Hali nchini Malawi haijatulia hata baada ya Mahakama ya Kikatiba juzi kutupilia mbali ya rufaa ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Arthur Peter Mutharika ya kuzuia uchaguzi mwingine.
Jana waandamanaji walifika katika ofisi za tume ya uchaguzi na kisha kufunga kwa mnyororo ofisi hizo kama njia ya kumlazimisha mwenyekiti wake kujiuzulu baada ya uamuzi huo wa mahakama.
Mamia ya waandamanaji hao walitembea kwa kilomita tano hadi kufika katika ofisi za tume hiyo zilizoko Blantyre, na kufunga geti la kuingilia kwa kutumia mnyororo wenye kutu.
Maelfu ya watu walifanya jambo kama hilo hilo katika jiji la Lilongwe wakimfungia ofisa wa jeshi.
Wiki iliyopita mahakama ilibatilisha matokeo ya uchaguzi ambayo yalishuhudia Mutharika akishinda kwa ushindi mwembamba, ikieleza kuwa yaligubikwa na uvunjifu wa sheria.
Kutokana na hayo mahakama hiyo iliamuru kufanyika kwa uchaguzi mwingine mpya wa urais ndani ya siku 150 pamoja na kufanyika kwa uchunguzi juu ya operesheni zote zinazoendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya nchini humo (MEC).
Hii ni mara ya kwanza kwa matokeo ya urais kufutwa mahakamani kwa misingi ya kisheria nchini Malawi tangu ipate uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1964, na matokeo ya pili kufutwa katika bara la Afrika baada ya yale ya Urais wa Kenya mwaka 2017.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇