Na Mwl.
Salehe S. Msonga
UVCCM
CHAMAZI
UTANGULIZI:
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!!
Mnamo
02/06/2018 niliandika Makala iliyoitwa ‘SIRI KUBWA YA CCM HII HAPA’, ni Makala iliyosambazwa kwenye
makundi ya WhatsApp na ilijikita zaidi katika kuonesha ni siri gani inayoifanya
CCM kushinda na kuwa na uhakika wa kushinda kila chaguzi kuu nchini, ambapo mwandishi
aliivujisha siri hiyo hadharani ya kuwa ni KUHANGAIKA NA SHIDA ZA WATU kupitia utekelezaji mzuri wa ilani
yake. Leo mwandishi yule yule nakuja na Makala hii nyingine inayoonesha ni kwa
jinsi gani serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inavyokoleza radha ya nchi yetu ya Tanzania kwa
watanzania.
Tangu
kuundwa kwake toka kwenye muungano wa Tanganyika na Zanzibar mnamo 1964,
Tanzania imekuwa na jumla ya awamu tano za uongozi wa nchi ambazo kwa bahati
nzuri zote zimetokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tanzania imekuwa ni nchi
yenye tunu nyingi za taifa ambazo zinatutangaza kama nchi kimataifa sambamba na
kumnufaisha mtanzania mwenyewe. Baadhi ya tunu hizo ni Amani na Utulivu, Madini
mbalimbali, Ardhi yenye rutuba, Lugha moja ya kitaifa licha ya kuwa na makabila
na tamaduni zaidi ya 120, Hifadhi kemkem za wanyama pori, Bahari, Maziwa na
Mito mikubwa, Milima mirefu na miundo mbinu mikuu muhimu kwa uchukuzi na
usafirishaji. Kuna baadhi ya tunu hizi adimu katika baadhi ya nchi za afrika na
hata nje ya afrika. AMANI na UTULIVU ni tunu kuu kwa nchi yetu kwani
tunashuhudia mataifa mengi duniani yamekuwa yakivutiwa nayo na hata Tanzania kuwa
ndiyo kipenzi chao kiutalii na hata kimbilio lao pale wapatapo matatizo mbalimbali nchini mwao mfano wakimbizi.
RADHA
YA TANZANIA YAKOLEA
Radha
ya u-tanzania imezidi kukolezwa na kuongeza ufahari wetu na kujivuia kuwa watanzania,
hii ni kutokana na awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ilivyo na inavyojidhatiti katika kuongeza kasi ya kuzigeuza tunu za taifa (Transformation)
kuwa mkombozi wa mtanzania hasa yule wa hali ya chini ili naye si aionje tu,
bali ale keki ya taifa lake. Haya yanaonekana pale tunaposhuhudia utendaji na
usimamizi makini wa viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Rais John
Pombe Magufuli katika sekta mbalimbali kwa lengo la kumsogezea karibu mtanzania
wa kawaida fursa, nyenzo na njia za kujifanyia maendeleo yake ya kila siku
Mnamo
mwezi oktoba, 2020, serikali ya awamu ya tano inaelekea kutimiza miaka mitano
kamili huku ikiwa imeshashughulikia karibia kila sekta muhimu kwa ustawi wa
mwananchi wa leo na hata wa kesho.
Tukianza
na sekta ya nishati, tunaona hatua kubwa tuliopiga kama nchi, kwani ndani ya
miaka minne tu, tumeona mafanikio yafuatayo katika sekta ya nishati: Ongezeko
la megawati 480 za umeme katika gridi ya Taifa, Bilioni 138 zimeokolewa kwa kutokana
na kuachana na matumizi ya mitambo mikubwa ya kufua umeme wa mafuta, Uwepo wa
ziada ya umeme usiopungua megawati 280 kwa siku, Kusitisha uagizaji vifaa vya
umeme nje ya nchi, Tanesco kutoka kampuni inayopata hasara na kuwa
inayotengeneza faida na kujiendesha pasipo ruzuku, Ongezeko la asilimia 400 uunganishaji
wa umeme vijijini, Gesi asilia imefikia futi za ujazo trilioni 57.54 na pia Uwepo wa mafuta yanayotosheleza
mahitaji pamoja na akiba. Haya yote ni mafanikio ya kujivunia ambayo nchi za
wenzetu hususani majirani zetu pengine huumiza kichwa ni kwa namna gani
Tanzania tumeweza kuyafikia kwa muda mfupi huu. Nasema ni mafanikio ya
kujivunia ni kwa kuwa mtanzania amepunguziwa mzigo mkubwa uliomuelemea katika
kuijenga nchi yake.
Pia
serikali ya awamu ya tano imeifanya Tanzania kuwa ni nchi ya kwanza barani
Afrika kwa kusambaza umeme karibia nchi nzima. Sote tunashuhudia jinsi mpango
wa REA ulivyomfikishia huduma ya umeme mwananchi wa kijijini tena kwa gharama
nafuu kabisa hali iliyompelekea mwananchi kuutumia umeme huo katika shughuri za
uzalishaji na biashara hatimaye kumuinua kiuchumi huku serikali ikipata kodi
yake (mutual relationship). Kwa mujibu wa waziri wa nishati, Tanzania imeongoza
barani Afrika kwa usambazaji wa umeme vijijini kwa asilimia 73.4 ikifuatiwa na
nchi ya Nigeria. Binafsi ni shuhuda kwa hili kwani nilistaajabishwa pale disemba
2019, niliporudi nyumbani Mwaya-Mang’ula wilayani Kilombero kusalimia ndugu na
jamaa na kukuta vile vijiji vya zamani na vya nje ya mji na maeneo ya mbali yaliyokuwa
ni mashamba ya wanakijiji tuliyokuwa tukilima kipindi hicho ya Msalise,
Mhelule, Mikoleko n.k. navyo vyote vikiwa vimesambaziwa umeme wa uhakika na
shughuri za kiuchumi zikiongezeka hali iliyovibadili vijiji na maeneo hayo kuwa
si mashamba tena bali ni makazi ya uhakika na yenye kukua kwa kasi. Kama hiyo
haitoshi, pia serikali ya awamu ya tano iko katika ujenzi wa mradi mkubwa wa
umeme wa bwawa la Mwl. Nyerere katika mto Rufiji, mradi ambao utazalisha zaidi
ya megawati 2000 za umeme na kuziingiza katika gridi ya Taifa na kufanya
gharama za umeme nchini kushuka mara dufu na pengine hata kuweza kuuza umeme wa
ziada kwa nchi nyingine za jirani. Hii kwa upande mwingine itachochea zaidi
kasi ya Tanzania ya viwanda kwani rasilimali ya nishati itakuwa ya uhakika na
ya bei ya chini pia kusababisha ongezeko la upatikanaji wa ajira viwandani.
Hakika huku ni kuzigeuza tunu za taifa za mito mikubwa kuwa mkombozi kwa
mtanzania mwenyewe.
Tukija
katika sekta ya afya na maendeleo ya jamii, kwa ufupi hapa tunajionea jinsi
serikali ilivyowahurumia mwananchi wake kwa kuongeza idadi ya zahanati nchini
kutoka 6,044 hadi kufikia 6,400, idadi ya vituo vya afya kutoka 718 hadi 1169, idadi
ya hospitali za halmashauri kutoka 186 hadi kufiki 321 na kukarabati hospitali
za rufaa za mikoa 23. Kutokana na
miundombinu iliyojengwa , idadi ya vituo vya
kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka 7,014 hadi 8,446 ndani ya miaka 4 ya awamu
hii ya tano. Pia tumeshuhudia upanuzi na uongezwaji wa vifaa tiba na vitendea
kazi vya kisasa kwa hospitali ya taifa ya muhimbili na zinginezo mfano
hospitali moyo ya Jakaya Kikwete, hospitali ya kansa ya Ocean road, hospitali
ya Benjamin Mkapa Dodoma na hospitali ya MOI sambamba na uimarishwaji wa bohari
kuu ya dawa nchini, Medical Store Department (MSD). Hii imepelekea idadi ya
wagonjwa wanaosafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu kupungua
kulinganishwa na hapo awali, pia hii imeifanya serikali kuokoa pesa nyingi
baada ya wagonjwa wengi kutibiwa hapa hapa nchini. Vivo hivyo kwa upande wa
ustawi wa jamii, serikali imeongeza fedha zaidi kwenye mfuko wa TASAF kwa ajili
ya kaya zisizojiweza sambamba na uimarishwaji / uboreshwaji wa utoaji bure wa
huduma za afya kwa wazee. Binafsi hili naitafsiri kama ni kudhihirisha kwa
vitendo ile moja ya imani ya CCM ya kwamba BINADAMU
WOTE NI SAWA, hivyo kila mtu anastahili kupata huduma sawa kama wengine.
Katika
sekta ya elimu, awamu hii ya tano imewatua jukumu na mzigo wazazi wote nchi
nzima wa kuwalipia watoto wao karo za shule katika shule za umma na badala yake
serikali imebeba mzigo huo na inatumia zaidi ya shilingi bilioni 23 kila mwezi
kuwalipia wanafunzi hao. Pia serikali imewajengea uwezo na mazingira rafiki
walimu wakuu, wakuu wa shule na maafisa elimu kata katika kusimamia vyema sera
hii ya utoaji elimu bure. Serikali inafanya hivyo kwa kuamini ya kuwa elimu
ndio ufunguo wa maisha ya mtoto. Sera ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza
hadi kidato cha nne ilianza rasmi mnamo mwaka 2016 na ikapelekea ongezeko kubwa
la udahili wa wanafunzi shuleni. Hii inamaanisha ya kuwa kabla ya sera ya elimu
bure kuna watoto wa kitanzania wa hali ya chini walikuwa wanakosa haki yao ya
kupata elimu kutokana na wazazi kukosa pesa za kulipia karo, hivyo ujio wa sera
hii ikaleta usawa kwa wote kwamba kila mtu apate elimu na hatimaye kuendana na
lengo endelevu namba nne la dunia yaani Sustainable Development Goals (SDGs) la
elimu bora kwa wote ambapo serikali kila uchwao inajitahidi kuifanya elimu yetu
iwe bora zaidi kwa kuboresha usimamizi, miundo mbinu, na vifaa vya elimu. Huku
nako ni kulekule kudhihirisha ya kuwa CCM ni chama kinachojali usawa wa watu
kwa kuamini ya kuwa BINADAMU WOTE NI SAWA
hivyo kila mtu anastahili huduma sawa kama mwengine.
Tukiiangazia
sekta ya ujenzi, uchukuzi na usafirishaji, nayo imezidi kwa kasi kubwa
kumfungulia fursa za kimaendeleo mwananchi. Hii ni kutokanana na ujenzi wa
miundombinu rafiki kwa shughuri za uzalishaji mali, kilimo, utalii, na biashara
kwa watanzania wengi.
Kwa
upande wa usafiri wa chini/ardhi, msukumo mkubwa wa Mhe. Rais John Pombe
Magufuli juu ya usimamizi makini wa majukumu ya TANROAD na TARURA umekuwa
chachu ya uboreshwaji wa miundombinu ya barabara nchini hasa ukizingatia miundo
mbinu ya usafirishaji na mawasiliano ni msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi
kote duniani.. Hapa tunaona barabara kuu na za kawaida karibia nchi nzima
zikiwa zimejengwa kwa kiwango cha lami, zikiunganisha makao makuu ya wilaya na
vijiji mbalimbali. Uboreshwaji huo umerahisisha usafirishwaji wa bidhaa na
mazao ya kibiashara kutoka yanakozalishwa kwenda kwenye masoko mbalimbali na
hata kurahisisha/kuongeza ukaribu na mawasiliano zaidi kati ya wananchi vijijini
na makao makuu ya wilaya zao kwa mahitaji ya huduma mbalimbali za kiutumishi na
kiraia. Kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, kwa miaka mingi wamekuwa wahanga
na kupoteza muda wao mwingi wakiwa barabarani kwa ajili ya foleni kubwa za
magari, lakini hivi punde wananchi wameshuhudia ufanisi uliopatikana kwa
kujengwa daraja la Mwl. Nyerere pale Kigamboni na barabara inayopita juu katika
makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere (Mfugale fly over). Hii imepelekea
wananchi kutopoteza tena muda wao mwingi katika shughuri zao za uzalishaji mali
na hata hivyo itakapokamilika “fly over” ya pale Ubungo hivi karibuni na za sehemu
zingine, upanuzi wa barabara ya Morogoro na ujenzi wa barabara ya mwendokasi ya
Mbagala, ndipo tatizo la foleni jijini Dar es Salaam litakapokwisha kabisa na
kuwa historia ya nchi. Kubwa lao katika haya, ni ujenzi wa reli ya treni ya
kisasa, Standard Gauge Railway (SGR) inayoanzia Dar es Salaam hadi Dodoma kwa
awamu ya kwanza na ya pili kuanzia Dodoma hadi Mwanza na Kigoma. Kukamilika kwa
treni hii ya SGR kwa awamu ya kwanza, kutawafanya watanzania kutumia takribani saa
3 tu kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kurahisisha shughuri zote za kiuchumi
kwani watu wataweza kuishi Dodoma na kufanya kazi/biashara zao Dar es Salaam
ambapo kwa usafiri wa basi hutumia si chini ya saa 8 kati ya Dar es Salaam na
Dodoma. Lakini pia SGR itakuwa ni mwarubaini wa usafirishaji wa mamia ya tani
za mizigo inayotoka bandarini na kuelekea mikoani au nchi jirani na kuiletea
serikali biashara na faida kubwa na ya haraka hivyo kukuza uchumi kwa kasi. Huku
kote ni kumlenga mtanzania aweze kufanya shughuri zake za kiuchumi kwa wakati
stahiki, katika mazingira rafiki na hatmaye kuifurahia radha halisi ya nchi
yake sambamba na kujivunia kwa fahari kubwa kuwa mtanzania katika dhana ya
ushindani wa kimaendeleo na nchi zingine za kiafrika, lakini pia kupata huduma
zote za msingi kwa ubora zaidi kwani serikali itakuwa ni yenye pato kubwa na la
uhakika la kuweza kubuni, kuboresha na kusambaza zaidi huduma hizo mfano maji,
elimu, pembejeo n.k.
Kwa
upande wa usafiri wa anga napo moto ni uleule, awamu ya tano imefufua ile tunu
ya taifa iliyofifia kwa nchi kutokuwa na ndege zake yenyewe. Serikali ya awamu
ya tano kupitia pesa zake yenyewe, imeweza kunua ndege 11 za kisasa na za aina
tofauti tofauti na hatimaye kulipa uhai shirika la ndege nchini, ATCL sambamba
na kuipandisha heshima ya nchi yetu kimataifa. Hii pia imeongeza idadi ya
watalii kuja nchini kwani ndege zetu zitakuwa zikienda nchi fulani za ughaibuni
na kuja moja kwa moja nchini pasipo kupitia nchi zingine hivyo kupunguza safari
ndefu na ya kuunga unga kwa watalii kuja nchini. Hili limeenda sambamba na
upanuzi na ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini na kuifanya sekta ya
anga nchini kutengemaa hatmaye kurahisisha usafiri wa haraka n.k. Hii ni fahari
kwa mtanzania.
MWISHO
Kwa
kumalizia ni vyema nigusie umakini na maono ya kweli ya serikali katika suala
zima la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini mfano safari za
holelaholela za nje ya nchi, gharama za uendeshaji wa vikao, uwepo wa
wafanyakazi hewa serikalini, wanafunzi hewa kuanzia shule za misingi hadi vyuo
vikuu na hata ufisadi katika ofisi nyeti za umma. Lakini pia, serikali
imejitahidi kwa kiasi kikubwa sana kudhibiti upotevu mkubwa wa mapato na nyara
za serikali mfano kuufanyia marekebisho usimamizi wa mamlaka ya mapato Tanzania
(TRA), kuijengea nguvu na makali TAKUKURU, kudhibiti ujangiri wa wanyama pori
na ujenzi wa ukuta kuuzunguka mgodi kule Mererani ili kudhibiti utoroshaji wa
madini ya Tanzanite. Upotevu huo wa mapato ulikuwa ukiiletea hasara kubwa nchi
yetu na hatmaye kufifisha jitihada za kuharakisha maendeleo ya watanzania walio
wengi na hata kuzimisha matumaini ya kesho yao sambamba na uzalendo kwa taifa
lao. Pia ukawa ni mzigo mkubwa kwa mlipa
kodi kwani pesa nyingi ilikuwa ikipotea. Hakika awamu ya tano ndani ya miaka
michache hii, imeweza kumulika kila sekta na kuondoa kwa asilimia kubwa uzembe
uliokuwa ukiigharimu nchi na kuirudisha nyuma katika safari ya kujiimarisha
kiuchumi na katika kumkomboa mwananchi. Kwa kufanya hivyo, (kukomesha uzembe
huo), nafuu huja kwa mwananchi wa kawaida ambaye anaitegemea serikali imjengee
mazingira rafiki ya kimiundo mbinu ya usafirishaji na uchukuzi, afya, elimu,
kilimo na kibiashara ili yamrahisishie shughuri zake za kiuchumi ziende vizuri
na kukuza kipato chake na cha familia yake, hatmaye ndio maendeleo ya taifa
zima. Huku ndiko nakokuita kuzigeuza tunu za taifa kuwa mkombozi wa mtanzania
hasa yule wa hali ya chini ili naye si aionje tu, bali ale keki ya taifa na
kuifurahia fahari ya nchi yake hatimaye kuongeza kiwango cha uzalendo kwa taifa
lake. Hakika AWAMU YA TANO YAKOLEZA RADHA YA TANZANIA, mweeeh!!
Mungu ibariki Tanzania!
Mungu ibariki Afrika!
Ameen!
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
REJEA
Jarida la
Nishati-Toleo Na.11 www.nishati.go.tz
TUNATEKELEZA 2020, Video clip. Channel ten TV
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇