Uchunguzi uliofanywa na timu ya wataalamu na madaktari nchini China pamoja na takwimu rasmi zinaonyesha kuwa idadi ya waathirika na vifo vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya Corona, inaendelea kupungua.
Kamisheni ya Afya ya Kitaifa nchini humo imetangaza kuwa, siku ya Jumapili iliyopita zaidi ya watu 5170 walikumbwa na maambukizi ya virusi vya Corona, lakini kiwango hicho kilipungua na kufikia 5070 siku ya Jumatatu. Aidha siku ya Jumanne idadi hiyo ilipungua na kufikia watu 3900. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu siku ya Jumanne kiwango hicho kimeendelea kusalia chini ya kesi 4000, ambapo wataalamu wa kitiba nchini China wameielezea hali hiyo kuwa ni alama ya mafanikio ya kuwaweka karantini waathirika na kuzuia ongezeko la maambukizi ya virusi hivyo.
Aidha katika siku za mwanzoni kulipoanza kuenea virusi hivyo, idadi ya vifo ilikuwa ikiongezeka mara mbili katika hali ambayo hivi sasa idadi ya vifo imeendelea kupungua kati ya asilimia 17 hadi 22 ikilinganishwa na siku za nyuma. Katika ripoti ya kamisheni ya Afya ya Kitaifa nchini China kumeelezwa kwamba mwanzoni mwa wiki karibu waathirika 600 wa virusi hivyo wametibiwa na kwamba idadi hiyo imepanda na kufikia watu 1208. Song Shouli, Msemaji wa Kamisheni ya Afya ya China amesema kuwa moja ya mafanikio mengine ni kutambuliwa haraka waathirika. Hata hivyo kamisheni hiyo imesema kuwa hadi sasa jumla ya watu 560 wamepoteza maisha kutokana na virusi vya Corona nchini humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇