopo nchini nao hawajui ipasavyo
mazingira yetu na endapo amri hiyo ikifuatwa hawajui athari ambazo zingetokea.
JPM, nakushukuru wewe na Mwenyezi Mungu
aliyekuongoza kutoa uamuzi huo mgumu wenye busara. Kinachotakiwa kwa Watanzania
ni kumuunga mkono kwa Rais Wetu, kwa kufuata maagizo na maelekezo ya Serikali,
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, jinsi ya kupambana na ugonjwa huo hatari.
JPM, pia nashauri Serikali yetu iendelee kuwa na
msimamo wa kulinda mipaka yetu, na njia zote za panya kuwabaini wageni wote
waingiao nchini kwa kuwapima joto (Korona) na kuwaweka eneo la uangalizi kwa
siku 14. Jambo hilo lisiwe na chembechembe zozote za upendeleo/ubaguzi, awe
raia, si raia au kiongozi yeyote, wote wapimwe kwa mujibu wa sheria na taratibu
zilizopo.
JPM, kila siku namuomba Mungu atuepushe na gonjwa
hili la hatari lisiendelee kusambaa nchini. Na ifikapo Aprili 17, mwaka huu,
siku ambayo tunatimiza mwezi mmoja tangu utoe uamuzi huo mgumu, Mungu akuongoze
tena kwa kutoa uamuzi wenye faraja kwa Watanzania, ili ikiwezekana hata shule
na vyuo vifunguliwe pamoja na mikusanyiko mingine irudi kama kawaida.
Lakini tutafikia hapo kwa watanzania kumuunga mkono
Rais wetu katika mapambano ya kuutokomeza ugonjwa huo. Tusipofanya hivyo, basi tusije tukamlaumu JPM kwa
atayoyatangaza siku hiyo.
Ndimi, Richard Mwaikenda
Senior Photojournalist
0754264203
Ukonga, Dar es Salaam.
March 31,2020.
Mimi naunga mkono busara za Rais wetu mpendwa kutofunga kabisa shughuli za kila siku bali kuchukua tahadhari ya hali ya juu.Ushauri wangu ili tuweze kuwa salama tufunge kwa muda wageni kuingia nchini kwani mataifa mengine idadi ya wagonjwa ni ya kutisha.Tusipo zuia tutajikuta wameingia wengi hata tukija kuzuia tutakua tumechelewa
ReplyDelete